Habari za Punde

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora yatoa tamko kuhusu zuio la Jeshi la Polisi la Mikutano na Maandamano ya Vyama vya Siasa

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Bahame Tom Nyanduga akiwa ameambatana na Kamishna wa Tume, Mhe. Ali Rajab (kushoto) na Katibu Mtendaji wa Tume, Bibi Mary Massay (kulia) akisoma tamko la Tume kuhusu zuio la polisi la mikutano na maandamano ya vyama vya siasa mbele ya vyombo vya habari leo (Agosti 10, 2016) mchana. Mkutano huo na vyombo vya habari ulifanyika Makao Makuu ya ofisi za Tume, Mtaa wa Luthuli jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wanahabari wakimsikiliza Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Bahame Tom Nyanduga akitoa tamko la Tume kuhusu zuio la polisi la mikutano na maandamano ya vyama vya siasa mbele ya vyombo vya habari leo (Agosti 10, 2016) mchana.
(Picha zote na Getrude Alex wa THBUB)

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Kitalu Na. 8, Mtaa wa Luthuli
S.L.P 2643, DAR ES SALAAM
Simu: +255 22 2135747/8; 2137125; 2135222
Faksi: +255 22 2111281
Barua Pepe: chragg@chragg.go.tz
Tovuti: www.chragg.go.tz

Agosti 10, 2016


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
                                
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, iliandaa mkutano leo tarehe 10/08/2016 ili kuzungumzia tamko la Jeshi la Polisi la tarehe 07/06/2016 la kuzuia mikutano na maandamano ya vyama vya siasa isiyo ya kiutendaji, na tamko la CHADEMA kuhusu “UKUTA” na mikutano wanayopanga kufanya tarehe 1 Septemba, 2016.

Mkutano huu ulihudhuriwa pia na Mhe. Jaji Francis Mutungi, Msajili wa Vyama vya siasa, Mhe. Vincent Mashinji, Katibu Mkuu wa CHADEMA na washauri wake na Ndugu Daniel Loya,  Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Demokrasia nchini (TCD).

Hivyo mkutano wa leo ulikuwa na lengo la kuwakutanisha viongozi wa Serikali, Jeshi la Polisi na CHADEMA na kwa pamoja kutafuta ufumbuzi wa kile Tume inachohofia kuhusu uvunjifu wa amani, haki za binadamu na utawala bora.

Aidha baada ya tamko la CHADEMA la kufanya maandamano nchi nzima, kumekuwa na matamko mbalimbali kutoka kwa viongozi wa kitaifa, baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya, Makamanda wa mikoa wa Jeshi la Polisi kukataza kufanyika kwa maandamano hayo na kwamba watakaokiuka zuio hilo “watashughulikiwa.”

Ni katika mazingira haya, Tume imepata wasiwasi kuwa endapo matamko haya yataachiwa yaendelee, yana viashiria vya machafuko na uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu unaoweza  kutokea. 

Mkutano huu kwa pamoja ulitaka kujihakikishia iwapo Tume ina mamlaka ya kujadili hoja hizo mbili yaani kujadili zuio la maandamano na mikutano ya vyama vya siasa, visiyokuwa vya kiutendaji na kuhusu lugha na matamshi yasiyo stahiki.

Baada ya majadiliano Tume inapenda kutamka yafuatayo:-
1.    Wajumbe wote waliohudhuria kikao hicho walikubaliana kuhusu umuhimu wa kudumisha amani nchini, na umuhimu wa kuwepo majadiliano katika kutafuta maafikiano ya tofauti zozote kila mara zinapojitokeza, na walipendekeza umuhimu wa kuendelea na majadiliano yaliyoanzishwa na Tume.

2.    Kwamba kuhusiana na mustakabali wa maandamano na mikutano ya vyama vya siasa ilibainika kuwa kuna kesi mbili zilizofunguliwa na CHADEMA katika Mahakama Kuu, Masijala ya Dar es Salaam na Mwanza na kesi zote zinaendelea.  Kwa kuzingatia Ibara ya 131 (2)(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, inaamini kwamba, tafsiri sahihi ya zuio lilitolewa na Polisi litapatikana Mahakamani.  Tume inaamini Mahakama itayapa mashauri hayo kipaumbele, kama ilivyofanya wakati wa kusikiliza kesi ya mita mia mbili hapo Oktoba, 2015 ili tafsiri yake ipatikane mapema.

3.    Pamoja na uamuzi huo wa Tume, kwa kuzingatia mamlaka ya Tume chini ya Ibara 130 (1) (g) na (h) ya Katiba ya nchi, kuhusu kutoa ushauri na kutafuta maelewano kati ya viongozi wa Serikali na Jeshi la Polisi kwa upande mmoja, na uongozi wa CHADEMA, Tume inawaasa viongozi wa pande mbili kuzingatia yafuatayo:-
(i)           Kusitisha matumizi ya lugha au maneno yenye viashiria vya uvunjifu wa amani, haki za binadamu na utawala bora kwani lugha hizi hazikidhi matakwa ya haki za binadamu, wala utawala wa sheria.

(ii)          Jeshi la Polisi linashauriwa lisitumie neno “tutawashughulikia wote watakao kaidi amri”, kwa kuwa Tume inaona kuwa maneno hayo yanaweza kusababisha matumizi mabaya ya mamlaka ya Jeshi la Polisi.

(iii)        CHADEMA warekebishe msamiati wa mikutano wanayopanga na kuondoa neno “UDIKITETA” katika mikakati yao ya kisiasa kwani Tanzania, ni nchi yenye taasisi za kidemokrasia na inaheshimu utawala wa Sheria, na ndiyo sababu CHADEMA wamekwenda Mahakamani.

(iv)        Kwa kuzingatia, ukweli kwamba kuna mashauri mawili yaliyoko Mahakamani, ambayo yatawezesha Mahakama kutoa tafsiri ya uhalali wa zuio la Jeshi la Polisi la tarehe 7 Juni, 2016 kuhusu maandamano na mikutano ya vyama vya siasa, Tume inashauri kwamba, pande zote mbili ziheshimu Mahakama na ziache kutoa matamko ambayo yanaendelea kuongeza joto kuhusu uwepo au kutokuwepo maandamano na mikutano ya tarehe 1 Septemba, 2016.

(v)         Tume inaishauri CHADEMA kusitisha maandamano yake ili kutoa nafasi kwa Mahakama kufanya kazi yake kwa umakini bila shinikizo la muda kati ya sasa na tarehe 1 Septemba, 2016.

Iwapo ushauri huu hautazingatiwa, Tume inatahadharisha kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kuwepo na uvunjifu wa haki za binadamu na iwapo itatokea hivyo wahusika wote pia itabidi wawajibike.

Imetolewa na:

(SIGNED)

Bahame Tom Nyanduga
                                                   Mwenyekiti

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA


Agosti 10, 2016

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.