SERIKALI ya Mapinduzi
ya Zanzibar imewatoa hofu Mfuko wa Hifadhi ya Huduma za Jamii Zanzibar, (ZSSF)
na kuwataka kuwekeza fedha zao kwenye miradi mikubwa ya Serikali ya kimakakati.
Pia, Serikali
imejizatiti kuweka dhamana ya miradi mikubwa ya maendeleo itakayotekelezwa na
Mfuko huo pamoja na kuwahakikishia usalama wa fedha zao endapo zitaathiriwa kwa
namna yoyote na ujenzi wa miradi hiyo.
Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, aliyasema hayo alipoweka jiwe la
msingi la ujenzi wa maegesho ya magari, Malindi Wilaya ya mjini, Mkoa wa Mjini
Magharibi.
Alisema, lengo la Serikali
kuweka ujenzi wa maegesho hayo ni kupunguza msongamano wa magari mjini pamoja
na kuweka usafiri wa umma wa aina moja na wa kisasa ili kwenda sambamba na
mahitaji ya mji kwa wakati uliopo.
Alisema, hayo ni maegesho
ya kwanza ya ghorofa kujengwa Zanzibar, yenye hadhi na mitambo ya kisasa.
Rais Dk. Mwinyi alitoa
ushuhuda wa Mifuko ya hifadhi ya Jamii kwa mataifa mengine duniani ikiwemo
Indoneia na Malaysia yamejenga nchi zao kwa kuweka miundominu ya kisasa, miji
mikubwa, maduka, barabara na madaraja makubwa ya maendeleo, hivyo aliwatoa
wasiwasi ZSSF na kuwataka kuiga mifano ya mataifa hayo kwa kuijenga upya
Zanzibar bila kujali hasara ya fedha zao kwani Serikali imewapa dhamana ya
fedha hizo.
Alisema, Serikali pia
imepanga kuweka vituo vikuu viwili vya mabasi ya umma kwa maeneo ya Kijangwani
na Malindi ili kukidhi hadhi ya mji yenye kwenda sambamba na maendeleo ya
mataifa mengine duniani.
Akizungumzia athari
zinazoathiri Hifadhi ya Taifa ya Mji MKongwe wa Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi
amesema ujenzi wa maegesho hayo umezingatia na kufuata taratibu zote
zilizowekwa na hifadhi hiyo kwa mujibu wa matakwa ya UNESCO juu ya mabadiliko
ya maendeleo yanayotekelezwa kwenye maeneo ya Mji Mkongwe.
Aidha, Dk. Mwinyi alieleza,
maegesho hayo yatapunguza msongamano maeneo ya Darajani na Mji Mkongwe kwa
kutoruhusu baadhi ya vyombo vya usafiri kuingia kwenye hifadhi ya mji Mkongwe
ili kuunusuru mji huo na athari ya vyombo hivyo.
Akizungumzia athari kwa
Hifadhi ya Taifa ya Mji MKongwe wa Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi amesema ujenzi wa
maegesho hayo umezingatia na kufuata taratibu zote zilizowekwa na hifadhi hiyo
kwa mujibu wa matakwa ya UNESCO.
Kuhusu mazingira ya
wafanyabiashara wa maeneo ya mjini (Darajani), Dk. Mwinyi alieleza Serikali
imekusudia kujenga eneo maalumu la wafanyabiashara hao lenye hadhi ya juu na
mwonekano wa kisasa, ili kuepusha wafanyabiashara kuenea kiholela barabarani na
kueleza kuwa eneo la Darajani ni kitovu kikuu cha biashara, Zanzibar.
Alisema, ujenzi huo pia
utahusisha barabara kuu ya Darajani pamoja na eneo maalum la wafanyabiasha.
Naye Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ,
Masoud Ali Mohammed, alisema
juhudi za Mapinduzi zinazoendelezwa na awamu ya nane ya Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar ni mapinduzi ya Uchumi na kuboreshwa maendeleo kwa kuendelezwa
miradi mikubwa ya maendeleo kwenye sekta zote za jamii ikiwemo Afya, elimu,
sekta ya miundombinu na Barabara, maji safi, makaazi ya kisasa ya wananchi na
viwanja vya michezo vyenye hadhi ya kimataifa.
Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Aboud Hassan Mwinyi, alisema ujenzi wa
maegesho hayo unatarajiwa kuchukua gari 200 kwa wakati mmoja, utagharimu bilioni
6.83 hadi kukamilika kwake na sasa umefikia asilimia 65 ya ujenzi wote.
Pia,
alisema ujenzi huo umetoa ajira kwa wazawa ikiwemo wakandarasi wasaidizi pamoja
na Serikali kukusanya mapato yanayotokana na ujenzi huo.
Mapema
akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mfuko wa Hifadhi ya
Jamii Zanzibar (ZSSF), Nassor Shaaban Ameir alisema mbali na mradi huo wa
maegesho ya magari ya ghorofa, Malindi pia wanatarajia kuanza ujenzi mwengine wa
kituo kikubwa cha mabasi ya uma kwenye eneo hilo.
IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment