Social Icons

zantel

pbz

Featured Posts

Thursday, July 24, 2014

Dk Shein azindua mradi wa SAEMAUL UDONG Cheju

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK.ALi Mohamed Shein akipata maelezo kutoka Naibu katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maliasili Nd,Juma Ali Juma wakati alipotembelea kituo cha kukausha Embe Dodo katika Kijiji cha Cheju kibonde maji leo  kilichojengwa na Shirika la misaada la Koika nchini Korea kupitia    Mradi wa  SAEMAUL UDONG   .[Picha na Ramadhan Othman Ikulu.]
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK.ALi Mohamed Shein na Balozi wa Korea Bw.IL Chung (katikati) wakiangalia embe zilizokaushwa zikiwa katika Mpango maalum wa kuhifadhiwa  wakati alipotembelea kituo cha kukausha Embe Dodo katika Kijiji cha Cheju kibonde maji leo kilichojengwa na Shirika la misaada la Koika nchini Korea kupitia Mradi wa  SAEMAUL UDONG   .[Picha na Ramadhan Othman Ikulu.]  
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK.ALi Mohamed Shein na Balozi wa Korea Nchini Tanzania Bw.IL Chung (katikati) wakiangalia embe zilizokaushwa zikiwa katika Mpango maalum wa kuhifadhiwa  wakati alipotembelea kituo cha kukausha Embe Dodo katika Kijiji cha Cheju kibonde maji leo  kilichojengwa na Shirika la misaada la Koika nchini Korea kupitia Mradi wa SAEMAUL UDONG   .[Picha na Ramadhan Othman Ikulu.]  
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK.ALi Mohamed Shein(katikati) na Balozi wa Korea Nchini Tanzania Bw.IL Chung wakipata maelezo kutoka Naibu katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maliasili Nd,Juma Ali Juma (kulia) wakati alipotembelea mitambo katika kituo cha kukausha Embe Dodo katika Kijiji cha Cheju kibonde maji leo kilichojengwa na Shirika la misaada la Koika nchini Korea kupitia  Mradi  SAEMAUL UDONG   .[Picha na Ramadhan Othman Ikulu.]  
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK.ALi Mohamed Shein akibadilishana mawazo na  na Balozi wa Korea Nchini Tanzania Bw.IL Chung mara baada ya kutembelea  kituo cha kukausha Embe Dodo katika Kijiji cha Cheju kibonde maji leo kilichojengwa na Shirika la misaada la Koika nchini Korea kupitia  Mradi  SAEMAUL UDONG   .[Picha na Ramadhan Othman Ikulu.]

SMZ yazuia kiwanja cha watoto kutumika Sikukuu Idd El Fitr

Na Rahma Suleiman
 
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema kiwanja cha kufurahisha watoto kilichopo eneo la Kariakoo, mjini Unguja, hakitatumika katika Sikukuu ya Idd El Fitr, mwaka huu, kutokana na ujenzi wake kutokamilika.

Akizungumza baada ya kufanya ziara ya kukagua kiwanja hicho, Waziri wa Fedha, Omar Yussuf Mzee, alisema dhamira ya serikali ni kuona kiwanja kinakamilia mapema lakini kumejitokeza changamoto za kiufundi.

Alisema pamoja na bembea zote 12 kukamilika, baadhi ya maeneo yanaendelea kufanyiwa matengenezo, ambayo yatachukua zaidi ya miezi miwili kukamilika kwake.

Mzee alisema hata kama kiwanja hicho kitafunguliwa kwa muda kwa ajili ya sikukuu inayoanza mwanzoni mwa wiki ijayo, kutakuwa na wasiwasi wa usalama, kwani hata milango mikuu haijawekwa.

Kaimu Mkurugenzi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) inayowekeza katika mradi huo, Khamis Filfil Thani, alisema matumaini yake kuwa ifikapo Sikukuu ya Idd El Hajj, mwaka huu, kiwanja hicho kitakuwa tayari kutumika.

