Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko (katikati) akizindua Mkakati wa Muda Mrefu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) wa miaka 25 (2024/25 hadi 2049/50) ambao umeweka mipango na malengo makubwa ya kuleta uhakika wa upatikanaji wa
nishati nchini, mkakati ambao utaisaidia nchi kutumia kikamilifu rasilimali za mafuta na gesi zilizopo katika maeneo mbalimbali. Kushoto kwake ni Waziri wa Maji, Nishati na Madini katika Serikali ya Mapiduzi Zanzibar, Shaib Kaduara na kulia kwake ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPDC, Balozi Ombeni Sefue. Wa kwanza kulia ni Mkuu
wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule.
Na.Teresia Mhagama
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameliagiza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuongeza kasi ya uendelezaji wa Vitalu vya utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia ikiwemo Mnazi Bay Kaskazini, Eyasi Wembere, Songo Songo Magharibi na Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia (LNG) ili nchi iendelee kuwa na uhakika wa upatikanaji wa nishati kwa ajili ya soko la ndani na nje.
Ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati akizindua Mkakati wa Muda Mrefu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) wa miaka 25 (2024/25 hadi 2049/50) ambao umeweka mipango na malengo makubwa ya kuleta uhakika wa upatikanaji wa nishati nchini, mkakati ambao utaisaidia nchi kutumia kikamilifu rasilimali za mafuta na gesi zilizopo katika maeneo mbalimbali.
”Tunapozindua Mpango Mkakati huu wa miaka 25, ni muhimu tutambue kuwa jukumu muhimu la TPDC ni kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa nishati nchini. Ni muhimu sisi sote hapa tukumbuke kuwa Sekta ndogo ya Mafuta na gesi ina mchango mkubwa sana katika maendeleo ya Taifa hili.” Amesema Dkt. Biteko.
Aidha, Dkt. Biteko ameiagiza TPDC kuimarisha mtandao wa mabomba na mifumo ya usambazaji wa gesi nchini ikiwemo kupitia teknolojia za Mini-LNG na CNG ili kuwafikia wananchi wengi ambao wapo mbali na Bomba la Usafirishaji wa Gesi Asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam ili kusaidia kuwafikishia watanzania manufaa yatokanayo na matumizi ya gesi asilia.
Pia ameitaka kujiimarisha kifedha ili kuweza kutekeleza miradi mbalimbali kwa kubuni mifumo ya ubunifu ya utekelezaji wa miradi, kuboresha shughuli za kibiashara, na kuendelea kupunguza utegemezi kwa ufadhili wa Serikali ambapo ameipongeza kwa kuanza kujilipa mishahara kwa kutegemea fedha za Shirika.
Vilevile ameitaka TPDC kudumisha uwazi, uwajibikaji, na kuzingatia kanuni za mazingira, jamii, na utawala (ESG) na kufanya kazi kazi kwa karibu na kampuni za kimataifa za nishati, wawekezaji binafsi, na wadau wa maendeleo ili kuvutia mtaji, utaalamu, na teknolojia inayohitajika kwa mafanikio ya mpango uliozinduliwa.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameendelea kusisitiza kuhusu miradi ya Mafuta na Gesi Asilia kutopuuza jamii zinazozunguka miradi hiyo kwani jamii hizo zinapaswa kuona manufaa ya rasilimali zilizopo katika maeneo hayo na wao wakiwa ndio walinzi wakuu wa miradi hiyo ambayo ni
muhimu kwa uchumi wa nchi.
Dkt. Biteko amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya kuendeleza Sekta ya Nishati ambapo kupitia uongozi wake, ametekeleza miradi mingi ikiwemo kukamilisha Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) na kuhakikisha kunakuwa na uhakika wa upatikanaji wa nishati ya mafuta na gesi asilia hapa nchini na hivyo kuleta maendeleo
endelevu ya Taifa na wananchi kwa ujumla.
