Habari za Punde

Zanzibar Kuunga Mkono Kampeni ya Chanjo ya Surua Itakayoendeshwa Tanzania Bara

Mkurugenzi kinga na elimu ya afya Dkt. Salim Slim akitoa taarifa kuhusiana na  zoezi la utoaji wa  chanjo kwa watoto chini ya umri wa miaka 5 litakalofanyia kuanzia febuari 15 hadi 18 mwaka huu, hafla iliyofanyika wizara ya afya  Zanzibar

PICHA NA FAUZIA  MUSSA- MAELEZO ZANZIBAR

Na Fauzia Mussa, Maelezo Zanzibar

Wizara ya Afya Zanzibar imesema itaunga mkono zoezi la kampeni ya chanjo ya Surua /Rubella kwa watoto wote wenye umri wa kuanzia miezi 9 hadi miaka 5 litakaloendeshwa na Wizara ya Afya Tanzania.

 

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya  Dkt Salim Slim  amesema kuanzia Februari 15 hadi 18 mwaka huu , Wizara ya Afya ya serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania  itaendesha zoezi hilo  katika mikoa yake yote hivyo Zanzibar itaunga mkono kwa kuwachanja watoto waliopo Zanzibar ambao wanaishi Tanzania bara katika tarehe hizo ili kuhakikisha kila mtoto anapata chanjo hiyo.

 

"Kwa vile zoezi la kampeni ya Chanjo ya Surua litakua linaendelea huko Tanzania Bara, watoto wote wenye umri kuanzia miezi 9 hadi miaka 5 ambao wanaishi Tanzania Bara, ila kwa kipindi hiki wapo Zanzibar, wanapaswa kupelekwa vituo vya Afya au maeneo yatakayokua yanatoa huduma za chanjo ndani ya Shehia ili kupatiwa chanjo ya Surua/Rubella" alifafanua Dkt Slim

 

Alifahamisha kuwa  wakati kampeni ya chanjo ya surua ikindelea kufanyika Tanzania Bara, Zanzibar itaendesha zoezi la kuwapatia chanjo watoto wote walioko chini ya umri wa  miaka 5 ambao hawakukamilisha ratiba za kupatiwa chanjo zinazostahiki.

 

“Zoezi la kuwachanja watoto waliokuwa hawakukamilisha ratiba za chanjo au kpata chanjo kabisa  litafanyika sambamba na  uendeshaji wa kampeni ya chanjo ya Surua/Rubella zoezi litakalofanyika Tanzania bara”.  Alifahamisha Dkt. Slim

 

Hivyo amewaomba na kuwashauri wazazi na walezi kuhakikisha kwamba wanatumia fursa hiyo kuwapatia chanjo watoto wao ambao hawajakamilisha ratiba  au hawajapata kabisa chanjo hizo.

 

Katika hatua nyengine amesema Zanzibar imefanikiwa kutokomeza magonjwa ya ndui, dondakoo, kifaduro, pepopunda ya watototo wachanga pamoja na kufanikiwa kuudhibiti ugonjwa wa surua na kuwa sio tishio tena kwa watoto na kusema kuwa  Zanzibar imekua miongoni mwa nchi zisizo na virusi pori vya Polio vinavyosababisha ulemavu kwa watoto wadogo.

 

Amesema imethibitika kuwa chanjo ni mkakati muafaka katika kutokomeza maradhi na kupunguza vifo vya watoto, ambapo kwa kwa sasa Zanzibar haina mripuko wa ugonjwa wa Surua.

 

Itakumbukwa kwamba Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limethibitisha kuwa chanjo huzuia takribani vifo million 2 hadi 3 kila mwaka kutokana na maradhi yanayokingwa kwa chanjo duniani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.