Habari za Punde

Waziri Mhe.Simbachawene Awataka Watendaji Serikalini Kutoa Fursa kwa Watumishi Wanaowaongoza Ili Waoneshe Uwezo Wao Kiutendaji

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akisalimiana na Menejimenti ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) jijini Dar es Salaam kabla ya kuzungumza nao kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza na Menejimenti ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) wakati wa  ziara yake ya kikazi  katika Chuo hicho jijini Dar es Salaam  ikiwa ni mwendelezo wa kuzungumza na Watumishi kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao.
                                                                                                                   

Na. Lusungu Helela-Dar es Salaam.                                                                              Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala           Bora, Mhe. George Simbachawene amewataka Watendaji Serikalini kuwapa             nafasi watumishi walio chini yao ili waweze kuonesha uwezo wao kiutendaji kwa lengo la kuchagiza dhana ya utawala bora badala ya kuhodhi kila kitu.

 

Mhe. Simbachawene ametoa kauli hiyo  wakati wa ziara yake ya kikazi  katika Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) jijini Dar es Salaam ikiwa ni mwendelezo wa kuzungumza na watumishi kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao.

 

‘’Ukiwa Kiongozi, hakikisha unaacha alama katika eneo unaloliongoza kwa kuwaandaa watumishi kiutendaji ili unapostaafu au kuondoka eneo hilo kwa taratibu nyingine, basi halitatetereka huku heshima yako ikibaki kama Kiongozi wa mfano katika mioyo ya watu’’ amesisitiza Mhe. Simbachawene.

 

Mhe. Simbachawene amesema anatamani kuona Taasisi zote za Serikali zinakuwa na mtazamo huo wa kutoa nafasi kwa Watumishi wao huku akisisitiza kuwa watumishi wenye uwezo wasifichwe kwa hofu ya wenye mamlaka kupokwa nafasi zao kwani serikali bado ina kazi nyingi sana.

 

Katika hatua nyingine, Mhe. Simbachawene ameonya tabia ya baadhi ya Watendaji katika Taasisi za Serikali kukaimisha nafasi za uongozi kwa watumishi wasio na sifa wakati wanaostahili kupewa nafasi hizo wapo.

 

Akizungumza na watumishi wa Wakala ya Ndege za Serikali, Mhe. Simbachawene amesema watumishi wanaokaimishwa katika nafasi mbalimbali za uongozi wanapaswa kuwa na sifa za kushika nafasi hizo ili kuirahisishia Ofisi ya Rais – UTUMISHI mchakato wa kuwathibitisha.

 

"Naomba niwaambie ukweli, ukimkaimisha Mtumishi ambaye hana sifa, inatuwia vigumu kumthibitisha kwani anakuwa hana vigezo kwenye nafasi hiyo" amesisitiza Mhe. Simbachawene. 

 

Aidha, Waziri Simbachawene ameelekeza kufanyiwa kazi kwa changamoto mbalimbali zinazokwamisha utendaji kazi wa watumishi katika maeneo yao ya kazi ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi.

 

Kwa upande wao, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi pamoja na Katibu Mkuu Ikulu, Bw. Mululi Mahendeka wakiongea kwa nyakati tofauti wamemshukuru Waziri Simbachawene kwa kuweka utaratibu wa kuwatembelea watumishi kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili na kuelekeza zifanyiwe kazi kwa maslahi mapana ya taifa.

 

Viongozi hao wameahidi kuzifanyia kazi changamoto za watumishi ambapo wamesema tayari nyingine zimeshaanza kufanyiwa kazi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.