Habari za Punde

Mkutano wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji la EAC Wafanyika Arusha

 Mkurugenzi wa Ukuzaji Viumbe maji katika Wizara ya  Mifugo na Uvuvi Dkt. Nazael Amos Madalla akifafanua jambo kwenye Mkutano wa Kawaida wa Sita wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uvuvi na Ukuzaji Viumbe maji katika Ziwa Victoria la EAC kwa Ngazi ya Wataalam unaoendelea jijini Arusha 

Mkutano wa Kawaida wa Sita wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji katika Ziwa Victoria la Jumuiya ya Afrika Mashariki unaendelea jijini Arusha katika ngazi ya Wataalam ikiwa ni maandalizi ya mkutano wa Mawaziri wa Sekta hiyo wanaotarajiwa kukutana tarehe 31 Mei 2024. 

Mkutano huo wa siku tano terehe 27-31 Mei 2024, unalenga kufanya tathimini ya utekelezaji wa maagizo, maamuzi na makubaliano yaliyofikiwa kwenye musuala mbalimbali katika mikutano iliyopita ya Baraza hilo, ikiwemo masuala ya kiutawala, utekelezaji wa programu na miradi ya Jumuiya inayoratibiwa na kutekelezwa na Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa Victoria (LVFO) ambayo inasimamiwa na Baraza hilo. 

 

Tathimini na majadiliano yakayofanyika katika mkutano huo pamoja na masuala mengine ni mahsusi katika kukuza sekta ya uvuvi na ustawi wa viumbe maji ikiwemo kuendeleza ufugaji samaki endelevu katika Bonde la Ziwa Victoria na kuweka mikakati ya pamoja ya kuzuia na kupambana na magojwa yanayoathiri ustawi wa samaki na viumbe maji.

Mbali na hayo mkutano huo umepoke taarifa ya maandalizi ya mkutano wa kikanda wa wadau wa tasnia ya ukuzaji viumbemaji katika Jumuiya ya Afrika Mashariki unaotarajiwa Agosti, 2024 Jijini Mwanza. 

 

Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa Victoria (LVFO) ya EAC yenye Makao Makuu yake mjini Jinja, Uganda chini ya usimamizi wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uvuvi na Ukuzaji Viumbemaji inajukumu la kuratibu na kusimamia uendelezaji wa rasilimali za uvuvi na ukuzaji viumbe maji katika Jumuiya. 

Miongoni mwa miradi inayotekelezwa na Taasisi hiyo ni pamoja uendeshaji wa boti katika ziwa Victoria zinazosaidia shughuli za doria na utafiti wa masuala mbalimbali ya samaki na viumbemaji na mradi wa UE-EAC TRUE-FISH unaolenga kukuza ufugaji samaki endelevu katika bonde hilo.

 

Mradi mwingine ni wa ECOFISH ambao umejikita katika kuendeleza matumizi bora na usimamizi endelevu wa rasilimali samaki na viumbemaji kwa kuweka sera na mifumo inayohimiza ufanisi ikiwemo matumizi ya mbinu bora za uvuvi.

 

Mkutano huo Ngazi ya Wataalam umehudhuriwa na nchi ya Tanzania, Kenya, Burundi na Uganda ambao ndio nchi wanachama za Taasisi hiyo.

 

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo Ngazi ya Wataalam unajumuisha wataalam kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), na unaongozwa na Dkt. Nazael Amos Madalla ambaye ni Mkurugenzi wa Ukuzaji Viumbe Maji katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.