Na Issa Mwadangala.
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Halungu iliyopo Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe, wametakiwa kuelewa na kutambua wajibu wao kama watoto katika jamii kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto.
Hayo yamesemwa Agosti 12, 2025 na Polisi Kata ya Halungu Mkaguzi wa Polisi, Miccah Mtafya, alipotoa elimu kwa wanafunzi wa shule hiyo kwa lengo la kuwajengea uelewa juu ya haki na wajibu wao.
Katika elimu hiyo, Mkaguzi Mtafya aliwafafanulia wanafunzi hao maana ya mtoto kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009 akieleza kuwa mtoto ni mtu yeyote mwenye umri chini ya miaka 18, huku akiwasisitiza kuwa mtoto ana haki za msingi kama vile kupata elimu, malezi bora, na ulinzi dhidi ya unyanyasaji wa aina yoyote.
Vilevile, Mkaguzi Mtafya alieleza wajibu wa mtoto kwa wazazi na kwa walimu akiwa shuleni, ukiwemo kuwatii, kuwaheshimu, na kusoma kwa bidii ili waweze kufaulu mitihani yao, na aliwataka wanafunzi kuwa na nidhamu, kufanya juhudi darasani, na kujiepusha na tabia zitakazowakosesha mafanikio yao ya baadaye.
Mkaguzi Mtafya, alihitimisha kwa kuwaonya kuhusu hatari ya kurubuniwa na wanaume na kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi wakiwa katika umri mdogo, huku akieleza kuwa hatua hizo huweza kuharibu maisha yao ya sasa na ya baadaye, pia aliwaeza madhara ya kiafya, kisaikolojia na kijamii yanayoweza kusababishwa na mahusiano hayo wangali wadogo.

0 Comments