Kamisha wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, ofisi ya Zanzibar, Khatib M. Mwinchande, akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali ofisini kwa Mbweni, Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi akitoa tamko la kulaani mauaji ya Wete Mkoa wa Kaskazini, Pemba
Na.Mwashamba Juma - THBUB
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesema inachunguza vifo vya watu wawili vilivyotokea hivi karibuni, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
THBUB imeeleza imepokea kwa
masikitiko makubwa vifo vya Nd. Athuman Hamad Athuman na Amour Khamis Salim,
waliokuwa wakaazi wa kijiji cha Kiungoni, Wete, Pemba vilivyotokea mwezi
Disemba mwaka 2024.
Akitoa tamko la Tume hiyo
kwa waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali, leo tarehe 10/01/2025, ofisini
kwake Mbweni, Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi, Kamishna wa Tume
hiyo Zanzibar, Khatib M. Mwinchande amesema, tukio la mauaji hayo ni ukiukwaji
wa haki ya kuishi kama ilivyotamkwa na Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Kifungu cha 13(2) cha Katiba ya Zanzibar
ya mwaka 1984 kinachoeleza kuwa kila mtu ana haki ya kuishi na kupata hifadhi
ya maisha yake kwenye jamii kwa mujibu wa sheria, hivyo Tume imelaani vikali
vitendo hivyo.
Akiizungumzia taarifa kwa
Umma iliyotolewa na jeshi la Polisi, Mkoa wa Kusini Pemba ya tarehe 25/12/2024 iliyoeleza
Jeshi hilo linaendeleza uchunguzi wa vifo vya watu hao waliofariki dunia wakati
wakipatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Ali Khamis Camp, Vitongoji Pemba.
Kamishna Mwinchande
amebainisha kuwa mauaji hayo ya Kiungoni Pemba yametokea wakati THBUB
inaendelea na kazi ya kufuatilia mauaji ya Kidoti, Kaskazini Unguja na matukio
mengine kama hayo kwa upande wa Tanzania bara ambayo yanarudisha nyuma juhudi
za Serikali zetu mbili za SMZ na SMT za kuimarisha ulinzi, amani na usalama wa
raia na mali zao nchini.
Aidha, Kamishna Mwinchande
amesema, kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari na mitandao ya kijamii vilidai
kwamba wakati wa uhai wao, marehemu walichukuliwa na askari wa Mamlaka ya
Kudhibiti Dawa za Kulevya wakiwa wazima kwa tuhuma za kuhusishwa na wizi wa
baskeli na matumizi ya bangi lakini walirejeshwa siku ya pili wakiwa
wamefariki.
Amebainisha kuwa mauaji hayo
ni Ukatili dhidi ya binaadamu ambao ni kinyume na Ibara ya 13(6)(e) ya Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Kifungu cha 13(3) cha Katiba ya Zanzibar ya
mwaka 1984. Pia alieleza kuwa mauaji hayo ni Ukiukwaji wa haki ya kuwa huru na
kuishi kama mtu huru kama ilivyotamkwa kwenye Ibara ya 15(1)(2) ya katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Akizungumzia suala la
Utawala Bora, Kamishna Mwinchande amesema, mauaji hayo ni Ukiukwaji wa Msingi
wa Utawala Bora hususan utawala wa Sheria.
Aidha, ameeleza dhamira ya THBUB
ya kufanya uchunguzi wa tukio hilo na kuendeleza uchunguzi kwa matukio mengine
kama hayo, ni kulinda misingi ya utawala Bora na Utawala wa Sheria nchini.
Halikadhalika, Kamishna
Mwinchande ametoa wito kwa wananchi na jamii, kutoa ushirikiano kwa THBUB na
vyombo vyengine vya uchunguzi
vinavyochunguza tukio hilo.
Vilevile ameeleza, THBUB
inawakumbusha wananchi na taasisi zote,
umuhimu wa kupiga vita vitendo vyote
vinavyokiuka Sheria, ukiukwaji wa misingi ya utawala wa sheria na haki za
binadamu, kwa kuwa haki ya kuishi ni haki ya msingi kwa kila mtu.
Kwa upande mwengine ametoa pole
kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu Athuman Hamad Athuman na
Amour Khamis Salim kwa msiba mzito wa kuondokewa na wapendwa wao kwa njia hiyo,
pamoja na kuwaomba wananchi kuwa watulivu na wenye subira hususan wakati huu
ambao vyombo husika vinaendelea na uchunguzi wa matukio ya mauaji.
Marehemu Athuman Hamad
Athuman alifariki dunia akiwa na miaka 75 na Amour Khamis Salim alikufa akiwa
na miaka 28 wote walikuwa wakaazi wa Kimango Kiungoni, Wete Pemba. Waliodaiwa
kukamatwa na maofisa wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupamba na dawa za kulevya
Zanzibar.
IDARA
YA ELIMU KWA UMMA NA MAWASILIANO,
TUME
YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Januari,
2025
“Jukumu
la ulinzi na utetezi wa haki za binadamu ni letu sote”.
No comments:
Post a Comment