Rais Kikwete afutarisha Wete PembaBaadhi ya waumini wa Dini ya Kiislamu pamoja na wananchi wa Mikoa miwili ya Pemba wakifutari pamoja hapo ikulu ya Wete futari iliyoandaliwa naRais wa Jamuhuri ya Mauungano wa Tanzania Dr. Jakaya MrishoKikwete akawakilishwa kwa niaba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ,h. Mohd Aboud Mohd kati kati akiwa pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Mh. Dadi Faki Dadi kulia yake na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba Mzee Mberwa Hamad Mberwa wakijumuika na wananachi wa mikoa miwili ya Pemba kwenye futari iliyoandaliwa na Rais wa Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akitoa shukrani kwa niaba ya Rais wa Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania Dr. Kikwete mara baada ya futari ya pamoja kwa wananchi wa mikoa miwili ya Pemba

Mandhari ya mji wa Beijing


 MJI wa Beijing ukioneka pichani ukiwa umepamba na msafara wa magari wakati wa jioni leo kama unavyooonekani pichani.
 
WAANDISHI wa Habari na Maofisa Habari kutoka Nchi 11 za Afrika   wakiwa nje ya jengo la Makumbusho la Red Sandalwood Museum Beijing, wakati wa mapumziko ya Semina yao ya Wiki mbili nchini China.  

 
 MTEMBEZA wageni wanaotembelea Makumbusho ya Red Sadalwood Beijing Bi Rose Sun, akitowa maelezo ya  sana za kale zilioko katika makumbusho hiyo ya Red Sadalwood, kwa Jopo la Waandishi kutoka Afrika walipotembelea jingo hilo kujionea  mapambo mbalimbali yaliokuwa yakitumika Nchini China
MTEMBEZA wageni wanaotembelea makumbusho hiyo akitowa maelezo ya meza iliotengenezwa kwa mti wa Sadalwood ikiwa katika makumbosho hiyo. Akiwaeleza waandhi wa habari walipofika kujuonea  sanaa za asili zilizokuwa zikitumika miaka ya zamani nchini China.
 

Sakata la wanafunzi kufundishwa bibilia


Wizara ya Elimu yachukua hatua

Uchunguzi wabaini ukweli wa madai hayo

Na Khamisuu Abdalla

SIKU mbili tu baada ya gazeti hili kuchapisha habari kuhusu wanafunzi kusomeshwa bibilia na kutakiwa kutokwenda skuli wakiwa wamefunga, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, imefanya uchunguzi na kubaini kwamba tuhuma hizo ni za kweli.

Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake Majestik, Mrajisi wa Elimu Zanzibar, Siajabu Suleiman Pandu, alisema baada ya uchunguzi kufuatia habari, waligundua malalamiko ya wazazi ya wanafunzi ni ya kweli.

Alisema alipohojiwa, mmiliki wa skuli hiyo inayoitwa Eden International,Pilsoon Youn (maarufu mama Kim), alikiri kwamba anatoa elimu ya bibilia kwa wanafunzi.

Alisema katika kuta za madarasa kumebandikwa vipande vya aya za bibilia  ambavyo vinathibitisha kwamba bibilia inasomeshwa.

Hata hivyo, alisema bibilia inafundishwa huku idadi kubwa ya wanafunzi wanaosoma katika skuli hiyo ni Waislamu.

Sita wafa ajilini


Na Said Abdulrahman, Pemba

WATU sita wamefariki dunia katika matukio mbali mbali za ajali  yaliyotokea mkoa wa kaskazini Pemba, kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake, Mkuu wa kitengo cha usalama barabarani mkoani humo, Khalid Ali Gulam, alisema vifo hivyo vilisababishwa na ajali sita ambapo mbili zilitokea wilaya ya Micheweni na nne wilaya ya Wete.

Aidha alisema katika ajali hizo watu 19 walijeruhiwa wakiwemo wanawake wanane.

Alisema katika kipindi hicho polisi walifanya operesheni 10 na kukamata vyombo 132 vikiwa na makosa mbali mbali.

