Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Dkt. Islam Seif Salum ambaye ni Mwenyekiti akiongoza kikao cha ushirikiano baina ya Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, ngazi ya Makatibu Wakuu kilichofanyika Zanzibar leo Februari 16, 2026. Kulia ni Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan Mitawi.
Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar zimefanya kikao cha ushirikiano kwa
ajili ya kujadili masuala mbalimbali ya Muungano na yasiyo ya Muungano, leo
Februari 16, 2026, Zanzibar.
Kikao hicho ngazi ya Makatibu Wakuu kimepokea na kujadili taarifa
ya maandalizi ya kikao maalumu cha Kamati ya Pamoja kinachotarajiwa kufanyika
mwaka huu.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Dkt. Islam
Seif Salum ambaye ni Mwenyekiti ameongoza kikao hicho pamoja na Mwenyekiti
Mwenza ambaye ni Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan
Mitawi.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Dkt. Salum alisisitiza
watendaji kutoka Serikali ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania (SJMT) na Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuendeleza ushirikiano ambao utaendelea
kuimarisha Muungano.
Alisema Serikali zote mbili zinaweza kuimarisha ushirikiano huo
kupitia sekta mbalimbali kwa mfano Uchumi wa Buluu ambao tayari SMZ imeanzisha
Wizara mahsusi ya kusimamia na kwa upande wa SJMT Ofisi ya Makamu wa Rais ina
kitengo maalumu cha usimamizi wa sekta hiyo.
“Niwaombe tu wataalamu wenzetu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar
tuendeleze ushirikiano katika Sekta ya Uchumi wa Buluu ili kuona namna gani
utanufaisha wananchi,” alisema.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu Mitawi alisema Ofisi ya Makamu
wa Rais imeanza mazungumzo na Wizara ya Fedha ya Jamhuri ya Muungano ili
uhakikisha ikiwezekana kupata mafunzo maalumu kuhusu utoaji wa elimu ya
Muungano.
Alisema suala la utoaji wa elimu ni la kimkakati hivyo, nguvu
kubwa imewekezwa katika kuhakikisha mkazo unatiliwa katika utoaji wa elimu ili
kutowapa nafasi wapotoshaji wa Muungano.
Bw. Mitawi pia, alitoa wito kwa watendaji kutoka pande zote mbili
za Muungano kutanua wigo wa ushirikiano kwa kuzungumzia agenda zingine
zinazogusa Tanzania Bara na Zanzibar.
“Sio mbaya tukiwa na watu wa Manunuzi na idara mbalimbali kama
Utumishi, Sheria, Mazingira na Uchumi wa Buluu mkikutana na kuzungumzia fursa
zen uau changamoto zenu na kushirikiana katika kuzifanyia kazi,” alisema.
Katika kikao hicho wajumbe wamepokea taarifa ya Mpango Kabambe wa
Elimu kwa Umma kuhusu Muungano ambao utatumika katika kuelimisha wananchi
kuhusu historia, misingi, faida na fursa mbalimbali za Muungano.
Sanjari na hilo pia, iliwasilishwa tarifa ya maendeleo ya mifumo
ikiwemo Mfumo wa Uratibu wa Shughuli za Serikali na Mfumo wa uratibu wa Masuala
ya Muungano na yasiyo ya Muungano.
Kikao hicho ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea kikao cha
ushirikiano baina ya Ofisi ya Makamu wa Rais na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais
ngazi ya Mawaziri. 
Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya
Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan Mitawi ambaye ni Mwenyekiti Mwenza
akizungumza wakati wa kikao cha ushirikiano kati ya Ofisi ya Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,
ngazi ya Makatibu Wakuu kilichofanyika Zanzibar leo Februari 16, 2026.
Wajumbe wakifuatilia kikao
cha ushirikiano kati ya Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, ngazi ya Makatibu
Wakuu kilichofanyika Zanzibar leo Februari 16, 2026.
Wajumbe wakifuatilia kikao
cha ushirikiano kati ya Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, ngazi ya Makatibu
Wakuu kilichofanyika Zanzibar leo Februari 16, 2026.

0 Comments