Na.Mwandishi wa Wizara ya Afya Zanzibar.
WIZARA ya Afya Zanzibar Kupitia Kitengo cha Macho kwa kushirikiana na Shirika la Specsavers wamefanya kambi ya huduma ya Macho pamoja na upimaji wa miwani katika Hospitali ya Kivunge.
Mratibu wa huduma za Macho Wizara ya Afya Zanzibar Dkt.Fatma Juma Omar amesema lengo la kufanya kambi hiyo ni kuhakikisha wananchi wanafikiwa na huduma hizo kwa ukaribu ili kuwapunguzia gharama za kutafuta matibabu maeneo ya mbali.
Amesema tatizo la macho bado limeendelea kuwasumbua wananchi wengi ambapo hadi kufikia sasa asilimia nne ya wananchi wanasumbuliwa na tatizo la macho nchini.
Amesema katika zoezi hilo limekusanya huduma mbalimbali za uchunguzi pamoja na matibabu kwa wagonjwa wenye matatizo ya macho sambamba na kupatiwa miwani kwa watakaohitajia miwani.
Amesema zoezi hilo linatolewa bure kwa wananchi wote watakaofika kwenye zoezi hilo na malengo yao ni kuwahudumia wagonjwa 350 kwa siku.
Kwa upande wake mratibu wa shirika la Specsavers Happiness Urasa Specsavers amesema wagonjwa wengi wanaojitokeza kwenye zoezi hilo ni watoto ambao wanakutwa na tatizo la mtoto wa jicho kutokana na kutokujua jinsi ya kutunza macho vizuri.
Happines ameisa jamii kuweka utaratibu wa kutumia miwani ya jua kwa lengo la kulinda macho dhidi ya tatizo la mtoto wa jicho linalosababishwa na miyonzi ya jua kali.
Wakizungumza mara baaada ya kupatiwa huduma ya vipimo na miwani baadhi ya wananchi wameishukuru serikali kupitia wizara ya afya kwa kuleta zoezi hilo.
Zoezi la upimaji na utoaji wa miwani kwa watu wanaogundulika na matatizo ya macho linafanyika kwa siku nne kwenye hospitali ya kivunge na linalofanywa na shirika la Specsavers kwa ushirikiano na wizara ya afya Zanzibar.
Mwisho.
0 Comments