Habari za Punde

KINANA ASHAURI WATUMISHI,WATAALAMU SERIKALINI WASITOE AHADI BILA MIPANGO.

 Na Mwandishi Wetu,Mara

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana ameeleza kuwa , ni vema watumishi na Wataalam wa Serikali kutotoa ahadi ambazo wanajua hazitatekelezeka au utekelezaji wake utachukua muda mrefu kukamilika kwani imekuwa ikisababisha kukwamisha shughuli za maendeleo na kusababisha malalamiko kwa wananchi.


Hayo yameelezwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM 

Tanzania Bara, Abdulurahman Kinana alipokuwa 

akizungumza na wananchi wa Bunda Mjini wilayani 

Bunda mkoani Mara baada ya kupokea malalamiko ya 

wananchi kuwa serikali iliwataka wahame katika 

maeneo yao kupisha ujenzi wa mradi wa maendeleo.


Pia, wananchi hao walionesha kukerwa na kitendo cha 

maeneo yao kuchukuliwa, nyumba kubomolewa na 

kupewa sharti la kutoendeleza maeneo hayo likiwemo 

eneo la Kijiji cha Nyantwale.


Hivyo kutokana na malalamiko hayo Kinana alisema 

"Viongozi wa serikali kabla ya kuwahamisha wananchi 

ni vema wakaeleza ni lini ahadi hiyo itatekelezwa, kama 

ni fidia, lini fidia hiyo itatolewa, kama ni watu kuhama 

watahama lini, kama watu ni kupewa fidia watapewa 

lini," alisema.


Aliongeza kuwa, hakuna sababu ya kutoa ahadi ambayo 

inachukua miaka mingi kutekelezwa na kila kiongozi 

anayekuja anatoa ahadi anaondoka.


Kinana alishauri watendaji wa serikali kabla ya kufanya 

uamuzi unayohusu kuhamisha watu, kufidia au kufanya 

jambo lolote linalohusu wananchi, ni vyema wafanye 

utafiti wa kutosha kupata uhakika kuhusu malipo ya 

wananchi, fedha zipatikanaje ndipo watoe kauli, na si 

vyema kauli itangulie kabla ya kutanguliza fidia.


Makamu Mwenyekiti Kinana alisema kuwa, 

kumekuwapo  na tabia ya kuwaeleza wananchi kuhusu 

kuhama au kutohama halafu hakuna kinachoendelea.


Kinana  alifafanua zaidia kwa kueleza kwamba, 

“viongozi na watendaji acheni utaratibu wa kutoa ahadi 

bila ya kujiandaa, ni muhimu mkajipanga kwanza ili  

mnapotoka na majibu muwe na uhakika na 

mnachosema.”


Alisema hata yeye anakumbuka wananchi hao 

waliahidiwa na mwaka jana mawaziri sita walifika 

katika eneo hilo wakiwa na usafiri wa helkopta na 

kuwataka watu wahame.


“Sasa walitoa ahadi bila kujiandaa na wamedanganya 

watu leo wananchi wanakuja kuniuliza mimi sasa 

nitawajibu nini?. Nataka kuwasihi hapa watendaji wa 

serikali kabla ya kuahidi kitu ni muhimu mkaanza 

kujipanga kuepusha usumbufu.


“Kama alivyosema Rais Samia Suluhu Hassan wakati 

anamwapisha mkuu mpya wa mkoa huu, alimtaka 

aende akahakikishe watu wanapewa haki yao.


“Nikifika Dar es Salaam nitaenda kuongea na Waziri wa 

Fedha (Dk. Mwigulu Nchemba) kumuuliza kuhusu 

malipo yenu aniambie kama umefika mwisho au bado.


“Kama jambo halijaiva msitoea ahadi kwa wananchi. 

Wananchi wakawa tayari kuhama. Nendeni serikali 

mkajiandae, sio mnatupa ahadi hewa mfano mzuri 

Nyantwale," alisema.


Mkazi wa Kijiji Cha Nyantwale, Saasita Mchanga 

alisema wananchi hao bado wanateswa na ahadi hiyo 

huku akitolea mfano kuwa wanashindwa hata kujenga 

matundu ya choo katika shule yao kwa kusuburi hatima 

ya kuhama.


"Shule yetu ina zaidi ya wanafunzi 400 na wana uhaba 

wa matundu ya vyoo, kwa sasa kuna matundu mawili 

pekee, sasa tunahofu ya kupata magonjwa ya mripuko,"


Kinana alitumia utaratibu wa kutoa nafasi kwa 

wananchi kuwasilisha kero na changamoto mbalimbali 

zinazowakabili kwa maswali na ushauri, kisha alizijibu 

au kutoa fursa kwa watendaji wa halmashauri hiyo 

kutoa ufafanuzi.


