Na.Omar Abdallah - Wizara ya Afya Zanzibar.
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
kupitia Wizara ya afya Zanzibar imetoa maelekezo ya kanuni mpya kuhusu
usimamizi na uchakataji wa taka za hospitali, ikiwa ni hatua muhimu ya kuhakikisha
usalama wa wananchi na usafi wa mazingira katika maeneo yote ya huduma za afya.
Maelekezo hayo yametolewa na
mkugenzi kinga na elimu ya afya Zanzibar Dr salim Slim wakati akizungumza katika
mkutano maalum wa uhamasishaji na
usambazaji wa kanuni za usimamizi wa taka amesema Wizara ya Afya imetangaza
rasmi kuanza kwa matumizi ya Kanuni za
Usimamizi wa Taka za Afya za mwaka 2025, chini ya Sheria ya Afya ya Umma na
Mazingira Na. 11 ya mwaka 2012. Kwa mujibu wa kanuni hizo zimeanzishwa kwa
lengo la kuimarisha usimamizi wa taka zinazotokana na huduma za afya, ikiwa ni
pamoja na taka hatarishi, taka laini na taka ngumu zinazozalishwa hospitalini,
vituo vya afya, maabara na maeneo mengine ya huduma za tiba.
Wizara ya afya tayari wameeka
makubaliano na Kampuni Wels co limited
ambao wanaohusika na ukusanyaji wa taka hizo wameanza kazi rasmi ya
kuzichukua kutoka hospitali mbalimbali. Taka hizo zitapimwa, kurekodiwa,
kuchakatwa na kufikishwa katika maeneo maalum yaliyotengwa kwa ajili ya
kuziteketeza kwa usalama.
Serikali imeeleza kuwa hakuna hospitali itakayoruhusiwa kutupa taka
kiholela, kwani taka za kitabibu ni miongoni mwa taka hatarishi
zinazoweza kusababisha maambukizi na madhara makubwa ya kiafya endapo
hazitashughulikiwa kwa utaratibu sahihi.
Aidha, imeelezwa kuwa maelekezo
haya yanaweza kuleta mabadiliko na usumbufu kwa baadhi ya wananchi,
ikizingatiwa kwamba taka hizo mara nyingi hukutwa katika maeneo ya makazi na
katika shughuli za kijamii Hata hivyo, serikali imesisitiza kuwa afya na usalama wa wananchi ndiyo kipaumbele
cha msingi.
Wadau wote husika, wakiwemo
wasimamizi wa hospitali, taasisi za usafi na makampuni ya ukusanyaji taka,
wametakiwa kuzingatia maelekezo hayo na kuhakikisha taka za kitabibu
zinachakatwa bila kuleta usumbufu wala hatari kwa wananchi.
Serikali itaendelea kufuatilia kwa
ukaribu utekelezaji wa maelekezo haya ili kuhakikisha mazingira yanabaki kuwa
safi na salama kwa wote.
Mkuu wa kitengo cha afya Mazingira
Mlenge Hisan Mlenge amesema Taka zote za hospitali za binafsi na serikeli zinatakiwa zikusanywe kwa kufanyiwa uchambuzi
ili kuweza kurahisisha uchakataji wa taka hizo
Nae Mkurugenzi wa kampuni ya Wels co Ltd Grangay Nyanghura amesema kanuni
hiyo inawasaidia kuongeza ufanisi wa kuhakikisha wanaweza kukusanya na kudhibiti taka katika maeneo yote ya
uzalishaji wa taka hatarishi.
0 Comments