Elimu ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma ni Muhimu Hasa Kwa Waajiriwa Wapya ili Kubaini Faida za Mifuko

 Naibu Katibu Mtendaji Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Bw. Juma Msafiri Karibona, akizungumza katika kikao na maofisa wa tume hiyo pamoja na maofisa kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar, (ZSSF) (hawapo pichani) wakati ZSSF ikiwapa elimu ya mafao hivi karibuni ofisi za THBUB zilizopo Mombasa Kiembesamaki, Wilaya ya Magharibi B Mkoa wa Mjini Magharibi.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Elimu kwa Umma wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar, (ZSSF) Bi. Raya Hamdan (wa kwanza kulia) akiwapa elimu ya mafao yanayotolewa na mfuko huo, Watumishi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (hawapo pichani), hivi karibuni ofisi za THBUB zilizopo Mombasa Kiembesamaki, Wilaya ya Magharibi B Mkoa wa Mjini Magharibi

NA MWASHAMBA JUMA, THBUB                                                                                              

Naibu Katibu Mtendaji Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Bw. Juma Msafiri Karibona, amesema elimu ya mifuko ya hifadhi ya jamii kwa watumishi wa umma ni muhimu hasa wa waajiriwa wapya ili kubaini faida za mifuko hiyo kwa lengo la ustawi bora wa watumishi hao.

Ameyasema hayo ofisi za THBUB, Mombasa alipozungumza na maofisa wa ofisi hiyo wakati wakipewa elimu ya Mafao kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) siku chache zilizopita.

Amesema, lengo la kuwapatia elimu watumishi hao ni kuwajengea uelewa baadhi ya wanachama wa mfuko huo na ambao sio wanachama wa ZSSF.

“Tukipata elimu hasa ikatujengea uelewa itatusaidia kutufumbua macho na kufahamu mengi tusiyoyajua” alifafanua Karibona.

Akizungumza na watumishi hao, Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano na elimu kwa umma kutoka ZSSF, Bi. Raya Hamdan Khamis aliyatambulisha mafao sita yanayotolewa na mfuko huo nakueleza namna yanavyowanufaisha wanachama wa mfuko huo.

Akitaja mafao hayo kwa wanachama wanachangia mfuko huo, wakiwemo watumishi wa sekta za Umma na binafsi, Bi. Raya alieleza fao la uzeeni ambalo mwanachama wa ZSSF atanufaika nalo akifikia hatua za kustaafu kisheria kwa kufikia umri wa kustaafu kwa hiari au kwa lazima, fao la Uzazi, fao la kuumia kazini, fao la kupoteza ajira na fao la elimu ambalo aliwashauri wanachama wa mfuko huo na ambao sio wanachama kufungua fao hilo kwa kujiwekea akiba kwa ustawi wa elimu kwa watoto wao.

Bi. Raya pia alizitaja kazi zinazofanywa na ZSSF, amesema ni pamoja na kusajili wafanyakazi wa taasisi mbalimbali, kukusanya michango, kuwekeza katika miradi salama na nyenye tija na kulipa mafao kwa wanachama wao ambao ni kiini kikuu cha kuanzishwa mfuko huo.

ZSSF ilianzishwa miaka 28 iliyopita kwa lengo la kulipa mafao kwa wanachama wake mbali na majukumu mengine yaliyoainishwa na Mkuu wa kitengo cha mawasiliano na elimu kwa umma. 

 Watumishi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), wakimfuatilia kwa makini Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Elimu kwa Umma wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar, (ZSSF) Bi. Raya Hamdan (hayupo pichani) wakati akiwapa elimu ya mafao yanayotolewa na mfuko huo, hivi karibuni ofisi za THBUB zilizopo Mombasa Kiembesamaki, Wilaya ya Magharibi B Mkoa wa Mjini Magharibi.

Post a Comment

0 Comments