Habari za Punde

KATIBU MKUU NISHATI AFANYA MAZUNGUMZO NA MWAKILISHI MKAZI WA IMF

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati,  Mhandisi Felchesmi Mramba (wa kwanza,kushoto),  na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) nchini Tanzania, Jens Reinke  (wa Pili kutoka kulia) wakiwa katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma tarehe 2 Juni, 2023. Wengine ni watendaji kutoka Wizara ya Nishati, TPDC na IMF
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati,  Mhandisi Felchesmi Mramba (wa tatu kushoto) na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) nchini Tanzania, Jens Reinke  (wa nne kutoka kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa Wizara ya Nishati, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na IMF baada ya  kikao kilichofanyika jijini Dodoma

Na.Teresia Mhagama na Godfrey Mwemezi

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) nchini Tanzania, Jens Reinke  na watendaji wengine wa Shirika hilo  ambapo kikao hicho kililenga kujadili masuala mbalimbali ikiwemo mwenendo wa uchumi, utekelezaji wa bajeti, mipango ya maendeleo ya nchi na program ya ufadhili  wa miradi (ECF).

Kikao hicho kimefanyika jijini Dodoma tarehe 2 Juni, 2023 na kuhudhuriwa na Kamishna wa umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, Kamishna wa Petroli na Gesi, Michael Mjinja, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mussa Makame na watendaji wengine kutoka Wizara ya Nishati na TPDC.

Katika kikao hicho, Mhandisi Mramba aliwaeleza watendaji hao kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali itakayopelekea nchi kuwa na umeme wa kutosha na uhakika ukiwemo mradi wa Julius Nyerere (JNHPP) utakaozalisha megawati 2,115, unaotarajiwa kukamilika mwezi Juni 2024.

Katibu Mkuu pia amewaeleza watendaji hao kuhusu Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia (LNG) ambao ameeleza kuwa, majadiliano yake ya Mkataba wa Nchi Hodhi (HGA) na Mkataba wa Uzalishaji na Ugawanywaji Mapato (PSA) kati ya Timu ya Majadiliano ya Serikali na Wawekezaji
katika Vitalu husika yamekamilika.

Vilevile, amewaeleza watendaji wa IMF kuhusu hatua zinazoendelea kufanyika katika  mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) ambao alisema kuwa kwa ujumla unaendelea vizuri.

Aidha, amewaeleza watendaji hao kuhusu hatua mbalimbali ambazo Serikali imezifanya hadi sasa za kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili ifikapo mwaka 2033, asilimia 80 ya wanachi wawe wanatumia nishati hiyo.

Katibu Mkuu pia ametanabaisha kuhusu vyanzo vya nishati jadidifu vilivyopo nchini ikiwemo Jua na Upepo ambavyo amesema kuwa, wawekezaji mbalimbali wanaweza kuvitumia kuzalisha umeme.

Katibu Mkuu ameishukuru IMF kwa kutoa fedha shilingi Bilioni 200 kupitia mpango wa ECF kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kuimarisha gridi ya Taifa pamoja na kupeleka umeme katika vitongoji vya mikoa ya Songwe na Kigoma.

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa IMF nchini Tanzania, Jens Reinke amemshukuru Katibu Mkuu kwa kupata taarifa hizo muhimu ambazo wao kama
wadau zinawasaidia katika kufahamu mwelekeo wa Serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.