Habari za Punde

Rais wa Jamhuri ya Poland Awasili Nchini Tanzania kwa Ziara ya Kitaifa ya Siku Mbili Nchini

Rais wa Jamhuri ya Poland, Mheshimiwa Andrzej Duda amewasili nchini kwa Ziara ya Kitaifa ya siku mbili.

Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam Mhe. Rais Duda na mkewe Agata Kornhauser-Duda wamepokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba, Waziri wa Fedha Mhe. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Mhe. Mudrick Soraga na viongozi wengine waandamizi wa Serikali.

Ziara hii ni ya kwanza kwa Rais kutoka Poland kutembelea Tanzania tangu kuanza kwa ushirikiano wa uwili kati ya nchi hizi ikilenga kuimarisha ushirikiano katika miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye sekta za kilimo, kodi, viwanda na biashara, utalii, elimu, usafiri, afya, tiba za mifugo, na maji.

Kwa kupitia ziara hii maeneo mapya ya ushirikiano yataibuliwa kati ya Tanzania na Poland kupitia sekta za ulinzi na usalama, nishati, madini, ulinzi wa mitandao, utamaduni na uchumi wa buluu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan atampokea rasmi Rais Duda Ikulu, Dar es salaam Februari 9, 2024 kwa mazungumzo na baadaye watazungumza na waandishi wa habari.

Akiwa nchini, Rais Duda anatarajiwa kutembelea mradi wa matibabu ya dharura katika Hospitali ya Aghakhan, Dar es Salaam kujionea utekelezaji wa mradi huo ambao Serikali ya Poland imetoa msaada wa Dola za Kimarekani milioni 1.136  kufadhili mradi huo wenye lengo la kutoa msaada kwa sekta ya matibabu na kusaidia elimu ya wahudumu wa afya katika mkoa wa Dar es Salaam.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akizungumza na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Poland Mhe. Andrzej Duda, mazungumzo hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa VIP Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam alipowasili Nchini kwa ziara ya Kitaifa ya Siku mbili Nchini.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akizungumza na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Poland Mhe. Andrzej Duda, mazungumzo hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa VIP Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam alipowasili Nchini kwa ziara ya Kitaifa ya Siku mbili na (kushoto kwa Waziri) Waziri wa Fedha na Mipango Tanzania Mhe. Mwigulu Nchemba na Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Mhe. Mudrick Soraga.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.