Rais wa Zanzibar na Mweyekiti wa Baraza la Mapinduizi
Dk. Hussein Ali Mwinyi ameziagiza sekta zote zilizoguswa na Ripoti ya Jiolojia
na Utafiti wa Madini kuyafanyia
kazi maeneo yao kwa kushirikiana na Wizara ya Maji, Nishati na Madini ili
ripoti hiyo ilete tija kwa taifa.
Alisema, matumizi sahihi ya ripoti hiyo yatachangia uwekezaji utakaozalisha
ajira katika sekta zote husika, na sekta ya ardhi itaweza kuweka mpangilio
mzuri wa matumizi ya ardhi ya kilimo, ujenzi na makaazi, na pia kuiwezesha nchi
kujikinga mapema na maafa kabla ya kutokezea.
Rais
Dk. Mwinyi ameyasema hayo ukumbi wa Golden Tulip, Kiembesamaki Wilaya ya Mjini
Mkoa wa Mjini Magharibi wakati akizindua Ripoti ya jiolojia na utafiti wa
Madini, Zanzibar.
Katika kufanikisha
agizo hilo, Dk. Mwinyi amesisitiza kwa Wizara ya Maji Nishati na Madini kuzipatia haraka nakala ya ripoti hiyo taasisi zote zilizoguswa ili zianze
kuifanyia kazi mapema iwezekanavyo.
Alibainisha kupitia ripoti hiyo nchi itakuwa na uwezo wa kujikinga na
maafa kabla ya kutokezea hatua aliyoieleza itathibitisha dhana ya Jiolojia ya
Zanzibar kuwa ni kichocheo cha Uchumi wa nchi.
Pia, amewasisitiza wakandarasi wa majengo na kamisheni ya maafa
kuitumia ripoti hiyo wanapopanga mipango yao kunusuru majanga yasitokee pamoja
na kutengeneza ramani ambayo itarahisisha kujua maeneo hatarishi.
Amesema, uzinduzi wa ripoti hiyo utasaidia kuimarisha dhamira ya
Serikali ya kuifanya Zanzibar kuwa kituo kikuu cha Utalii kwani mapango
yaliyogundulika katika ripoti hiyo, yataweza kutumika kama sehemu za vivutio
vya utalii baada ya kuimarishwa.
Hata hivyo, Rais Dk. Mwinyi ameeleza kufarajika kwake na ushirikiano wa
Wizara mbili za SMZ na SMT kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na wataalamu wa
ndani kushirikiana na wenzao wa Wizara ya Madini ya Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kupitia Taasisi ya Utafiti wa Miamba na Madini (GST) ya
Dodoma kufanikisha utafiti na hatimae kuandaa ripoti hiyo.
Mapema Waziri wa Maji Nishati na Madini wa Zanzibar, Shaibu Hassan Kaduara
amesema, Zanzibar inahitaji kufanya utafiti wa kina zaidi hususani baharini
kwani viashiria vinaonesha kuwa bado kuna madini zaidi yanayoweza kupatikana
ambayo hayajagundulika katika utafiti huo uliotajwa kuwa ni wa awali.
Naye, Waziri wa Madini wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Antony Peter
Mavunde amesema, Kisiwa cha Pemba kinaweza kuwa na miradi mikubwa kupitia Sekta
ya madini baada ya kugundulika kwa madini muhimu yanayohitajika kwa kiasi
kikubwa duniani ambayo hutumika kutengenezea injini za ndege, vigae vya
marumaru na vifaa vya hospitali. Pia kutasaidia ukuaji wa viwanda, upatikanaji
wa malighafi na kuongezeka fursa za ajira.
Amesema, chimbuko la ripoti hiyo ni maagizo ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi Dk. Mwinyi ya kuzitaka Wizara mbili za Madini za SMZ na
SMT kuimarisha ushirikiano kwa dhamira ya kuimarisha Uchumi wa Zanzibar.
Amebainisha kuwa sekta ya Madini kwa Tanzania bara imekuwa ikichangia
kiasi kikubwa cha mapato ya nchi na kuongoza kuingiza fedha za kigeni ambapo
kwa mwaka wa fedha wa 2022 /2023 sekta ya madini Bara ililiingizia taifa kiasi
cha shilingi trilioni moja na milioni mia saba kutokana na mauzi ya madini.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji Nishati na Madini Joseph Kilangi amesema ripoti
hiyo iliyoanza utafiti wake Mwezi Novemba, 2023 na kukamilika tarehe 14 Machi,
2024 itaisadia Zanziabr kupiga hatua kwenye sekta ya madini.
Alisema, kwa mujibu wa uchunguzi wa kina wa miamba uliofaywa kwa maeneo
mbalimbali Unguja na Pemba ulibaini sampuli 189 za madini nakuonesha kuwepo kwa
miamba yenye chokaa kwa matumizi ya viwanda, kiasi kikubwa cha maji kutokana na
miamba inayohifadhi maji, mafuta na gesi.
IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment