Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo (katikati)
akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 20, 2024 Jijini Dodoma kuhusu
hatua za utekelezaji wa katazo la matumizi ya kuni na mkaa. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais
(Muungano) Bw. Abdallah Hassan Mitawi.
Taasisi
za umma zinazolisha watu zaidi ya 100 kwa siku kutoka katika Wizara sita zimetekeleza
maelekezo ya Serikali ya kuhama kutoka matumizi ya kuni na mkaa na kuhamia
katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Wizara
ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imekuwa kinara kwa taasisi zake kutekeleza
agizo hili la Serikali kwa zaidi ya asilimia 85.
Hayo
yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe.
Dkt. Selemani Jafo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 20,
2024 Jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa maelekezo ya
usitishaji wamatumizi ya kuni na mkaa kwa taasisi za umma.
Amesema
lengo la maelekezo hayo ni kupunguza madhara ya kiafya na mazingira
yanayosababishwa na kukithiri kwa matumizi ya kuni na mkaa katika jamii zetu na
ukataji wa miti kwa ajili ya nishati ya kupikia.
Dkt.
Jafo amesisitiza kuwa katazo hilo haliwahusu watumiaji katika
ngazi ya kaya na watumiaji wadogo bali limeanza kwa watumiaji wakubwa na Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi hao
ili waanze kutumia nishati safi ya kupikia
“Kama
nilivyosema awali Taasisi hizo ziko chini ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa,
Wizara ya Afya, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum, Wizara
ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,”
amesema Dkt. Jafo.
Dkt.
Jafo amesema Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021 inahimiza umuhimu wa
kulinda na kuhifadhi mazingira ikiwemo rasilimali za misitu, hivyo ili kufikia
lengo hilo, Sera inahamasisha matumizi ya nishati mbadala wa kuni na mkaa kwa
lengo la kupunguza ukataji miti na uharibifu wa misitu.
Ameongeza
kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais ilitoa katazo la matumizi ya kuni
na mkaa kwa taasisi zinazoandaa na kulisha watu zaidi ya mia moja (100) kwa
siku, ifikapo Januari, 2024 ambapo katika taarifa yake ya utekelezaji Wizara
hizo zimetuma mipango husika ya matumizi ya nishati mbadala na jinsi
zitakavyotekeleza agizo hili.
Kwa
mujibu wa Dkt. Jafo, katika sekta ya Elimu hadi kufikia Januari 31, mwaka huu
jumla ya Vyuo vya Ualimu 30 kati ya 35 sawa na asilimia 85.71 ya lengo, Vyuo
vya Maendeleo ya Wananchi 51 kati ya 54 sawa na asilimia 94.44 ya lengo, na
Vyuo vya Elimu ya Ufundi (VETA) vinane (8) kati ya 36 sawa na asilimia 22.22
vimeshaunganishwa na huduma ya Nishati Mbadala ya Kuni Poa.
Amefafanua
kuwa Sekta ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, kuna
jumla ya Taasisi 8 ambapo 6 ni vyuo vya maendeleo ya Jamii na taasisi mbili ni
vyuo vya maendeleo ya jamii na ufundi. Vyuo vya Maendeleo ya Jamii Tengeru na
Uyole kwa sasa vimeanza kutumia Nishati mbadala sawa na asilimia 25 ya lengo.
Aidha
Dkt. Jafo ameeleza kuwa katika Sekta ya Afya hadi kufikia Januari 31 mwaka huu
Hospitali tatu (3) ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala (DSM),
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma na Kituo cha Afya Sinza (DSM) tayari zimeanza
kuzalisha gesi.
Kuhusu
taasisi zilizopo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Chuo cha Chuo cha Maafisa wa
Polisi Kidatu na shule ya Polisi Tanzania zinatumia majiko yenye mfumo wa gesi.
Na baadhi ya vyuo ikiwemo Chuo cha Polisi Zanzibar wanatumia gesi na kuni
kidogo.
“Jeshi
la Magereza lina jumla ya Magereza 129, Vyuo vya Magereza vinne (4) na Shule za
Sekondari Bwawani. Kati ya vituo hivyo jumla ya Magereza 76 sawa na asilimia
58.91, Vyuo 3 sawa na asilimia 75 ya vyuo vya magereza, na Sekondari ya Bwawani
yameanza kuacha kutumia kuni na mkaa na kuanza kutumia nishati mbadala ikiwemo
gesi asilia” amesema Dkt. Jafo.
Katika
Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Jafo amesema asilimia 90 ya
baadhi ya vikosi vinatumia nishati mbadala kama vile gesi wakati huo vikosi
vingine vikiwa vimetekeleza kwa kiwango cha wastani kwa kupunguza matumizi ya
kuni na mkaa na kuanza kutumia gesi.
Aidha
Dkt. Jafo amesema katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali
za Mitaa (TAMISEMI), ambayo inamiliki kiwango kikubwa cha shule za Msingi na
Sekondari nchini, jumla ya shule 571 za bweni zenye wanafunzi wapatao 156,622.
Kati ya shule hizo za bweni, shule 67 sawa na asilimia 11.73 zimefungwa mifumo
ya gesi ambapo shule 60 kati ya hizo zinatumia mufumo ya gesi.
Amesema
kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Wizara za Kisekta ipo kwenye
maandalizi ya kuunda Timu ya Wataalam itakayoweza kutembelea taasisi husika ili
kufuatilia hatua zinazoendelea katika utekelezaji wa katazo hilo na kutoa
ushauri wa kitaalam.
Itakumbukwa kuwa tarehe 01 Novemba, 2022, Jijini Dar es Salaam, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alizindua Mjadala wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia ambapo aliekeza kusitisha matumizi ya kuni na mkaa kwa taasisi zinazolisha watu Zaidi 100 kwa siku, ifikapo Januari 31, 2024.
No comments:
Post a Comment