Tanzania mwenyeji mkutano mabunge MadolaNa Joseph Ngilisho,Arusha

TANZANIA itakuwa mwenyeji wa mkutano mkuu wa 45 wa Umoja wa Wabunge wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola,kanda ya Afrika (CPA), utakaofanyika Julai 24 hadi 26 mwaka huu,jiji Arusha.

Aidha mkutano huo utatanguliwa na vikao mbali mbali kikiwemo cha kamati tendaji,mkutano wa umoja wa wanawake wa jumuia hiyo,mkutano wa Makatibu wa Mabunge na vikao vya kanda za mashariki,magharibi,kusini na Afrika ya kati,vitakavyoanza leo.

 

Akizungumza na vyombo vya habari Rais wa CPA ambaye pia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Anne Makinda,alisema bunge la Tanzania limepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo utakaofunguliwa na Rais Jakaya Kikwete na kwamba nchi 18 wanachana zinatarajia kuhudhuriwa,huku washiriki wapatao 500 wakitarajiwa kushiriki.

Wednesday, July 23, 2014

Dadi akerwa na uchafu MtemaniNa Masanja Mabula,Pemba
SERIKALI ya mkoa wa kaskazini Pemba, imeelezea kusikitishwa na uchakavu wa makaro katika nyumba za maendeleo Mtemani wilaya ya Wete na kuagiza taasisi husika kuyafukia ili kuepusha uwezekano wa kutokea maradhi ya mripuko.

Mkuu wa Mkoa huo, Dadi Faki Dadi, alitoa agizo hilo wakati akizungumza na watendaji wa Wizara ya Majenzi, Baraza la mji Wete,Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na Shirika la Umeme Pemba.

Alisema ni vyema taasisi hizo kushirikiana pamoja na kuyafukia makaro hayo ambayo yamekuwa yakitiririsha maji machafu yenye vinyesi vya binadamu.

"Hili ni tatizo na linatakiwa kuchukuliwa hatua za haraka ili kunusuru afya za  wakaazi wa nyumba hizi kupata maradhi ya mripuko,”alisema.

Mkuya:Afrika inashikilia hatma ya duniaNa Mahmoud Ahmad, Arusha
WAZIRI wa Fedha, Sada Mkuya,amezitaka nchi za Afrika kutambua kwamba bara lao ndilo linalotupiwa macho na dunia kuwa sehemu yenye uhakika wa maisha  yao ya siku za usoni.

Aidha alisema  Afrika ni kituo kikubwa cha shughuli zote za uchumi wa dunia kutokana na kuwepo kwa rasilimali ambazo bado hazijatumika.

Alisema hayo alipokuwa akifungua mkutano wa wadau wa kodi za ndani kwa nchi za Afrika, unaoendelea  jijini Arusha  lengo likiwa ni kubadilishana mawazo, uzoefu na namna ya ukusanyaji wa kodi kwa maendeleo ya nchi washirika.

Alitaja baadhi ya rasilimali zilizogundulika kuwa ni pamoja na gesi asilia na mafuta yanayotarajiwa kuanza kupatikana miaka michache ijayo.

Alisema kutokana na hali hiyo nchi za bara hilo zinapaswa kujitambua na kuweka miundombinu mizuri itakayowezesha kuvunwa rasilimali hizo kwa faida ili ziwanufaishe na kinua uchumi wa nchi zao.

Kesi mauaji ya Donge yashindwa kusikilizwaNa Khamis Amani
KWA mara nyengine tena, kijana Abdallah Mohammed Kangoma (38) mkaazi wa Donge Mtambile wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja, aliyeshitakiwa kwa kumuua mkewe, Msikitu Juma Ali anaendelea kusota rumande baada ya upelelezi wa kesi hiyo ukiwa bado haujakamilika.

Hayo yamebainika mbele ya Mrajisi wa mahakama kuu, George Joseph Kazi, wakati mshitakiwa huyo alipofikishwa mahakamani hapo kuendelea na kesi ya mauaji inayomkabili.

Mshitakiwa aliwasili mahakamani hapo akitokea rumande ya chuo cha mafunzo kilichopo Kilimani mjini Unguja.

