RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi, amekutana na Ujumbe kutoka Shirika la Umoja wa
Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kujadili masuala mbalimbali kuhusu
utunzwaji wa hifadhi ya kimataifa ya Mji Mkongwe.
Dk. Mwinyi alikutana na ujumbe huo Ikulu,
Zanzibar ukiambata na Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Simai Mohammed Said
pamoja na maafisa wa Wizara hiyo.
Alisema, licha ya maendeleo makubwa
yaliyofikiwa na Zanzibar bado Urithi wa hifadhi ya kimataifa ya Mji Mkongwe
unaendelea kulindwa na kuenziwa kwa mujibu wa taratibu na kanuni zilizowekwa.
Rais Dk. Mwinyi aliueleza ujumbe huo kwamba,
Selikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukua hatua mbalimbali za kuutunza urithi
ikiwemo kuondosha msongamano wa maegesho ya vyombo vya moto kwenye maeneo yote
ya Mji Mkonge wa Zanzibar, ili kuenzi haiba ya mji huo kuendelea kuwa kivutio
mashuhuri cha watalii na wageni wanaoutembelea mji huo.
Aidha, alisema katika kutekeleza hatua hiyo,
Serikali imeamua kujenga maegesho ya vyombo vya moto eneo la Darajani ikiwa
njia mbadala ya kuondosha msongamano wa magari kwenye maegesho ya Mji Mkongwe.
Pia Dk. Mwinyi, aliueleza Ujumbe huo kwamba
hatua nyengine iliyochukuliwa na Serikali ni kushirikiana na sekta binafsi
kuutunza Urithi huo hasa kuyaendeleza majengo yaliyochakaa kwa kuyakarabati kwa
mujibu wa kanuni na taratibu za kuyaenzi majengo hayo kuyarudisha kwenye
uhalisia wake.
Alisema,
Serikali inasimamia kwa karibu na kuhakikisha thamani na mali zote za asili
zilizokuwemo kwenye majengo hayo zinarudishwa sehemu husika baada ya ukarabati.
Akizungumzia jengo la Beit el Ajaaib na la
People’s Palace, Rais Dk. Mwinyi aliueleza ujumbe wa UNESCO
kwamba Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano na Serikali ya Oman wanaendelea
kusimamia ujenzi wa majengo hayo.
Hata hivyo, Dk. Mwinyi alieleza Beit el Ajaaib
na la People’s Palace ni alama muhimu inayoitambulisha Zanzibar duniani kote.
Nao, Ujumbe huo wa UNESCO, uliitaka Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar, kuendelea kuuenzi na kuutunza urithi huo ili
kuunusuru na athari za mabadiliko ya teknolojia ikiwemo kukua kwa maendeleo ya nyanja
mbalimbali nchini ambayo kwa namna moja ama nyengine itakua sababu ya kubadili
mandhari halisi na mwonekano wa mji huo.
IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment