Hot Posts

6/recent/ticker-posts

SADC yakabiliwa na Pengo kubwa la mawasiliano ya sayansi


 Na Veronica Mrema, Pretoria.

Wakati dunia ikikimbiza mageuzi ya teknolojia—kutoka akili bandia (AI) hadi tiba bunifu—ukanda wa SADC bado unakabiliwa na changamoto kubwa: taarifa za sayansi na ubunifu hazimfikii mwananchi kwa kasi inayohitajika.

Mkurugenzi Mkuu wa Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Sayansi ya Afrika Kusini (DSTI), Mwampei Chaba, amesema nchi nyingi za SADC hazina mkakati mahsusi wa mawasiliano ya sayansi, hali inayowafanya waandishi kukosa taarifa, ushirikiano kutoka serikalini na hata fursa za ufadhili.
Akizungumza kwenye mdahalo wa waandishi wa sayansi kutoka nchi 18 za SADC, ulioungana na Mkutano wa Kimataifa wa Waandishi wa Habari za Sayansi (WCSJ2025), Chaba alisisitiza kuwa bila mawasiliano mazuri, sayansi haiwezi kuonekana wala kuthaminiwa na jamii.

“Sayansi inapaswa kuelezeka kwa mtoto wa miaka 5 na mtu wa miaka 85,” alisema, akitoa wito kwa waandishi kuwasukuma wanasayansi kutumia lugha nyepesi na inayoeleweka.

Amesema Afrika inahitaji waandishi mahiri wa sayansi kuliko wakati mwingine wowote, na anaamini vipaji hivyo vinaweza kutoka ndani ya SADC endapo kutakuwa na ushirikiano wa kimkakati.

Chaba pia amehimiza matumizi ya mitandao ya kijamii—TikTok, YouTube na Instagram—kufikisha maudhui ya kisayansi kwa vijana wengi waliopo kwenye majukwaa hayo.

Kwa mara ya kwanza Afrika inaandaa WCSJ, na warsha hiyo inalenga kuimarisha uwezo wa waandishi kuibua, kueleza na kuhamasisha masuala ya sayansi ndani ya jamii.

Post a Comment

0 Comments