Kuhusu Nishati Safi ya Kupikia, Dkt. Biteko ameiagiza TPDC kuhakikisha wanalipa kipaumbele suala la nishati hiyo kwa kuendelea kusambaza gesi asilia kwa ajili ya matumizi ya kupikia na hivyo kupunguza hewa ukaa na uchafuzi wa mazingira kutokana na matumizi ya mkaa na kuni.
Pia ameipongeza Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya TPDC pamoja na Kampuni zake tanzu kwa juhudi za kuhakikisha Tanzania inaenda kujipambanua kama kitovu cha nishati ya mafuta na gesi asilia ndani na nje ya Tanzania.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Nishati na Madini katika Serikali ya Mapiduzi Zanzibar, Shaib Kaduara ameeleza kuwa mkakati huo unatoa mwanga wa kukua kwa uchumi wa watanzania na kielelezo cha mafanikio yanayopigwa katika Sekta ya Nishati akisisitiza kuwa amani na umoja ndiyo msingi wa maendeleo.
Aidha, amempongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Dkt. Doto Biteko kwa maendeleo yanayofanyika na kuisimamia vyema Sekta ya Nishati.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema kuwa,kuzinduliwa kwa mpngo huo kunaonyesha jinsi nchi nchi inavyopiga maendeleo kwani mipango ya muda mrefu haishii katika ngazi ya kitaifa tu bali hata katika ngazi za Taasisi ili kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake.
Amesema kuwa kuzinduliwa kwa mpango huo kunatoa mwanga kwa miradi ya
Gesi Asilia kufika maeneo mbalimbali ikiwemo Mkoa wa Dodoma akieleza
kwamba Mkoa upo tayari kupokea miradi ya gesi asilia kwa ajili
matumizi mbalimbali ikiwemo kupikia na kuendesha vyombo vya moto
ikiwemo magari.
Awali Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Maendeleo ya
Petroli Tanzania (TPDC), Balozi Ombeni Sefue alisema kuwa Mpango
Mkakati huo wa muda wa miaka 25 unakwenda sambamba na Ilani ya Chama
cha Mapinduzi kuhusu masuala ya nishati, unalingana kwa karibu na
malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, hasa katika maeneo ya
kuimarisha sekta ya nishati kama kichocheo kikuu cha uchumi wa
viwanda, maendeleo ya miundombinu, kukuza matumizi ya teknolojia
bunifu, kuongeza ajira na mapato ya Serikali, pamoja na kuhakikisha
upatikanaji wa nishati ya uhakika, safi na nafuu kwa Watanzania wote.
“Kwetu sisi, hili siyo andiko tu kama maandiko mengine ya awali bali
ni mwongozo madhubuti wa kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Sita,
inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Nishati ya
kufanikisha upatikanaji na usalama wa nishati na hivyo kuboresha
maisha ya watanzania na kukuza uchumi endelevu.” Amesema Balozi Sefue
Ameeleza kuwa, kupitia Mpango mkakati huo, TPDC inakusudia kuongeza
matumizi ya gesi asilia nchini kutoka matumizi ya kawaida kama
uzalishaji wa umeme, viwandani, kupikia majumbani na nishati mbadala
kwa magari kwenda kwenye matumizi ya kuongeza thamani kama vile
kutumia gesi asilia kama malighafi katika viwanda vya petrokemikali,
ikiwemo uanzishaji wa kiwanda cha mbolea.
Viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo ni Mkuu wa Mkoa wa
Morogoro, Adam Malima Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga,
Wawakilishi wa Wakuu wa Mikoa ya Tanga na Tabora, Wajumbe Kamati
mbalimbali za Bunge wakiongozwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. David Mathayo, Watendaji kutoka
kampuni zinazofanya uwekezaji katika Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia
pamoja na Watendaji wa Wizara ya Nishati na Taasisi zilizo chini ya
Wizara.
No comments:
Post a Comment