Habari za Punde

SMZ inathamini mchango wa Benki ya CRDB katika kukuza uchumi wa Zanzibar na kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini mchango wa Benki ya CRDB katika kukuza uchumi  wa Zanzibar na kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar.

Amesema, benki ya CRDB pia imechangia kukuza sekta mbalimbali za uchuni Zanzibar zikiwemo Utalii, Kilimo, Elimu, Michezo, Ufugaji, Uvuvi, Biashara na Ujasiriamali. 

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo alipofungua semina ya Wanahisa wa Benki ya CRDB kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa  Mikutano Arusha  (AICC).

Alisema, matarajio ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuona taasisi nyingi za umma kutoka Zanzibar zinawekeza kwenye benki hiyo  ili kuendelea kuipa nguvu zaidi ya kukuza ushiriki wake katika miradi ya maendeleo Zanzibar.

Pia Dk. Mwinyi alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni mmoja wa wanahisa wa benki ya CRDB kupitia Taasisi yake ya Mfumo wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), ambayo  inajivunia kwa utendaji wa CRDB. 

Hata hivyo, Rais Dk. Mwinyi ameipongeza CRDB kwa mafanikio waliyofikia kwa mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa mkakati mpya wa biashara.

Pia, Dk. Mwinyi ametoa wito kwa wanahisa wa benki hiyo kutumia vyema fursa ya kujifunza kupitia semina hiyo.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya  CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema benki hiyo itakuwa mdau muhimu wa maendeleo ya Zanzibar na kuendelea kutoa ushirikiano baina yao na Serikali.

IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.