Habari za Punde

SERIKALI KUSAINI MKATABA WA UKAGUZI WA MIAMALA YA KIMATAIFA

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) akijibu swali bungeni, jijini Dodoma.

Na. Peter Haule, WFM, Dodoma

Serikali inatarajia kusaini mkataba ujulikanao kama (Multilateral Convention on Mutual Administrative Assistance in Tax Matters) ambao utaiwezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupata taarifa mbalimbali kutoka nchi 146 duniani ambazo zitasaidia katika kuongeza ufanisi wa ukaguzi wa miamala ya kimataifa.

 

Hayo yamebainishwa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande, wakati akijibu swali la Mbunge wa Kisesa, Mhe. Luhaga Mpina, aliyetaka kujua kiwango ambacho Serikali imejiimarisha kukagua miamala ya uhamishaji wa bei ya mauziano ya bidhaa na huduma baina ya kampuni za kimataifa.

 

Mhe. Chande alisema kuwa kwa kuzingatia vihatarishi vilivyopo kwenye miamala husika, Serikali imekua ikichukua hatua mbalimbali zinazolenga kuimarisha udhibiti na kuzuia upotevu wa mapato ikiwemo ya kuanzisha kitengo maalum cha usimamizi wa kodi za kimataifa.

 

“Mwaka 2011 Serikali ilianzisha kitengo maalum cha usimamizi wa kodi za kimataifa ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania ili kuimarisha udhibiti na upotevu wa mapato”, alieleza Mhe. Chande.

 

Alisema hatua nyingine zilizochukuliwa ni pamoja na kuandaa na kusimamia utekelezaji wa kanuni na miongozo kuhusu ukaguzi wa kodi kwenye kampuni zenye uhusiano, pia Mamlaka ya Mapato Tanzania imenunua kanzidata ya Orbis kwa ajili ya kupata taarifa za kusaidia kufananisha bei za miamala ya kimataifa ili zisaidie katika ukaguzi wa kampuni zilizopo nchini.

 

Aidha alieleza kuwa Tanzania imejiunga na jukwaa la kimataifa la ubadilishanaji taarifa za kikodi ili kuhakikisha kuwa inajenga uwezo wa kubadilishana taarifa za kikodi na nchi nyingine.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.