Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb)
akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalaum, Mhe. Nusrat
Shaaban Hanje, kuhusu miradi iliyotekelezwa kwa fedha za
Uviko – 19 na swali la Mbunge Viti Maalum, Mhe. Janejelly
Ntate, kuhusu changamoto ya uhaba wa watumishi katika
vyombo vya Bodi ya Rufaa za Kodi (TRAB) na Baraza la Rufani
za Kodi (TRAT).
(Picha na Kitengo Cha Mawasiliano – Wizara ya
Fedha)
Na. Chedaiwe Msuya, WF, Dodoma.
Serikali imetumia fedha za UVIKO-19 kiasi cha shilingi trilioni 1.29 zilizotolewa kama mkopo nafuu na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kutekeleza mirandi katika sekta za maji, elimu, utalii, afya na uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Hayo yameelezwa bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa
Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), wakati akijibu
swali la Mbunge wa Viti Maalaum, Mhe. Nusrat Shaaban
Hanje, aliyetaka kufahamu miradi iliyotekelezwa kwa fedha za
Uviko – 19
Mhe. Chande alisema kuwa katika Sekta ya Maji, fedha za
mkopo zilitumika kununua mitambo 25 ya kuchimba visima,
seti tano za mitambo ya kuchimba na kujenga mabwawa, seti
nne za vifaa vya uchunguzi wa maji chini ya ardhi na miradi ya
maji 172 vijijini na miradi 46 mijini.
Alisema Sekta ya elimu yalijengwa madarasa 12,000 (shule za sekondari) na 3,000 (shule za msingi shikizi), ukamilishaji wa vyuo vinne vya VETA ngazi ya mikoa na vyuo 25 ngazi ya wilaya na ununuzi wa vifaa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu kwenye vyuo 11 vya elimu ya juu.
Sekta zingine zilizotumia mkopo wa Uviko – 19 ni pamoja na Sekta ya Utalii ambapo mitambo mitano (5) ilinunuliwa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu kwenye hifadhi 13 za Taifa na kuimarisha mifumo ya utangazaji wa fursa za utalii ikiwemo The Royal Tour.
Kwa upande wa sekta ya Sekta ya Afya, Mhe. Chande alisema miradi iliyotekelezwa ni ujenzi na ukarabati wa vyumba vya wagonjwa mahututi (ICU) katika hospitali 70 na miundombinu ya kutolea Huduma za Dharura (EMD) katika hospitali 101, ununuzi wa X-ray 169, CT-Scan 29, MRI nne na mashine za huduma za uchunguzi wa moyo -Echo Cardiography 7 na ujenzi wa nyumba 150 za wafanyakazi.
“Fedha za mkopo zilitumika katika uwezeshaji wa wananchi kiuchumi ambapo Serikali imeboresha miundombinu na mazingira ya kufanyia biashara kwa wafanyabiashara wadogo (wamachinga) eneo la Bahi Road Dodoma, Halmashauri za Majiji ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Tanga, Mbeya, Morogoro pamoja na Halmashauri za Manispaa ya Kinondoni, Temeke na Ubungo mkoani Dar es Salaam” Aliongeza Mhe. Chande.
Naibu Waziri Mhe. Chande alisema shilingi bilioni 5.542 zimetumika kusaidia kaya maskini 51,290 zilizotambuliwa katika halmashauri 35 kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF).
Kwa upande mwingine akijibu swali la Mbunge Viti Maalum
Mhe. Janejelly Ntate aliyetaka kujua wakati ambao Serikali
itamaliza changamoto ya uhaba wa watumishi katika vyombo
vya Baraza la Rufani za Kodi (TRAT) na Bodi ya Rufaa za Kodi
(TRAB), Mhe. Chande alisema kuwa TRAB ina jumla ya
watumishi 27, ambao kwa sehemu kubwa wanamudu
kutekeleza majukumu ya taasisi ikilinganishwa na ikama ya
watumishi 35.
Aidha alieleza kuwa kwa upande wa TRAT inapaswa kuwa na
watumishi 36, ambapo kwa sasa kuna watumishi 15,
hivyo Wizara ya Fedha imefanya “head hunting” ya kupata
watumishi wanne wenye uzoefu na kuwasilisha maombi ya
uhamisho Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora, mwezi Januari, 2024 ili kutatua changamoto
hiyo.
No comments:
Post a Comment