Habari za Punde

Waziri Mkuu Mhe.Majaliwa Aagiza Uchunguzi Zaidi Ufanyike Kisa cha Binti Kupotea ShuleniMbeya

 

 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera na Kamati ya Usalama ya Mkoa huo wafanye uchunguzi zaidi na kwa haraka kuhusiana na tukio la kupotea kwa binti Esther Noah Mwanyiru ambaye alikuwa akisoma shule ya sekondari ya Panda Hill mkoani humo.

 

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Juni 22, 2023) baada ya kupokea clip yenye maelezo ya mzazi wa binti huyo ambaye alikuwa akisoma kidato cha tano, tahsusi ya PCB kwenye shule hiyo.

 

Katika clip hiyo, Mama yake Esther anadai kwamba yeye na mume wake waliitwa na uongozi wa shule hiyo na kujulishwa kwamba Esther hajaonekana tangu asubuhi ya tarehe 18 Mei, 2023 na kwamba hadi sasa zimepita siku zaidi ya 20 wamekuwa wakimtafuta binti yao kila mahali lakini hakuna dalili za kumpata.

 

Mama Esther anadai kuwa Esther aliacha ujumbe wa maandishi akiwaaga rafiki zake na kuomba Mwalimu Jimmy aache kuwafanyia wanafunzi wengine kitendo alichomfayia yeye kwani kimesababisha maisha yake kuwa magumu.

 

“Naomba umfikishie salamu Mwalimu Jimmy, mwambie ameyafanya maisha yangu kuwa magumu sana hapa shuleni. Asiendelee kuwafanyia wanafunzi wengine kama alivyoyafanya maisha yangu mimi kuwa magumu,” alisema mama yake Esther akisoma sehemu ya ujumbe huo.

 

(mwisho)

 

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

S. L. P. 980,

41193 – DODOMA

ALHAMISI, JUNI 22, 2023.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.