Habari za Punde

Maonesho ya Sanaa ya Picha za Kuchora Yazinduliwa Zanzibar

Katibu Mtendaji Baraza la Sanaa,Sensa ya Filamu  na Utamaduni BASFU Dkt.Omar Abdalla Adam akipata maelezo kuhusia na maonesho  ya tatu ya sanaa ya uchoraji wa picha yenye  mada ya  “Hadithi ya bibi” kutoka kwa Lisenka Beetstra Mjumbe wa bodi ya  Taasisi ya  Emerson’s Foundation  huko nyumba ya sanaa Hurumzi Mjini Unguja.

Na fauzia Mussa,   Maelezo

WAKFU wa Emerson Zanzibar umezindua maonesho ya picha za kuchora zilizoingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania tuzo ya mchoraji bora wa mwaka 2023.

Akizungumza baada ya kuzindua maonesho hayo Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa, Sensa ya Filamu na Utamaduni Zanzibar (BASFU) Dkt. Omar Abdalla Adam amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inafarijika kuona  wadau wa sanaa wanaanzisha matukio mbalimbali yanayolenga kuibua na kukuza vipaji vya wasanii.

Alisema Maonesho na tuzo kama hizo zinazobuniwa na Taasisi binafsi, ni njia moja ya  kukuza vipaji na kuwaletea tija wasanii kwa kuuza kazi zao ndani na nje ya Nchi pamoja na kuinua uelewa wa wasanii wenye tafsiri  inayounganisha kizazi kipya na historia ya zamani katika malezi na maadili ya Kizanzibari.

 “Zanzibar tuna utajiri mkubwa wa vitu vya historia vinavyohitaji kuchorwa ili visipotee, kwa mfano baibui la kamba lenye aina nyingi za uvaaji na maana zake hakuna kazi mbaya ya sanaa, bali tafauti ipo katika ubunifu na ujumbe unaopatikana.”Alifahamisha Katibu huyo

Katika kuthamini juhudi za Wasanii hao Katibu huyo aliahidi kuwapatia vyeti vya usajili vitakavyowawezesha kutambuliwa rasmi na BASFU kuwa ni wasanii halali bila ya malipo  ili kuweza   kupata haki zao nyengine ndani na nje ya Nchi.

“kwa kawaida cheti hicho kinalipiwa shiligi laki moja na nusu lakini nyinyi tutawapatia bure kabisa kama mchango wa Serikali katika kuibua vipaji vya vijana”Alieleza Katibu huyo

Awali aliwapongeza wachoraji ambao kazi zao zimeteuliwa kuwania tuzo hiyo, zinaonesha hazina ya vipaji vilivyopo nchini na kuwataka waliokosa nafasi ya kushiriki  wasivunjike moyo na kujaribu katika mkupuo mwengine wa mashindano hayo.

Mratibu wa Wakfu wa Emerson Salma Adim amesema Taasisi hiyo imekuwa ikiandaa tuzo mbalimbali kwa wasanii wa filamu, muziki na picha za kuchora, kwa ajili ya kuibua na kustawisha vipaji  vyao pamoja na kuitangaza Zanzibar kimataifa.

Alifahamisha kuwa mbali na uangalizi na uamuzi wa majaji, wadau mbalimbali waliohudhuria ufunguzi huo na watakaotembelea maonesho hayo watapata fursa ya kuchagua picha walizoona zinastahiki kupatiwa  tuzo hiyo.

Alisema Maonesho ya picha hizo yataendelea hadi Disemba  7 na kutangazwa mshindi  ifikapo  Disemba 8, 2023 ambae atakabidhiwa cheti, tuzo (Trophy) pamoja na fedha taslim kiasi cha  shilingi milioni mbili za Kitanzania.

Kwa upande wa Mshindi wa pili alisema atapatiwa nafasi ya kuonesha kazi zake katika nyumba hiyo na kuuzwa  kwa watakaohitaji.

Maonesho hayo ni ya tatu kufanyika tangu kuanzishwa katika nyumba ya sanaa ya Emerson Hurumzi mjini Zanzibar yakibeba ujumbe“Hadithi ya Bibi”  na kushirikisha wachoraji wazawa wenye umri kati ya miaka 18 hadi 35.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.