Baada ya Kinana kutoa utaratibu huo, mkazi wa Bunda 

Stoo, Chacha Wambari alieleza kero ya barabara za 

mitaa kutopitika na kutaka kufahamu ni lini 

zitatengenezwa.


Katika kero hiyo pamoja na majibu yaliyotolewa na 

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk. Vicent Naano, Kinana 

alisema barabara nyingi nchini zinatakiwa zirekebishwe 

kutokana na kuharibiwa na mvua zinazoendelea 

kunyesha, lakini kwa sasa serikali haiwezi kurekebisha 

kwa kuwa mvua bado zinaendelea hivyo zinaweza 

kuharibika tena.


“Ngoja mvua ziishie zikaisha barabara zitakarabatiwa ili 

zipitike,” alieleza.Kwa upande wake William William 

ambaye ni mkazi wa Bunda alisema kero yake 

ya kwanza inakwenda kwa Halmashauri ya Mji wa 

Bunda kwa kutokuwa na mkakati ya kuimarisha hali ya 

uchumi wa wananchi.


“Umasikini ni mkubwa katika nchi yetu ni jambo lisilopingika, hawa unawaona hapa wamesimama hawana fedha, pamoja na jitihada za serikali kupeleka maendeleo kwa wananchi lakini fedha kwa mtu mmoja mmoja hali ni mbaya.


“Chama Cha Mapinduzi katika kujipambanua kwake ni Chama kinachoangalia maisha ya watu, hivyo nikuombe ukamwambie mama (Rais Dk. Samia) alegeze kidogo ili twende katika uchaguzi wa serikali za mitaa vizuri, watu tukiwa na pesa,”


Aidha, alisema ni vyema halmashauri hiyo ikaweka mikakati mbalimbali katika kutafuta ya kufungua na kuongeza fursa za kiuchumi hususan katika kilimo kwa kuwawezesha wananchi kushiriki kilimo cha mazao ya kibiashara ambayo serikali inayahimiza.


Alisema kuwa serikali ya CCM iliweka mpango wa kuhamasisha mazao ya kimkakati ikiwemo kahawa, mchikichi na korosho hivyo ni muhimu halmashauri hiyo ikafanya utafiti na kuona ni zao gani lialoweza kulimwa hasa baada ya kilimo cha pamba kilichokuwa kikitegemewa na wana Bunda kuendelea kuzorota.


“Tunaomba mpelekee salamu Rais Dk. Samia kwamba Bunda kuna haja ya kuletewa mazao mengine lakini pia tuna EPZA hapa , nashindwa kuelewa kwasababu hakuna jitihada zozote za Serikalisasa hatujui shida ni nini?


“Mtaani vibaka wamekuwa wengi lakini halmashauri imeshindwa kuona haja ya mazao ambayo serikali inayasisitiza yakaleta kipato kwa mtu mmoja mmoja  Bunda hatuyaoni. Kama mchikichi hauwezi kulimwa, alizeti haiwezi kulimwa na kama tafiti zimefanyika pamba haiwezi kulimwa kwa nini tusieletewe mazao mengine tulime?” alieleza.


Akijibu changamoto hizo Kinana alisema anamheshimu mwananchi huyo kwa kuwa yote aliyoyaeleza yana ‘pointi’ (maana).


“Una akili sana kwa sababu EPZA iliyopo hapa ipo kwa muda mrefu na imepita miaka 16. Waliweka EPZ kabla ya kujua wanataka kufanya nini. Pili anasema kwa nini tusiweke mazao mbadala,” alisema.


Makamu Mwenyekiti Kinana alisema ni vema ushauri wa mwananchi huyo ukasikilizwa na kufanyiwa kazi kwa lengo la kuimarisha hali za wananchi na halmashauri kwa ujumla.


Kwa upande wake Sharifu Masumbuko aliyedai kuwa ni mmoja wa wapiganaji walioshiriki vita ya Uganda mwaka 1978, alisema kero yake ni kutolipwa fedha baada ya kumalizika kwa vita hiyo, hivyo alitaka kufahamu Chama kinawasaidiaje kupata fedha hizo.


Akijibu jambo hilo Kinana alisema hakuna mwananchi yeyote au mwanajeshi aliyepigana vita ya Uganda na hajalipwa kwa kuwa serikali iliyokuwa ikiongozwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ilihakikisha wote walioshiriki wanalipwa na malipo hayo yalifanyika kwa awamu mbili.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.