Habari za Punde

Kinana : Viongozi Serikalini Fuateni Nyayo za Rais Mhe. Simia Kuheshimu Sheria,Kanuni Mnapochukua Hatua Dhidi ya Watendaji

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa Komred AbdulRahman Kinana, Akizungumza na Viongozi na Wanachama wa CCM Mara Baada ya kuzindua Ofisi za CCM Wilaya ya Bukombe Mkoani Geita

Na Mwandishi Wetu

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana ametaka viongozi na watenaji serikalini kuzingatia kanuni, sheria, utaratibu na Katiba wanapowakosoa watendaji.


Amesema ni vyema wakajifunza kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye pamoja na kuwa na uwezo na mamaka lakini hajawahi kusimama hadharani na kuvunja haki ya utu wa mtu hususan watendaji katika ngazi mbalimbali.


Kinana aliyasema hayo jana Ushirombo, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita alipokuwa akizungumza na wanachama wa CCM, viongozi na wananchi alipofungua jengo la ofisi za CCM la wlaya hiyo.


“Nataka kufafanua hili ambalo nimezungumza katika Mkutano Mkuu hapa Bukombe, ni kwamba viongozi wasimamie watendaji serikalini, wasimamie sheria, kanuni na utaratibu lakini si vizuri kuwasema hadharani na kuwafedhehesha watendaji wa serikali.


“Mfano mzuri wa kuigwa ni wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwani hatujawahi kuona akisimama hadharani akmfedhehesha mtendaji serikalini, kwa sababu yeye ni muumini wa utawala bora, unaozingatia katiba, sheria, kanuni na taratibu,” alisema.


Kinana alsisitiza watendaji wote wa serikali wanasimamiwa na kanuni, sheria, katiba na utendaji serikalini.


Pia, alieleza kuwa watendaji hao wanasimamiwa na tume mbalimbali zinazosimamia maadili ya utendaji pamoja na nidhamu serikalini, hivyo ni vizuri kutumia utaratibu huo.


“Ninyi wenyewe mmeona mfano mzuri wa Rais, tuige huu mfano, Rais hajawaji kusimama hadharani hata siku moja akamfukuza mtumishi kazi kwa kuwa anaelewa utararibu na amekuwa akizingatia utaratibu huo, tunawataka viongozi na watendaji serikalini kuzingatia utararibu hizo.


“Mfano mwingine naweza nikawapa kuna ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa kuzingatia ripoti ya CAG Rais anauwezo wa kumfukuza mtu yeyote wakati wowote kwa sababu anazozijua yeye,” alieleza.


Kwa mujibu wa Kinana, Rais Samia hafanyi hivyo bali husubiri utaratibu na kanuni zifuatwe kwa sababu anaweza kumfukuza au kumsema mtu hadharani lakini baadaye ikabainika hana kosa “sasa unamuombaje radhi.”


Aliwataka viongozi kuurudisha utaratibu wa kuzingatia utawala bora, kuheshimu sheria, kwani hata Katiba inasema kwamba utu wa mtu ni lazima uheshimiwe na kwamba kwa kuzingatia hilo Rais Dk. Samia anaonesha mfano kwa vitendo.



Aidha alimpongeza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko (Mbunge wa Bukombe)  kwa kubuni na kuleta mawazo hayo ya ujenzi ambayo yalienda Kamati ya Siasa na Halmashauri Kuu na baadaye Wanachama na hivyo  uamuzi wa kujenga majengo hayo ulifanyika.


Kutokana na ujenzi wa majengo ya CCM, Bukombe kumfurahisha Komredi Kinana,  ameitaka CCM, Mkoa wa Dar es Salaam kujenga Ofisi za kisasa za CCM katika Wilaya zake kama ilivyo Bukombe.


Alisema  WanaCCM nchi nzima wana wajibu wa kuhakikisha kuwa, Ofisi wanazojenga na kumbi zinafanana na heshima na hadhi ya ukubwa wa CCM kama ambavyo Bukombe walivyotoa heshima hiyo kwa Chama cha Mapinduzi.


