Habari za Punde

Serikali kujenga chuo cha Ufundi Veta, Kata ya Liganga

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama (Mb) Peramiho  akizungumza na Mabalozi wa kata ya Mpandangido, Peramiho, Parangu, Maposeni na Kilagano katika Halmashauri ya Songea Vijijini Mkoani Ruvuma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama (Mb) Peramiho akiwa katika Picha ya Pamoja na wenyeviti wa Mashina Katika shule ya sekondari Mtopesi Halmashauri ya Songea  Vijini Mkoani Ruvuma.

Na Mwandishi wetu.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama (Mb) Peramiho amesema Serikali imefanya Maboresho makubwa katika sekta ya elimu katika kipindi cha miaka mitatu.

Kauli hiyo ameitoa Wakati alipoongozana na Wenyeviti wa Mashina wa CCM katika kata ya Parangu, Mpandangido, Kilagano na Maposeni kujionea utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwenye ujenzi wa Miundo Mbinu ya Mambweni na Madarasa uliyofanyika katika shule ya sekondari Maposeni na Mtopesi Leo tarehe 28/02/2024 katika Halmashauri ya Songea Mkoani Ruvuma.

Waziri amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongoza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu ya elimu, ili kupunguzia wananchi adhaa ya kuchangishana michango kwa ajili ya ujenzi. 

Katika shule ya Sekondari Maposeni kuna ujenzi wa vyumba vya madarasa zaidi ya 40, ambapo kuna madarasa ambayo ujenzi umekamilika na mengine yako mbioni kujengwa.

"Hivyo basi jamii inawajibu wa kumlinda mtoto wa kike na kumlinda mtoto wa kiume kwa kuwapatia elimu bora itakayosaidia kujenga Jamii yenye weledi," alisema.

Ameongeza kusema zawadi nyingine aliyotupatia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt, Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha anafuta ada na kusaidia watoto wengi kwenda shule.

Kutokana na ongezeko la wanafunzi, tunahitaji kuongeza miundo mbinu ya elimu kwa ajili ya vijana wetu.

"Serikali inaandaa mitaala mpya ambayo itasaidia kuwapa elimu ya ufundi vijana wetu waweze kupata ujuzi " alibainisha

Sambamba na hilo Halmashauri yetu ya Songea Vijijini, serikali itajenga chuo kikubwa cha Ufundi cha VETA katika Kata ya Liganga ili kuwezesha vijan kupata elimu ya ujuzi katika chuo hicho.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Songea Vijijini Mhe. Menace Komba amesema tayari wameshaanza utaratibu wa kuomba wizara ya elimu ili kupata kibali cha kubomoa majengo ya zamani ya shule ya sekondari Maposeni na Mpitimbi ili kujenga Madarasa mapya.

"Uamuzi huo umeafikiwa na Halmashauri ya Songea Vijijini ili kuipatia shule ya sekondari  Maposeni pamoja na Mpitimbi muonekano mzuri na wakuvutia,"alisema.

Awali Mwalimu Mkuu wa shule ya sekondari Mwalimu Dismass Nchimbi akizungumza mbele ya ujumbe wa wenyeviti wa Mashina alisema serikali imefanya mambo mengi katika shule ya sekondari Maposeni.

"Tumepata mradi wa ujenzi wa Mambweni 2, na Madarasa 4 na vyoo matundu 10 mradi unaofadhiliwa na Barick katika Jimbo la Peramiho, " alisema.

Serikali kwa kupitia Mbunge wa Peramiho amesaidia pia ujenzi wa jengo jipya la utawala ambalo limegharimu kiasi cha shilingi million 74 na ujenzi wake umefikia kwenye lenta

Akitoa neno la shukrani Mwanafunzi, Ahad Antony Bugari umeshukuru serikali kwa kuimarisha Miundo Mbinu ya elimu katika shule ya sekondari Maposeni.

Amemshukuru walimu wa Maposeni kwa kusimamia vizuri ujenzi wa Miundo Mbinu ya elimu katika sekondari ya Maposeni.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.