Kufunguliwa kwa Tawi la taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume Pemba kutasogeza kwa karibu huduma za masomo ya sayansi na teknolojia kwa wananchi na kutoa fursa kwa vijana kujiendeleza kielimu wakiwa Kisiwani Pemba badala ya kufuata masomo nje ya kisiwa hicho.
Hayo yamesemwa na Mkamu wa Pili wa Rais Mhe. Hemed Suleiman Abdulla wakati akifungua Tawi la chuo cha Sayansi na Teknolojia ya Karume Pemba uliofanyika katika viwanja vya Mnazimmoja Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Amesema Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume inatoa mchango mkubwa katika kukuza taaluma ya Sayansi na Teknolojia ndani na nje ya nchi sambamba na kutoa mafanikio lukuki ikiwemo kuongezeka kwa Wataalamu wa fani ya Sayansi na Teknolojia nchini na Barani Afrika kwa ujumla.
Amesema uwepo wa Tawi hilo kutafungua milango ya kuitangaza Pemba kielimu katika nyanja za sayansi na Teknolojia na kuwavutia watu wengi na kutoa fursa za kiuchumi kwa wananchi kutokana na wanafunzi watakaosoma chuo hicho watahitaji mambo mbali mbali ambayo yatachangia kuleta maendeleo ya kibiashara nakuongezeka kipato kwa wafanyabiashara.
Mhe. Hemed amesema katika kuipa kipaombele sekta ya elimu Serikali kupitia Wizara ya elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, imekuwa ikiboresha sekta ya elimu ikiwemo kuimarisha miundombinu, ubora wa elimu na maslahi ya walimu ambayo yamechangia kupata mafanikio mazuri ya ufaulu kwa wanafunzi wazanzibar.
Aidha, amesema serikali imeongeza bajeti ya Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu Zanzibar hadi kufikia shilingi bilioni 37.5 kwa mwaka wa fedha 2025-2026 ambayo itawanufaisha zaidi ya wanafunzi elf 14 wakiwo wanafunzi wapya na wanaendelea kupatiwa mikopo ambapo na wanafunzi wa ngazi ya diploma watanufaika na kikopo hio.
Sambamba na hayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleo kuimarisha sekta ya elimu kwa kuiongeza bajeti ya Wizara ya elimu hadi kufikia shilingi bilioni 864 kwa mwkaa wa fedha 2025-2026 kwa lengo la kuendeleza mapinduzi ya kielimu nchini ili kuendana na mabadiliko ya kielimu na soko la ajira duniani.
Waziri wa elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Mohamed Mussa amewatoa hofu wakufunzi na wanafunzi wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Pemba kuwa Tawi kubwa na la kisasa litajengwa Kisiwani humo ili kutoa fursa kwa wananfunzi kujisomea vizuri na kwa ufanisi wa hali ya juu.
Waziri Lela amesema Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar itahakikisha chuo cha KIST kinaendela kutoa taaluma yenye ubora na viwango vinavyokubalika vitakavyowawezesha wahitumu wa chuo hicho kuweza kufanya kazi mahala popote duniani.
Aidha Mhe. Lela amewataka wazazi na wananchi kwa ujumla kuitumia fursa ya uwepo wa tawi la KIST kisiwani Pemba kwa kuwasajili vijana wao kujiunga na chuo hicho na kuamini kuwa elimu inayotolewa hapo ni sawa Sawa na elimu inayotolewa katika vyuo vinavyotoa taaluma kama hio nje ya kisiwa cha Pemba.
Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume (KIST) Dkt. Mahmoud Abdulwahab Alawi amesema KIST imejikita katika kutoa mafunzo mbali mbali yanayohusu sayansi na teknolojia yakiwemo pia mafunzo ta muda mfupi ili vijana waweze kujifunza na kufanya kazi zao kwa kujiamini kitaaluma.
Dkt. Mahmoud amesema katika kuunga mkono juhudi za serikali za kuifungua Pemba kiuchumi na kielimu KIST imeamua kufungua Tawi lake Kisiwani Pemba ili kuhakikisha wanatoa fani mbali mbali za sayansi na Teknolojia ambapo kwa sasa wanafunzi 90 wameshajiunga na chuo hicho.
Amesema Tawi la KIST Pemba limenza kutoa mafunzo ya cheti ambapo Uongozi wa Taasisi hio upo katika mchakato wa kuanzisha mafunzo ya ngazi ya Diploma ili kuwawezesha wanafunzi wanaoishi Kisiwani Pemba kujiunga na chuo hicho ili kuwapunguzia gharama za masomo.
Mwenyekiti wa bodi ya Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume (KIST) Dkt. AFWA KHALFAN MOHD amesema kuanzishwa kwa Tawi la KIST Pemba kumeondoa kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Pemba ambao walihitaji kufunguliwa kwa Tawi la chuo hicho ili kuwapunguzia gharama za ada ya masomo pamoja fedha za kujikimu wawapo vyuoni.
Dkt. AFWA amesema kwa sasa Taasisi hio inafanya kazi zake katika jengo la kukodi ambalo halitoshelezi kutoa mafunzo ya ngazi ya cheti hadi diploma kama ilivyo malengo ya chuo hicho, hivyo ameiomba serikali kusaidiwa kupatikana kwa jengo la kudumu ambapo tayari eneo la kutosha lipo kwa ajili ya ujenzi limeshapatikana.
Imetolewa na kitengo cha Habari ( OMPR )
Leo tarehe 16 / 09 / 2025



No comments:
Post a Comment