Makamu wa pili wa rais wa Zanzibar akizungumza na viongozi na watendaji wa Ofisi ya Makamu wa Pili mara baada ya kuwasili ofisini hapo tokea ateuliwe tena kwa mara ya pili kuendelea kuhudumu nafasi hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewataka viongozi na wafanyakazi wa Ofisi ya Makamu wa Pili kuendeleza ushirikiano katika kutekeleza majukumu yao ya kazi za kila siku.
Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na viongozi na watendaji wa Ofisi ya Makamu wa Pili mara baada ya kuwasili ofisini hapo tokea ateuliwe tena kwa mara ya pili kuendelea kuhudumu nafasi hiyo.
Amesema umoja na mshikamano ndivyo vitakavyofanikisha Dira, Miongozo na malengo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Mhe. Hemed amewataka watendaji hao kufanya kazi zao kwa kuzingatia kanuni, sheria, maadili na miongozo iliyowekwa na Tume ya Utumishi Serikalini ili kuweza kufikia malengo ya serikali ya kutoa huduma zilizo bora kwa wananchi wote wa Zanzibar.
Amewasisitiza watumishi hao kuzidi kuimarisha mashirikiano mazuri na Ofisi zote za Serikali ikizingatiwa kuwa Ofisi ya Makamu wa Pili ndio inayosimamia shughuli zote za Serikali.
Makamu wa Pili wa Rais ametumia hadhara hio kumpongeza na kumshukuru Dkt. Hussein Ali Mwinyi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kumuamini na kumteuwa tena ili aendelee kumsaidia katika kufanikisha malengo ya Serikali ya kuwaletea wazanzibari maendeleo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Dkt. Islam Seif Salum amempongeza makamu wa pili kwa kuendelea kuaminiwa na rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuteuliwa kwake na kumuahidi Makamu wa Pili kumpa kila aina ya mashirikiano katika kufanikisha majukumu yake ya kazi na kufikia malengo ya serikali.
Dkt. Islam amesema kuwa uongozi na wafanyakazi wa ofisi ya Makamu wa pili wa rais wana Imani kubwa na yeye katika utendaji wake wa kazi kwani ameonesha ushirikiano mkubwa kwa awamu ya kwanza na watahakikisha wanaendeleza pale palipobakia ili kufika malengo ya serikali ya kuwaletea maendeleo wananchi wake wote.
Wakati huo huo wasaidizi wa Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais na wafanyakazi wa Ofisi ya Faragha walimkabidhi Mhe. Hemed tunzo ya pongezi kwa kuteuliwa tena kushikilia wadhifa wake huo kwa kipindi cha pili katika Serikali ya awamu ya nane.

Imetolewa na kitengo cha Habari ( OMPR )



No comments:
Post a Comment