Mshitakiwa alirejeshwa tena rumande hadi Julai 31 mwaka huu atakapofikishwa tena mahakamani.

Abdallah Mohammed Juma alidaiwa kumuua kinyama mke wake kwa kumkata kwa mapanga kwa shaka ya wivu, tukio ambalo lilitokea Donge Mtambile Oktoba 3 mwaka jana majira ya saa 12:00 za asubuhi.

Alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Oktoba 9 mwaka jana na kusomewa shitaka la kuua kwa makusudi kinyume na vifungu vya 197 na 197 vya sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar.

Dk. Karume ahimiza walimu, wazazi kushirikianaNa Bakar Mussa, Pemba
RAIS mstaafu wa awamu ya sita, Alhaj Dk. Aman Abeid Karume, amewataka wazazi kuongeza ushirikiano na walimu wa madrasa ili kuwaendeleza watoto katika kuhifadhi na kusoma Quran.

Alisema bila ya ushirikiano lengo la kuendeleza mbele juhudi zinazochukuliwa na waalimu wa madrasa za kuendeleza dini hiyo hazitazaa matunda.

Aliyasema hayo katika msikiti wa Ijumaa wa Miembeni Chake Chake kisiwani Pemba,wakati akizungumza na walimu, wazazi na wanafunzi, walioshiriki mashindano ya kuhifadhi Quran ambapo alikuwa mgeni rasmi.

Fedha za TASAF si za anasa, kaya maskini zaambiwaNa Haji Nassor, Pemba
FAMILIA maskini kisiwani Pemba, ambazo zinawezeshwa kifedha na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) awamu ya tatu, zimekumbushwa kuwa fedha wanazopatiwa sio kwa ajili ya kununulia madira na sare za harusini na badala yake wazitumie kwa kujikwamua na umaskini.

Kauli hiyo imetolewa na Muwezeshaji wakati wa ugawaji wa fedha hizo, shehia ya Ndagoni wila

Kamishna wa Polisi Z’bar, DCI waburuzwa mahakamaniNa Mwandishi wetu
KAMISHNA wa Polisi Zanzibar, Hamdan Omar Makame na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Zanzibar (DCI), Salum Msangi, wamefunguliwa kesi mahakama kuu ya Zanzibar, baada ya watu wanane waliokamatwa wakihusishwa na matukuo ya miripuko kuwekwa kizuizini kwa muda mrefu bila kufikishwa mahakamani.

Kesi hiyo namba 7 ya mwaka 2014 imepangwa kuanza kusikilizwa kesho mbele ya Jaji wa mahakama kuu, Mkusa Issack Sepetu.

Washtakiwa hao tayari wametakiwa kujibu hati za kiapo kabla ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa.

Kesi hiyo imefunguliwa na Wakili Abdallah Juma Mohamed akishirikiana na Rajab Abdallah Rajab kutoka kampuni ya uwakili ya AJM Solicitor ambao wanataka mahakama kuwaita viongozi hao ili waeleze mahali walipo wateja wanane wanaowatetea tangu walipokamatwa katika maeneo na nyakati tofauti visiwani Zanzibar.

Kwa mujibu wa hati hiyo ya kiapo, watu hao ambao wanadaiwa kukamatwa na kuwekwa kizuizini ni Nassor Ahamad Abdallah, Mohamed Ishaq Yussuf, Said Kassim Ali, Hassan Bakari Suleiman, Rashid Ali Nyange Antar Homuod, Khamis Salum Amour na Salum Ali Salum.

Imani za kishirikina zakamwisha miradi ya maji ChembaNa Fatina Mathias,Chemba

KATIKA hali isiyo ya kawaida, imani za kishirikiana katika baadhi ya maeneo ya halmashauri ya Chemba mkoani Dodoma, zimetajwa kuwa ni chanzo cha kukwamisha utekelezaji miradi ya maji na umeme kufuatia wakandarasi kukumbana na vioja mbali mbali ikiwemo nyoka kila wanapochimba.

Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, katika zoezi la kutia saini mikataba ya ujenzi wa mifumo ya usambazaji maji katika vijiji vitano vya wilaya hiyo.

