KAMISHNA wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB),
ofisi ya Zanzibar, Mhe. Khatib Mwinyichande, amewasihi wanasiasa kuzingatia
zaidi na kuweka mbele maslahi ya watu kuelekea uchaguzi mkuu ujao wa Oktoba,
2025.
Kamishna Mwinyichande ameyasema hayo mara baada ya Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar ZEC, kuzindua rasmi kampeni kwa vyama vya siasa, Septemba 12,
2025 kuelekea uchaguzi mkuu.
Katika nasaha zake kwa viongozi wa vyama vya siasa, Kamishna
Mwinyichande amewasihi wanasiasa hao kuzingatia na kuweka mbele maslahi ya watu
kwa kuendeleza amani iliyopo ili kulinda haki za binadamu na utawala bora.
Amesema, Kiongozi anaweza kusema jambo lolote kwa maslahi
yake ya uchaguzi, lakini maneno yake yakawaathiri watu wengi waliomzunguka
na kusababisha uvunjifu wa amani.
"Tume inawasihi viongozi wa siasa wanapopanda katika
majukwaa yao wazingatie maslahi ya watu wengi hasa wanapozungumza, ili
kuimarisha amani iliopo" alisisitiza Kamishna Mwinyichande.
Pia, aliwasihi wanasiasa hao, kutohubiri kauli
zitakazosababisha fujo na kuvunja usalama wa watu, wanapokua kwenye mikutano
yao.
Amesema, mikutano yawanasiasa huhudhuria watu wa rika
tofauti, wakiwemo wazee, watoto na wasiojiweza, hivyo aliwaasa viongozi hao
kuimarisha amani ili kulinda usalama wa watu hao.
"Wanasiasa wanapoanzisha fujo kwenye majukwaa yao kwa
maslahi ya vyama vyao, wataathiri maslahi ya watu wengi wanaowazunguka
kwasababu kuna wazee, watoto na wasiojiweza, hivyo watakiuka misingi ya utawala
bora, na viongozi wa aina hiyo watakuwa hawafai kwenye jamii, kwasababu
wamekiuka misingi ya Utawala bora". Alitanabahisha Kamishna Mwinyichande.

0 Comments