Na Maulid Yussuf. WMJJWW. MWANZA
Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Zanzibar Mhe.Riziki Pembe Juma amesema jukumu la kumlinda mtoto juu ya matukio mbalimbali ya ukatili sio la Serikali pekee bali ni la kila mtu.
Mhe. Riziki ameyasema hayo wakati akitoa Salamu kutoka Zanzibar, wakati wa ziara ya Kamati Tendaji ya Mradi wa "Hapana marefu yasiyo na mwisho", katika Mkoa wa Mwanza.
Mhe Riziki amesema kuwa Serikali zetu zote mbili zimekuwa zikishirikiana na wadau mbali mbali katika kuhakikisha maslahi ya jamii yanapatikana pamoja na kukemea na kupiga vita vitendo hivyo.
Amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inasimamia sheria ya Mtoto no 6 ya mwaka 2011 ambapo inamtambua mtoto ni kuanzia umri 0 hadi 18, na hivo kupiga vita suala zima la ndoa kwa watoto wa umri huo na yeyote anaebainika kwenda kinyume na hilo hatua kali za kisheria zimekuwa zikichukuliwa dhidi yao.
Hivyo amewaomba viongozi wa dini, watendaji wa Serikali, NGOs na wadau wote wa mradi huo kuhakikisha kila mmoja kwa nafasi yake kuwa na jukumu la kupiga vita ndoa za utotoni, kuziangalia sheria zilizopo ili ziendane na azma nzima ya kutokomeza suala hilo na kuwaacha watoto wa kike kusoma ili kutumiza ndoto zao za baadae.
Katika ziara hiyo, pia Mhe. Riziki alipata nafasi ya kuzungumza na Maafisa Usafirishaji maarufu BODABODA katika kituo cha KONA YA BWIRU, Mkoani Mwanza na kuwapongeza kutokana na kazi nzuri wanayoifanya ya kuelimisha abiria wao juu ya suala la ndoa za umri mdogo pamoja na ukatili wa kijinsia, inayotokana na elimu waliyoipata kupitia mradi huo.
Mhe Riziki amesema Serikali ipo pamoja nao na ameuomba uongozi wa Kanisa la KKKT kwa kushirikiana na Serikali na wadau wengine kuangalia uwezekano wa kuwatatulia changamoto zao na kuwawezesha zaidi ili waweze kutimiza ndoto zao za kufikisha elimu hiyo mbali zaidi ya maeneo yao.
Mapema, Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji ya Mradi huo na Mkuu wa Kanisa Mstaafu wa KKKT, DKt Fredrick Onael Shoo, amesema ni vyema kuchukua hatua kwa pamoja na kuleta mabadiliko chanya juu ya suala zima la ndoa za utotoni ili kuwaacha huru watoto wa kike katika masomo yao.
Kwa upande wake Kiongozi Mkuu wa Mradi wa "Hapana Marefu Yasiyo na Mwisho", mama Patricia Mwaikenda amesema lengo la mradi huo ni kuwashirikisha zaidi viongozi wa dini mbalimbali katika kuona wanasaidia na kuielimisha jamii na kukemea ndoa za utotoni.
Mradi huo unasimamiwa na Kanisa la KKKT, ukiwa na kauli mbiu "Ndoa za utotoni sasa mwisho".
No comments:
Post a Comment