Alisema wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo wanakumbana na hali hiyo kila wanapofukua  mashimo ya kuweka nguzo za umeme kutoa nyoka badala ya mchanga na kwa upande wa maji  maji mabomba yanapasuka muda mfupi baada ya kufukiwa ardhini kwa madai kuwa wakandarasi hao hawajawashirikisha wazee wa kimila kabla ya miradi kuanza.

Aliwataka wakandarasi  kuhakikisha wanawaona wazee wa vijiji hivyo ili kuepuka matukio kama hayo kuendelea kujitokeza na hivyo kuchelewesha maendeleo kwa wananachi.

“Mambo ya kimila jamani ni muhimu naomba tuyafuate ili tuondokane na hali hii, wewe mkandarasi ukawakusanye wazee wa eneo husika unawanunulia mbuzi na pombe ili wafanye tambiko uweze kufanikiwa
katika utekelezaji wako,”alisema.

JK:Hatutapigana na MalawiNa Mwandishi wetu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, amesema kamwe Tanzania haitatumia nguvu kumaliza mvutano kati yake na Malawi kuhusu mpaka kati ya nchi hizo.

Aidha, Rais Kikwete alisema Tanzania haioni matinki ama busara yoyote kuingia vitani na nchi yoyote jirani kwa sababu yoyote ile.

Alitoa uhakikisho huo wakati alipohutubia mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na mamia ya wananchi kwenye uwanja wa michezo wa mjini Mbamba Bay, mji mkuu wa wilaya mpya ya Nyasa.

Aliwambia wananchi hao: "Nataka kuwatoeni wasiwasi. Hakuna sababu ya vita. Laleni usingizi bila wasiwasi, kuleni samaki wenu kwa sababu Tanzania haioni busara ya vita."

"Tanzania haiwezi kutumia nguvu kupata suluhisho la mvutano wa mpaka.Tuna uwezo wa kupata jawabu la tatizo hilo bila kutumia njia ya vita.Tanzania haioni busara hiyo ya vita. Tuna uwezo wa kupata ufumbuzi kwa njia ya madiliano. Na wala msimamo huo siyo kwa mpaka wetu na Malawi pekee bali kwa mipaka yote ya Tanzania," alisema.

Baadhi ya makosa yanayotokea wakati wa kutoa Zakaatul Fitr


Abu Ammaar

Baadhi ya makosa yanayotokea wakati wa kutoa Zakaatul Fitr

1     Kuitoa wakati wa Sala ya Idd, siku ya Idd yenyewe.

Zakaatul Firtr hupaswa kutolewa mapema ili iwafikie walengwa waliokusudiwa. Ikitolewa wakati wa Sala hukosa ile dhamira iliyokusudiwa ya kuwalisha maskini na wenye kuhitaji na kuwafika kwa wakati.
Ni Sunna ikatolewa siku moja au mbili kabla ya siku ya Idd. Baadhi ya Maulamaa wamejuzisha kutolewa hata kabla ya hapo ikiwa itakuwa na manufaa zaidi na kuweza kuwafika wahusika kwa wakati.

 2  Kuisafirisha kuipeleka sehemu nyengine bila ya dharura

Hasa ndugu zetu hupenda kupeleka Zakaatul fitr nchi walizotoka au huenda Misikitini na kuweka katika masanduku yaliyoandikwa Zakaatul Fitr wakidhani tayari wameshatekeleza wajibu.
Asli ya Zakaatul Fitr ni kutumika sehemu inayotolewa kama kuna wanaostahiki na wanahitaji. Kama hakuna hapo inajuzu kuisafirisha kuipeleka sehemu nyingine na huwajibika kwa mwenye kuitoa kwa njia hii kuhakikisha kwamba aliowapa ni watu thika wanaoaminika na ni kweli wataifikisha kwa wahusika kabla ya siku ya Idd.

