Habari za Punde

Serikali Yaahidi Kuendeleza Ushirikiano na IMF

Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akimkabidhi zawadi Kiongozi wa Timu ya Wataalam ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Bw. Charalambos Tsangarides, anayemaliza muda wake wa kuisimamia Tanzania baada ya kuhudumu kwa zaidi ya miaka mitatu na nusu, katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Mhe. Waziri wa Fedha, jijini Dodoma.
Kiongozi wa Timu ya Wataalam ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Bw. Charalambos Tsangarides, anayemaliza muda wake nchini Tanzania akizungumza wakati wa kikao kifupi na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), wakati alipofika kwa ajili ya kumuaga pamoja na kumtambulisha Kiongozi Mpya wa Timu ya Wataalam ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Bw. Nicolas Blancher, katika ukumbi wa Mikutano wa Mhe. Waziri wa Fedha, jijini Dodoma.
Kiongozi Mpya wa Timu ya Wataalam ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Bw. Nicolas Blancher, akizungumza wakati wa kikao kifupi na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), wakati alipofika kwa ajili ya utambulisho, katika ukumbi wa Mikutano wa Mhe. Waziri wa Fedha, jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akizungumza wakati wa kikao kifupi akiagana na Kiongozi wa Timu ya Wataalam ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Bw. Charalambos Tsangarides, anayemaliza muda wake nchini Tanzania na kumkaribisha Kiongozi Mpya wa Timu ya Wataalam ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Bw. Nicolas Blancher, katika ukumbi wa Mikutano wa Mhe. Waziri wa Fedha, jijini Dodoma.

Na. Saidina Msangi na Asia Singano, WF, Dodoma

Serikali imesema kuwa itaendelea kushirikiana na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), na kuhakikisha Fedha zote za maendeleo zinazotolewa na Shirika hilo zinatumika kukamilisha azma ya kukuza uchumi wa nchi.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), jijini Dodoma wakati akimuaga Kiongozi wa Timu ya Wataalam ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa Tanzania, Bw. Charalambos Tsangarides, aliyemaliza muda wake baada ya kuhudumu kwa zaidi ya miaka mitatu na nusu.

Alisema Serikali itaendelea kutekeleza dhamira yake ya kuwaletea wananchi maendeleo na kukuza uchumi kwa ujumla kupitia juhudi mbalimbali inazofanya ikiwemo kutafuta fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati.

‘Kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, napenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa kujitolea kwako katika kusaidia safari ya maendeleo ya kiuchumi ya nchi yetu, ninawahakikishia kwamba Timu yangu itawapa ushirikiano wote unaohitajika, kwa upande mwingine, nina furaha kuwajulisha kwamba tunaendelea vyema na hatua zetu za mageuzi chini ya program mpya ya Serikali ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia dirisha la Resilient and Sustainable Fund (RSF),’’ alisema Dkt. Nchemba.

Dkt. Nchemba, mbali na kumuaga Kiongozi huyo wa IMF nchini, alitumia fursa hiyo kumkaribisha Kiongozi mpya anayechukua nafasi hiyo Bw. Nicolas Blancher, huku akimuahidi ushirikiano kutoka Serikali ya Tanzania.

‘’Napenda kuchukua fursa hii kumkaribisha rasmi Bw. Nicolas Blancher, kama Kiongozi wetu mpya wa “Mission” kwa Tanzania na tunafurahi kupata nafasi ya kushuhudia mwongozo kutoka kwa mtaalamu mwingine kama tulivyofanya na Kiongozi wa “Mission”anayemaliza muda wake katika kufanikisha maendeleo yetu endelevu ya kiuchumi’’ alisema Dkt. Nchemba.

Kwa upande wake Kiongozi wa Timu ya Wataalam ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa Tanzania, anayemaliza muda wake, Bw. Charalambos Tsangarides, ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano mkubwa alioupata wakati akitekeleza majukumu yake nchini.

Aidha, ameipongeza Serikali kwa juhudi za kusimamia maendeleo ya kiuchumi na kuahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha ustawi wa wananchi wake hata baada ya kumaliza muda wake wa kuhudumu.

Naye Kiongozi Mpya wa Timu ya Wataalam ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Bw. Nicolas Blancher, ameahidi kushirikiana kikamilifu na Serikali ya Tanzania na kumhakikishia Dkt. Nchemba kuwa ataendeleza ushirikiano na kazi zilizofanywa na mtangulizi wake huku akisisitiza dhamira ya kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanatimia.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.