Habari za Punde

Wananchi Wahamasishwa Utalii wa Ndani wa Wanyamapori

Afisa Utalii Mamlaka ya Usimamizi wa wamyama pori Tanzania (TAWA ) Ndg.Lusajo Nsweve  Akizungumza na Waandishi wa Habari  wakati akihamasisha utalii wa wamyama pori hai huko viwanja vya Kashangae Paje Mkoa wa Kusini Unguja katika Tamasha la Kizimkazi linalotarajiwa  kuzinduliwa kesho Agosti 26,2023 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi.

Muhifadhi wa Wanyama Pori Mamlaka ya Usimamizi wa wamyama pori Tanzania (TAWA) Ndg.Ashraf Shemoka  akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusiana na wanyama pori wanaopatikana katika hifadhi ya wanyama pori ya Taifa wakati walipotembelea Tamasha la Kizimkazi linalotarajiwa kuzinduliwa rasmin kesho Agosti 26, 2023 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi katika viwanja vya mpira Kashangae Paje Mkoa wa Kusini Unguja.
PICHA NA FAUZIA MUSSA-MAELEZO ZANZIBAR 

Na Rahima Mohamed, Asya Khamis Maelezo 25/8/2023

Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama Pori Tanzania (TAWA) imewataka wananchi wa Zanzibar kujitokeza kwa wingi katika ufunguzi wa Tamasha la Kizimkazi ili kujionea wanyama pori mbalimbali kutoka Tanzania Bara.

 

Hayo yamesemwa na Afisa Utalii kutoka Mamlaka ya usimamizi wa wanyama Pori Tanzania (TAWA) Lusanjo Nsweve wakati akizungumza na Waandishi wa habari  huko Paje Mkoa wa Kusini Unguja.

 

Amesema  wanyama hao watakuepo kuanzia leo hadi tarehe 31 na wananchi  watajionea wanyama hao mubashara ikiwemo nungunungu, simba, chui, fisi, pundamilia, ndege mbalimbali na kupata elimu pamoja na kujua tabia za wanyama hao.

 

Afisa Lusanjo  amesema Wananchi wanaweza kupata elimu ya ufugaji wanyama pori  kwa kutumia Mbuga au mashamba Ili kuongeza pato la taifa Nchini.

 

Aidha amesema sekta ya  utalii ni  muhimu sana katika nchi yetu  hivyo kuwepo kwa wanyama hao Zanzibar kutasaidia kuvitangaza vivutio mbalimbali nchini ili wanachi na  wageni wajionee kwa macho yao na kutembelea vivutio hivyo.

 

Vilevile afisa huyo amesema kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutumia Tamasha hilo kutasaidia kuhamasisha wenyeji na wageni kujionea vivutio hivyo  kwa ajili ya kuutangaza utalii na kuongeza wageni.

 

Hivyo amewasisitiza na kuwatoa wasiwasi wananchi watakaotembelea maonesho hayo kwani wanyama hao wapo katika hali nzuri na wametunzwa kitaalamu na kuekwa kwenye vizimba ambavyo viko imara kabisa.

 

Nao wakaazi wa Paje wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea fursa za maonesho mbalimbali ikiwemo wanyama pori ikiwa ni kivutio cha utalii.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.