Vyenginevyo bado mtoaji atakuwa na dhimma kwa Zakaah hii ikiwa haikuwafika walengwa katika muda unaotakiwa

3    Kutoitoa kabisa
Baadhi ya ndugu zetu katika dini wanadhani kutoa Zakaatul Fitr si wajibu au si lazima hiyo wakiitoa sawa na kama hawakuitoa pia ni sawa.
Zakaatul Fitr ni wajibu kwa kila Muislamu aliyeshuhudia mfungo wa Ramadhaan. Kama haikutolewa hiyo ni dhambi kubwa na mas’uuliyah (jukumu) kwa mhusika na atakwenda  kuulizwa na Mola wake. Hutolewa na mwenye kuisimamia familia na huwatolea wote wanaomtegemea katika familia yake. 
4    Kuchanganya kati ya Zakaatul Fitr na Zakaatul Maal
Baadhi ya ndugu zetu hawaoni tofauti kati ya Zakaah ya mali na Zakaatul Fitr hivyo hujiweka katika kundi la kwamba hawana sifa ya kuitoa.

Dk Shein ashiriki futari iliyoandaliwa na Makamo wa Rais Dk Bilal

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (wa pili kushoto) akijumuika na Waislamu na Viongozi mbali mbali katika futari iliyoandaliwa na Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Mohamed Gharib Bilali jana katika viwanja vya Ofisi ya Makamo Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja,(wa kawanza Kushoto) Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Omar Kabi   [Picha na Ramadhan Othman Ikulu.] 
 Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Mohamed Gharib Bilali akimkaribishaRais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein jana alipowasili katika futari aliyowandalia wananchi mbali mbali na Viongozi katika viwanja vya Ofisi ya Makamo Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja,[Picha na Ramadhan Othman Ikulu.] 
 Wananchi walioalikwa katika futari iliyoandaliwa na Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jana katika viwanja vya Ofisi ya Makamo Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja,wakijumuika kwa pamoja.[Picha na Ramadhan Othman Ikulu.] 
Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Mohamed Gharib Bilali ,Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein pamoja na Viongozi na wananchi wakijumuika katika swala ya Magharibi jana kabla ya futari iliyoandaliwa na jana   katika viwanja vya Ofisi ya Makamo Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja, [Picha na Ramadhan Othman Ikulu.] 


Zakaatul Fitr - Umeshatekeleza wajibu wako?

Abu Ammaar

Zakatul Fitri , ambayo pia hujulikana kama Sadaqatul Fitri , kilugha inatokana na neno la kiarabu fitri na  maana yake ni kula  au futari kama inavyojulikana.

Katika sheria ni ile sadaqa inayotolewa mwishoni  mwa mwezi wa Ramadhan na kabla ya kusaliwa Eid na kupewa wanaostahiki.

KUFARADHISHWA KWAKE

Zakatul Fitri ni wajibu kwa kila muislam awe mwanamke au mwanamme ,mkubwa au mdogo ,almuradi ana uwezo wa kuitoa au kutolewa kwa niaba yake ikiwa yuko anaemuangalia.

Dalili ya kufaradhishwa kwake ni  Hadithi ya Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam kutokana na  ‘Abdullah Ibn  ‘Umar, Allah awawie radhi(yeye na baba yake), kwamba  Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam amesema :

 Amefaradhisha Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam Zakatul Fitri katika Ramadhaan kwa kila mtu miongoni mwa waislamu huru na mtumwa, mwanamke na mwanamme, mdogo na mkubwa kutoa  pishi moja ya tende au pishi moja ya uwele, Na akaamrisha kutolewa kabla ya watu kutoka kwenda kusali (Eid)

                                                           Imepokewa na Bukhari

Kwa mujibu wa hadithi hii, Zakatul Fitri itabidi itolewe kwa waislamu wa aina zote bila ya kujali hali, jinsi na mazingira ya muislamu husika pindi uwezo ukiruhusu na huyu muislamu kuushuhudia mwezi mtukufu wa Ramadhan.Uwezo unaokusudiwa ni kwa muislamu kuweza kuwa na vya kujitolesheza katika siku ya eid na bado kuwa na cha ziada.

