Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar Mhe. Riziki Pembe Juma ameiagiza Idara ya Utamaduni Zanzibar na Baraza la Sanaa, Sensa ya Filamu na Utamaduni kuendelea kusimamia Mila,silka na Utamaduni wa Zanzibar.
Ameyasema hayo, katika Ukumbi wa Studio Rahaleo wakati wa majumuisho ya ziara yake kutembelea Idara ya Utamaduni, Baraza la Sanaa, Sensa ya Filamu na Utamaduni (BASSFU), Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA) na Baraza la Taifa la Michezo (BTMZ).
Amesema iwapo Watumishi wanaweza kulinda Mila silka na tamaduni za kizanzibar kutasaidia kulinda asili ya Zanzibar na Taifa kwa ujumla.
Aidha amewataka Viongozi wa Taasisi hizo, kuzipa kipaumbele changamoto zilizopo sambamba na kusisitiza nidhamu na uadilifu katika utekelezaji wa majukumu ya Kazi zao.
Hata hivyo ameliagiza Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKIZA) kuelimisha matumizi sahihi ya lugha ya kiswahili ili iwe ni chanzo ya kupata fursa za Ajira kwa jamii na kukuza Uchumi wa Nchi.
Kwa Upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mattar Zahour Masoud amewataka Watumishi hao, kujenga mashirikiano ya pamoja sambamba na kuongeza Ari ili kuleta ufanisi wa kazi.
Amesema Iko haja ya kuyatengeneza mazingira mazuri ya wafanyakazi ili kuweza kufanyakazi Kwa ufanisi mkubwa.
Nao wafanyakazi wa Taasisi hizo ambazo zipo chini ya Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo wameeleza changamoto zinazowakabili ikiwemo ufinyu wa nafasi, uhaba wa vitendea kazi, Rasili Mali watu na Usafiri.
Imetolewa na kitengo cha Habari,
WHSUM.


.jpg)

0 Comments