Aidha, Kinana amepongeza umoja na mshikamano ulioko wilayani Bukombe pamoja na Mkoa wa Geita kwa ujumla na kueleza kuwa wao ni Walimu wazuri wa Kusema na Kutenda hivyo atawatuma viongozi wa Chama wa Mikoa na Wilaya  kutoka maeneo mbalimbali nchini, waende Bukombe kujifunza mfano wa kuimarisha Chama Kitaasisi na kujitegemea.



MSISITIZO UTEKELEZAJI


ILANI UPANDE WA CHAMA


Kuhusu ujenzi wa ofisi za CCM za pamoja na majengo ya kitegauchumi katika ngazi ya kata na matawi, Kinana alisema ni muhimu kwa kuwa ujenzi wake unatekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025.


“Ilani ya Uchaguzi ya CCM Chama Cha Mapinduzi ambayo tumekuwa tikiitoa kuna sehemu inazungumza juu ya Chama , Ilani hiyo inazungumza mambo yote, elimu, afya, miundombinu, utawala bora na kadhalika.


“Katika Ilani ya 2020 - 2025 sehemu ya 10, Ibara ya 246 imeweka mkazo kwenye shughuli zinazohusiana na Chama, nayo inasisitiza juu ya kusimamia maadili, nidhamu katika Chama, kusimamia mafunzo ya Chama na kukijenga katika misingi ya kuimarisha taasisi zake (jumuiya) kwa kujenga ofisi za Chama.


Pia, alisema ni lazima Chama kujenga uwezo wa kujitegemea na Bukombe wameonyesha mfano kwa vitendo kuimarisha juhudi za kujitegemeam hivyo alihimiza CCM kote nchini kuzingatie maagizo hayo ya Ilani kwamba ni lazima ibara hiyo itekelezwe kwa vitendo.


NAIBU WAZIRI MKUU


Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge wa Bukombe, Mhe. Dkt. Doto Biteko alimshukuru Makamu Mwenyekiti wa CCM (TZ) Bara, Komredi Abdulrahman Kinana kwa  heshima aliyowapa CCM Bukombe ya kuzindua Majengo ya Ofisi.


Alisema wadau mbalimbali waliochangia katika ujenzi wa majengo hayo wakiwemo WanaCCM wenyewe ndani ya Wilaya ya Bukombe hasa Vijana wa CCM walioshiriki shughuli za ujenzi kwa kujitolea, wananchi wa makundi mbalimbali, baadhi ya Wabunge na viongozi wa Serikali.  


Alisema kuwa, mradi unaofuata  utahusisha makazi ya Watumishi wa CCM, wakiwemo Makatibu wa Chama ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi.


Alitoa mwito  kwa wananchi kuwa na umoja na kueleza kuwa nchi haiwezi kufanikiwa kama watu watachukua muda mwingi kuangalia na kujadili madhaifu ya mtu na kuacha kuangalia mazuri ya mtu kwani suala hili linachelewesha maendeleo ya nchi.


Dkt. Biteko aliwataka wanaCCM kuendelea kukiimarisha Chama katika ngazi za chini kwenye mashina na matawi kwani ndiko wananchi wengi walipo.


MWENYEKITI KAMATI YA UJENZI


Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Kamati ya ujennzi wa ofisi hizo, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, Said Nkumba uzinduzi wa majengo hayo ni awamu ya pili.


"Hapa, mbali na ofisi, tuna ukumbi wa kisasa wenye uwezo wa kubeba watu 1,000 na 'facilities' zote ikiwemo 'system' ya mziki na viti. 


"Hii ofisi tunayoizundua awamu ya pili ya ujenzi ikijumuisha ofisi ya Mwenyekiti wa CCM wilaya, Katibu wa Chana, makatibu wa jumuia zote, ofisi ya mbunge, chumba cha masjiala, ofisi ya PS, chumba cha TEHAMA, ukumbi kwa ajili ya wajumbe wa halmashauri Kuu, duka pamoja na mgahawa wa kisasa” alisema.


Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Naibu Waziri Mkuu ambae pia ni Waziri wa Nishati Mhe. Dotto Biteko,Akizungumza katika Mkutano wa Uzinduzi wa Ofisi ya CCM Wilaya ya Bukombe
Katibu wa Idara ya Oganaizesheni CCM Ndg.Issa Gavu,  Akizungumza na Viongozi na Wanachama wa CCM Mara Baada ya kuzindua Ofisi za CCM Wilaya ya Bukombe Mkoani Geita






No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.