Kwa hivyo kama muislamu ni mwenye jukumu la kuwahudumia wengine kwa mahitaji yao ya lazima basi ni wajibu kwa mtu huyo pia kuwatolea wale wote ambao wako chini ya jukumu lake katika kuwahudumia. Hii ni kutokana na  ufafanuzi uliotolewa na Sahaba Abu  Saeed Al Khudhriy ,Allah amuwie radhi, pale aliposema -:                                                                          

“Tulikuwa tukitoa enzi za Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam  pishi  moja ya nafaka au pishi moja ya tende au pishi moja ya uwele au pishi moja ya zabibu.”                                     

                                         Imepokewa na  Bukhari na Muslim

Picha na matukio kutoka Pemba

 
KATIKA Kamishna wa tume ya taifa ya uchaguzi NEC, John Mkawawa, akizungumza na waandishi wa habari kisiwani Pemba, juu ya uimarishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa kutumia teknologia mpya ya ‘BVR’ kutoka ile ya zamani ya OMR, mkutano huo ulifanyika hoteli ya hifadhi Chakechake Pemba (picha na Haji Nassor, Pemba)

 
AFISA kutoka wizara ya ardhi, makaazi, maji na nishati Pemba bw Salim, akiwasilisha mada kwenye mafunzo ya kuzielewa sheria za ardhi kwa wasaidizi wa sheria wa majimbo ya Pemba, mafunzo yalioandaliwa na ‘ZLSC’ na kufanyika afisini kwao mjini Chakechake Pemba (picha na Haji Nassor, Pemba)

 
MWANAHARAKATI wa asasi za kiraia Pemba, Juma Bakari Alawi ‘JB’ akiwafahamisha wanajumuia ya mendeleo ya wanawake wa kijiji cha Tundauwa ‘JUMATU’ wilaya ya Chakechake, namna ya kujaza fomu za tathimini, baada ya kumaliza mradi wa haki za binaadamu na utawala bora, mkutano huo ulifanyika skuli ya Kilindi (picha na Haji Nassor,Pemba)

 
WANAFUNZI wa chuo cha elimu na biasahara Zanzibar ‘ZCBE’ wakiwa darasani kuanza mwana mpya wa masomo, ambao umezunduliwa juzi na mkuu wa chuo hicho Abdull-wahabi Said Bakari, hafla iliofanyika chuoni hapo Vitongoji wilaya ya Chakechake Pemba (picha na Haji Nassor, Pemba)

Tuesday, July 22, 2014

Semina ya Waandishi na Maofisa wa Habari yafanyika nchini China

 MAOFISA Habari na Waandishi kutoka Nchi za Afrika zinazozungumza Kiigereza wakimsikiliza wakisikiliza Mada ya kuhusu Maendeleo ya Nchi ya China kutoka kwa  Deputy Administrator of China Foreing Languages Publishing Administration. Ndg. Huang Youyi, akitowa mada yake katika Semina hiyo ya Wiki Mbili inayofanyika katika ukumbi wa hoteli ya 21st Century Beijing China(Picha na Othman Maulid) 

WAANDISHI habari wakimsikiliza Mkurugenzi Ndg Ding Xiaoming, akifungua mafunzo hayo ya Wiki Mbili Mjini Beijing China leo 22/7/2014
Mada ya kuhusu Maendeleo ya Nchi ya China ikitolewa na Deputy Administrator of China Foreing Languages Publishing Administration. Ndg. Huang Youyi, akitowa mada yake katika Semina hiyo ya Wiki Mbili inayofanyika katika ukumbi wa hoteli ya 21st Century Beijing China(Picha na Othman Maulid) 


MKURUGENZI wa Kituo cha Mafunzo cha cha Baraza la Taifa (SCIO) Ndg. Ding Xiaoming, akifungua Semina ya Maofisa wa Habari na Waandishi wa habari wa Nchi za Afrika zinazozungumza lugha ya Kiingereza, ufunguzi wa Semina hiyo umefanyika katika ukumbi wa hoteli ya 21st Century Beijing,leo na kuwashirikishwa waandishi wa nchi za Afrika 10 .(Picha na Othman Maulid)

Sala na Baraza la Iddi el Fitr 1435/2014

KUH: SALA NA BARAZA LA IDDI EL FITRI 2014
 
Kwa heshima naomba uhusike na mada ya hapo juu.
Swala ya Iddi El Fitri inatarajiwa kuswaliwa 1:00 asubuhi katika viwanja vya Maisara siku ya Jumatatu tarehe 28 au Jumanne ya tarehe 29 Julai 2014 itategemea na kuandama kwa mwezi.
Iwapo itanyesha Mvua itaswaliwa katika Mskiti wa Mwembe-Shauri .
 
