Habari za Punde

TAMWA-Zanzibar Yataka Uwazi na Mawasiliano Yaendelee Kwenye Kesi za Ukatili.

 

CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kinaziomba taasisi zinazosimamia masuala ya sheria na upatikanaji wa haki likiwemo Jeshi la Polisi, Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na Mahakama kuendeleza uwazi na mawasiliano katika kushughulikia kesi za ukatili wa kijinsia ikiwemo mauaji.


Hivi karibuni Mahakama Kuu Zanzibar ilitoa taarifa kuwa imemuhukumu mshitakiwa Haji Jaha Issa (37) kunyongwa hadi kufa kwa kosa la kumuua kwa makusudi Hajra Abdallah Abdallah (21) ambapo alimchoma kisu kifuani, ubavuni na tumboni.


Taarifa hiyo ilitaja kuwa hukumu hiyo ilitolewa na Jaji Rabia Hussein Mohammed ambaye aliridhishwa na ushahidi uliotolewa katika mauaji hayo yaliyofanyika februari 26, 2020 huko Paje, Mkoa wa kusini Unguja.


TAMWA,ZNZ inaamini kwamba uwazi na utoaji taarifa kwa Mahakama ni msingi mzuri wa utawala bora na kwamba itaongeza imani kwa wananchi katika kutegemea hukumu za vyombo vya sheria na pia kupunguza kiwango cha uhalifu kwa vile kitawatisha wanaotaka kutenda makosa hayo. 


Hivyo, TAMWA, ZNZ inategemea kuwa Mahakama pamoja na vyombo vingine vya sheria vitaweka wazi taarifa zake kuhusu mashitaka na hukumu ili kufikia matakwa hayo ya nchi na ya kidunia.


Ni aula pia kwa taasisi hizo kutoa taarifa za kila mwezi kuhusiana na mwenendo wa kesi na kueleza mafanikio na changamoto zake na kuweka mifumo ya kuripoti malalamiko.


Kwa mujibu wa rekodi ya TAMWA ZNZ, jumla ya wanawake 19 na watoto wanne (4) wameuawa katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar tokea mwaka 2016 hadi Mei 2023, ambapo mwezi mei mwaka huu wasichana wawili Laura Msemwa (23) na Khairat Juma Bakari (28) waliuwawa kikatili huko Bububu Kijichi na Mbuzini Wilaya ya Maghari “A” Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.


Tunaomba pia Mahakama na taasisi nyengine husika kuendelea kutoa taarifa za kesi zilizosalia na hivyo kuongeza amani na ustawi kwa maisha ya wanawake na watoto ambao mara nyingi ndio wanaoathirika katika vitendo hivi vya ukatili wa kijinsia. 


TAMWA ZNZ inatoa wito kwa jamii kuendelea kushirikiana na mihimili hii muhimu ili kuharakisha na kufanikisha uchunguzi wa makosa ya kihalifu na hatimae haki itendeke.

Dkt. Mzuri Issa,

Mkurugenzi,
TAMWA ZNZ.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.