Habari za Punde

Katibu Mkuu Fatma Atembelea Ujenzi wa Mradi Shirika la Magezeti ya Serikali Zanzibar

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Fatma Hamad Rajab, amemtaka mkandarasi anayesimamia ujenzi wa mradi wa Shirika la Magazeti ya Serikali kuongeza kasi ya utekelezaji ili kuweza  kukamilisha kwa  wakati uliopangwa.

Akitoa agizo hilo mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo unaoendelea katika eneo la Tunguu, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja, ambapo alionyesha kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa kazi hiyo. 

Amesema kuwa mradi huo ulipaswa kukamilika mwezi Septemba mwaka huu lakini hadi sasa bado haujakamilika, jambo ambalo haliridhishi kutokana na umuhimu wake kwa Serikali na wananchi wa Zanzibar.

Aidha, Katibu Mkuu huyo amefafanua kuwa kukamilika kwa jengo hilo kutakuwa ni hatua muhimu itakayowezesha uchapishaji wa magazeti na nyaraka muhimu hapa Zanzibar, hatua itakayopunguza gharama kubwa zinazotumika sasa kwa uchapishaji wa magazeti Tanzania Bara. 

Kwa upande wake, Mhandisi kutoka Kampuni inayosimamia mradi huo ya Skywards Construction Company Ltd, Abuu-Bakar Khamis Shaaban, aliahidi kuwa watafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha mradi huo unakamilika ifikapo mwisho wa mwezi Desemba 2025. Alisema hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 84 na miezi miwili pekee imebaki kukamilisha kazi zilizobakia

Amesema licha ya changamoto zilizojitokeza za ucheleweshaji wa vifaa muhimu vya ujenzi jambo ambalo limechangia ucheleweshwaji wa  Ujenzi huo.

Alibainisha kuwa mradi huo unajumuisha majengo matano yakiwemo ofisi, kiwanda cha uchapaji, nyumba mbili za makazi na msikiti. 

Mradi huo uliwekwa jiwe la msingi mwezi Januari mwaka huu na Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Shaib Hassan Kaduara, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.








Imetolewa na Kitengo cha Habari. WHVUM.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.