Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amewahimiza wanafunzi na wananchi wote kwa ujumla kuona umuhimu na kulipa uzito suala la usafi wa mazingira kwa ustawi wa nchi.
Ametoa wito kwa taasisi za kifedha, mashirika
mbalimabali na vyuo kuendelea kushiriki katika kampeni za usafi mazingira safi
na kuwasaidia wanafunzi wenye tunu ya kushiriki kikamilifu.
Mhe. Khamis ametoa wito huo kwenye Mahafali ya Tatu ya
Klabu ya Mazingira ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Juni 22, 2024 na
kusema Serikali itaendelea kusimamia usafi kuhakikisha taifa linapiga hatua katika
utunzaji wa mazingira.
Amesema ni muhimu kuendelea kutolewa kwa elimu ya
mazingira hasa katika vyuo hatua itakayosaidia kuchagiza mapambano dhidi ya
mabadiliko ya tabianchi yanayotokana na kutokulindwa ipasavyo kwa mazingira
katika nyanja mbalimbali za maisha.
Halikadhalika, Naibu Waziri Khamis amesema ujumbe wa
mwaka huu wa mahafali hayo "Tunza Mazingira na Wewe Yakutunze" unahimiza
kuwa suala la usafi wa mazingira ni jambo nyeti kwa afya, ustawi na maendeleo
ya kila mtu.
“Kupitia mahafali haya nawasihi wanafunzi kuendelea kuwa
mfano bora wa kuendeleza harakati za kulinda, kutunza na kudumisha mazingira
katika maisha ya kila siku kuonesha taaswira kwamba taaluma zao sio ombwe tupu
bali zimebeba mategemeo na uelekeo ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania na ile Mapinduzi ya Zanzibar,” amesema.
Aidha, Mhe. Khamis amewapongeza wanafunzi hao kwa
kuonesha wazi ukomavu wa fikra yakinifu kwao na walimu wao kwa elimu ya utunzaji
wa mazingira chuoni na hivyo kuamsha hamasa ya kushiriki kwa vitendo zoezi hilo
pamoja na changamoto wanazopitia.
Mahafali ya Klabu ya Mazingira ya SUZA hufanyika kila mwaka kwa kila wanafunzi wanaomaliza masomo yao kwa ngazi mbalimbali ili kutathmini maendeleo ya utunzaji wa mazingira chuoni, kuhamasisha utunzaji na ulinzi wa mazingira.
No comments:
Post a Comment