 Aidha, Baraza la Iddi linatarajiwa kufanyika siku hiyo hiyo saa 4:00 za asubuhi katika ukumbi wa Salama, Hoteli ya Bwawani
Mgeni Rasmi katika shughuli hizo za Sala na Baraza la Iddi anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dkt. Ali Mohamed Shein.
 
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR

Uzinduzi wa mpango wa elimu kwa wananchi kuhusu kuanzishwa kwa sheria ya Biashara Zanzibar

 Katibu Mkuu Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar Julian Raphael akimkaribisha Waziri Mazrui (hayupo pichani) azungumze na wandishi wa Habari katika sherehe ya uzinduzi wa mpango wa elimu kwa wananchi kuhusu kuanzishwa kwa Sheria ya Biashara Zanzibar No. 14 ya mwaka 2013 katika Hoteli ya Grand Palace Malindi Mjini Zanzibar.
 Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Mhe. Nassor Ahmed Mazrui akizungumza na wandishi wa Habari (hawapo pichani) juu ya uzinduzi wa mpango wa elimu kwa wananchi kuhusu kuanzishwa kwa sheria ya Biashara Zanzibar No. 14 ya mwaka 2013. Sherehe hiyo imefanyika Hoteli ya Grand Palace Malindi Mjini Zanzibar.
 Mwandishi wa Habari Abdallah Pandu wa Star tv akiuliza swali juu ya uanzishwaji wa sheria hiyo.
 Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Mhe. Nassor Ahmed Mazrui akijibu maswali ya wandishi wa Habari (hawapo pichani), kulia Naibu Waziri wake  Thuwaiba Edington Kisasi na (kushoto) Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Julian Raphael.
Baadhi ya wandishi wa Habari waliofika katka sherehe ya uzinduzi wa mpango wa elimu kwa wananchi kuhusu kuanzishwa kwa sheria ya Biashara Zanzibar No. 14 ya mwaka 2013 wakifuatilia maelezo ya Waziri Mazrui (hayupo pichani) Sherehe hiyo iliofanyika Hoteli ya Grand Palace Malindi Mjini Zanzibar .
(Picha na Makame Mshenga -Maelezo Zanzibar).

Balozi Seif afutarisha mkoa wa Kusini Unguja

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akijumuika na wananachi wa Mkoa wa Kusini Unguja katika futari ya pamoja hapo katika Ofisi ya Idara ya Uhamiaji Tunguu Wilayha ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.

Kulia ya Balozi Seif ni Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Dr. Idriss Muslim Hija na Mkuu wa Wilaya ya Kati Nd. Vuai Mwinyi wakati upande wa kushto yake ni Mkuu wa Wilaya ya Kusini Nd. Haji Makungu Mgongo.
 Baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Kusini UInguja wakifutari  pamoja na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisi za Uhamiaji Tunguu.
 Baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Kusini UInguja wakifutari  pamoja na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisi za Uhamiaji Tunguu.
 Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Dr. Idriss Muslim Hija akiwashukuru wananchi wa Mkoa huo waliohudhuria futari ya pamoja kwa niaba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.

Kushoto ya Dr. Idriss ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif wakati upande wake wa kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kati Nd. Vuai Mwinyi.
 Diwani wa Wadi ya Koani Wilaya ya Kati Nd.Shaaban Jabu Kitwana akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja kwa kumpongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kuwaandalia futari ya pamoja.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiagana na Wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja mara baada ya kufutari nao pamoja hapo Ofisi za Ohamiaji Tunguu.

Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.