Wadau wa mafuta na gesi wakifuatilia Kongamano la Kimataifa la Sekta ya Nishati na Viwanda Zanzibar linalofanyika tarehe 26 na 27, Julai, 2023 mjini Unguja, Zanzibar
Mhandisi Mkuu eneo la Mafuta na Gesi wa Wizara ya Nishati Mha. Joyce Kisamo akichangia mada wakati wa Kongamano la Kimataifa la Sekta ya Nishati na Viwanda Zanzibar linalofanyika tarehe 26 na 27, Julai, 2023 mjini Unguja, Zanzibar.
*Awataka Wazanzibari kuvuta Subira wakati Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inafanyia kazi utafutaji wa mafuta na Gesi.
Na Dorina G. Makaya- Zanzibar
Waziri wa Nishati January Makamba, amewasihi viongozi kutoa taarifa sahihi kwa wananchi na kuwapa matumaini sahihi kuhusu uwezekano wa upatikanaji wa rasilimali za Mafuta na Gesi ili kuepuka taharuki inayoweza kutokea kwa wananchi pale itakapotokea kukosekana kwa rasilimali wanazotarajia.
Hayo yamesemwa tarehe 26
Julai, 2023 Mjini Unguja, Zanzibar, na Waziri wa Nishati, January Makamba
wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa la Sekta ya Nishati na Viwanda Zanzibar
linalojulikana kwa Lugha ya Kiingereza (Zanzibar Energy and Industrial Summit
-ZEIS)
Amesema, upatikanaji wa Mafuta
na Gesi ni zoezi lenye mchakato mrefu kuanzia taratibu za majadiliano na
makubaliano, leseni ya utafutaji hadi kufikia upatikanaji wa mafuta na
linahitaji muda na kuwataka Wazanzibari kuvuta Subira wakati Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inalifanyia
kazi jambo hili.
Waziri Makamba ameeleza
kuwa, katika Kongamano hilo, Tanzania Bara imeelezea walichojifunza Bara kuhusu
Majadiliano ya kufikia makubaliano ya utafutaji na uchimbaji wa Gesi na Mafuta
na mambo ya kutahadhari na pia subira inayotakiwa, matayarisho na utayari wa Serikali,
Rasilimaliwatu, na mfumo mzima wa Serikali wa kusimamia utekelezaji.
Waziri Makamba ameeleza zaidi
kuwa, mkutano huo pia umezungumzia juu ya umuhimu wa Sekta ya Mafuta na Gesi
kutoingiliwa na siasa kwa sababu wawekezaji huwa wanatazama kama kuna muafaka
katika nchi husika kuhusu namna wanavyotaka rasimilimali zitumike.
Amesema, endapo ikionekana
kwa wawekezaji kuwa uwekezaji wakati mwingine utatumika kama sehemu ya siasa,
basi mara nyingi inakuwa ni vigumu kuwekeza katika eneo hilo.
Aidha, Waziri Makamba amesisitiza
kuwa, uwekezaji wa Gesi na Mafuta una gharama kubwa na hauna uhakika sana, kwa
sababa mwekezaji anaweza kutumia fedha nyingi sana kutafuta mafuta na Gesi na asiyapate
hivyo muundo na mfumo wa makubaliano ni lazima uzingatie uhalisia huo ya kwamba
ni teknolojia ya juu, ni mtaji mkubwa vinavyotumika na na upatikanaji wake si
wa uhakika.
Waziri Makamba amesema uwepo
wa Taasisi kutoka Tanzania Bara, zikiwemo, Shirika la Maendeleo ya Petroli
Tanzania (TPDC), Mamlaka ya udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA),
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati (EWURA) katika Kongamano hilo,
unaelezea na kunaonyesha ushirikiano wa hali ya juu baina ya Pande mbili za
Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar kwenye eneo la Nishati.
Amesema, katika Kongamano
hilo, wameeleza kwa ujumla nafasi ya Nishati katika maendeleo ya nchi, umuhimu
wake na wamezunguzia pia kwa undani kuhusu Mafuta na Gesi, kwani Zanzibar tangu
2016 imetunga Sheria yake ya Gesi na Mafuta hivyo kumekuwa na matumaini makubwa
kuhusu upatikanaji, utafutaji na utunzaji wa Gesi na Mafuta na mchango wa Sekta
ya Mafuta na Gesi kwa Maendeleo ya Zanzibar na kuwa, ni jambo jema kwamba kuna
dalili na viashiria vya upatikanaji wa
gesi.
Amesema, awali, suala hilo
lilikuwa linasimamiwa na Serikali ya Muungano, na kuwa mwaka 2022, Waziri wa
Nishati, January Makamba, aliwakabadhi Wizara ya Nishati Zanzibar taarifa zote
ambazo zinahusu upande wa Zanzibar ili iwe rahisi kwa Zanzibar kukaribisha
wawekezaji ili kuweza katika kutafuta mafuta na Gesi.
Waziri makamba ameeleza
zaidi kuwa, Zanzibar ikipata Gesi, wakati huo Tanzania Bara ina Gesi, itakuwa
ni jambo bora kabisa na litabadilisha uchumi na maisha ya watu wa nchi husika.
Amesema ni muhimu kuharakisha
uwekezaji kutokana na mwelekeo wa dunia kwenye Nishati mpya ambazo ni jadidifu
hivyo, ucheleweshaji wa uwekezaji kwenye Nishati za mafuta na Gesi kunaweza
kupelekea changamoto ya upatikanaji wa wawekezaji kwa wakati.
Akijibu swali, ni kwa kiasi
gani Zanzibar inahitaji kuelekea katika uwekekezaji katika Bahari, Waziri
Makamba amesema, maeneo ya Bahari yanayomilikiwa na Tanzania na nchi nyingine
za Afrika yaliyofanyiwa utafiti, ni asilimia ndogo sana iliyofanyiwa utafiti ikilinganishwa
na maeneo mengine duniani.
Naye Waziri wa Uchumi wa
Buluu na Uvuvi Mhe. Suleiman Masoud Makame, amesema, moja ya Azma ya mkutano
huo ni kuitangaza Zanzibar kwenye suala zima la Mafuta na Gesi na kuwa mkutano
huo unakwenda sambamba na utangazaji wa maeneo ya uwekezaji wa mafuta na Gesi
ambayo yako tayari kwa uwekezaji.
Amesema, Maelekezo ya Rais
wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni Kwenda kwa kasi zaidi na jitihada zinafanyika
katika kulitimiza hili ili wawekezaji
wajitokeze kuwekeza katika utafutaji wa Mafuta na Gesi na tayari kampuni tano
zimeonyesha nia ya kuja kufanya uwekezaji katika eneo hilo.
Ameongeza kuwa, Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar itahakikisha kuwa Kampuni watakayofanya nayo kazi ni Kampuni yenye uwezo.
Kongamano hilo la siku mbili la Kimataifa linalofanyika tarehe 26 na 27 Julai, 2023, la Sekta ya Nishati na Viwanda Zanzibar, limeshirikisha zaidi ya nchi tisa zikiwemo Marekani, Uingereza, Ujerumani, China, Uturuki, Afrika ya Kusini na Bulgaria.
No comments:
Post a Comment