Na mwandishi wetu Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dk Hussein Ali Mwinyi ameipongeza Benki ya Absa Tanzania, kwa kudhamini matembezi na mbio fupi zenye lengo la kuchangia vifaa tiba kwa uzazi salama wa mama na mtoto.
Akizungumza mara baada ya matembezi hayo yaliyoitwa ‘Wogging Marathon 2023’ yaliyoandaliwa na Shirika la Amref kwa kushirikiana na Serikali ya Zanzibar chini ya udhamini wa Absa, Rais Dk. Mwinyi alisema anatambua na kuthamini udhamini mkubwa wa Benki ya Absa pamoja na waandaaji wa matembezi hayo.
“Kwa niaba ya serikali natoa shukurani kwa Benki ya Absa Tanzania na kuwataka waendelee kutupa ushirikiano katika kuhakikisha tunafanikiwa katika malengo yetu ya kupunguza idadi ya vifo vya mama wajawazito na watoto vinavyotokana na uzazi.
“Nimefurahi kusikia kuwa kampeni hii ni ya miaka mitatu na ilianza tokea mwaka jana ikiwa na lengo la kukusanya shilingi bilioni moja huku taarifa nilizonazo zikionyesha kuwa hadi sasa ahadi za jumla ya shs milioni 792 zimetolewa huku kilichopatikana ni shs milioni 557”, alisema mheshimiwa rais.
Akizungumza mara baada ya matembezi hayo yaliyokuwa ya umbali wa kilomita tano na kumi, ambapo pia alishiriki matembezi hayo akiwa na mkewe Mama Mariam Mwinyi, viongozi kisiasa, kiserikali, taasisi za umma na binafsi na wananchi ndani ya kisiwa hicho na wageni wengine kutoka nje ya Zanzibar alisema, kampeni ya Uzazi Salama inaunga mkono juhudi za serikali katika kupunguza na kuepusha vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga kutokana na ukweli kuwa bado takwimu za vifo hivyo bado vipo juu.
“Takwimu zinaonyesha vifo vya kina mama 134 kati ya vizazi hai 100 kwa mwaka na vifo 28 vya watoto wachanga kati ya vizazi hai 1,000 kwa mujibu wa takwimu za Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania (TDHS) za mwaka 2017”, alisema Rais Mwinyi akiongeza kuwa kiwango hicho kinasababishwa na changamoto mbalimbali zikiwemo upungufu wa vifaa tiba, uhaba wa wahudumu pamoja na kukosekana kwa dawa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa, Bwana Obedi Laiser alisema kampeni hii inaenda sambamba na dhumuni kuu la benki ya Absa ambalo ni kuiwezesha Afrika ya kesho, pamoja, mtu mmoja baada ya mwengine katika kuiwezesha jamii yenye afya bora na mustakabali mzuri
“Sisi kama Absa tunatambua juhudi kubwa zinazofanywa na serikali ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya pamoja na mashirika kama Amref katika kuleta mabadiliko katika jamii hususan katika sula zima la afya ya mama wajawazito na mtoto kwani afya ya mtoto ni msingi wa Taifa la watu wa sasa na wa kesho.
“Tutaendelea kushirikiana na serikali za Zanzibar katika jitihada zake za kuwaletea wananchi wake maendeleo, tuna malengo makubwa ya kibiashara hapa Zanzibar katika kutanua huduma zetu za kibenki, na tutaendelea pia kushirikiana na Amref katika jitihada hizi za kuokoa maisha ya mama na mtoto japo hii ni mara yetu ya kwanza”, alisema Bwana Laiser.
Matembezi na mbio fupi za Amref wogging ni hafla la kila mwaka inayoandaliwa na shirika hilo kwa ushirikiano na serikali huku yakiwezeshwa kwa udhamini wa taasisi mbalimbali, wananchi pamoja na wadau wengine yakiwa na lengo kutafutu suluhu za changamoto zinazosababisha vifo vya wamama wajawazito na watoto wachanga nchini.
No comments:
Post a Comment