MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali (WEMA) imeteleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa wa kupigiwa mfano.
Hemed ameyaeleza hayo kwenye ufunguzi wa kongamano lililoandaliwa na Shirikisho la Walimu Zanzibar, kwa ajili ya kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, lililofanyika katika ukumbi wa skuli ya Utaani iliyopo Wete Pemba.
Amesema katika kipindi cha miaka mitano, WEMA imesimamia vyema miundombinu ya ujenzi wa miundombinu ya elimu, ambapo jumla ya skuli 36 za ghora kwa ngazi ya msingi na sekondari katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar zimejengwa.
Ameeleza kuwa skuli hizo zimejengwa za kisasa zikiwa na majitaji yote ya kufundishia na kujifunzia ikiwemo maabara za kisasa za masomo ya sayansi, maktaba, vyoo, vyumba vya kompyuta, sambamba na kufanyika kwa mgao wa vitabu vya kusomea na kufundishia zaidi ya milioni tatu kwa skuli zote.
Mhe. Hemed amesema moja ya sababu iliyochangia kuongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi kwenye mitihani ya taifa, ni ujenzi wa wa miundombinu ya kisasa ya elimu ambayo kimsingi imesimamiwa na wizara hiyo.
Mhe. Hemed alizitaja jitihada nyengine zilizochukuliwa na serikali ya awamu ya nane ni pamoja na kuongeza ajira za walimu kufikia 3,531 mwaka 2025, kuongezeka bajeti ya bodi ya mikopo ya elimu ya juu shilingi bilioni 33.4 mwaka 2025.
Amefamisha kuwa idadi ya wanafunzi wa kike wanaosoma masomo ya sayansi imeongezeka na kufikia 3,409 mwaka 2025 na kukamilika kwa majengo 21 ya dakhalia Unguja na Pemba, huku mengine 14 yanaendelea na ujenzi yakiwa katika hatua mbalimbali.
Makamu wa Pili wa Rais, amesema serikali inaendelea na ujezi wa miundombinu katika sekta mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara, bandari, viwanja vya ndege, afya, elimu, uchumi wa buluu na mengineyo ikiwa na lengo la kuweka ustawi bora kwa wananchi wa Zanzibar.
Sambamba na hayo, Makamu wa Pili wa Rais aliwataka wanachama wa Shirikisho hilo na wazanzibari kwa ujumla kushirikiana katika suala la maendeleo kwa maslahi ya wazanzibari.
Aliwasisitiza wananchi kuendelea kudumisha amani, kuimarisha upendo, ushirikiano na mshikamano mambo ambayo yamekuwa nyenzo muhimu katika mafanikio yaliyopatikana.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ametumia fursa hiyo kuipongeza Wizara ya Elimu na walimu wa Zanzibar kwa jitihada kubwa wanazozichukua katika kuwapatia elimu watoto na malezi watoto wa Zanzibar.
Kwa upande wake, waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Muhammed Mussa, amesema Shirikisho la Walimu linaishukuru serikali ya awamu ya nane kwa kuipa hadhi sekta ya elimu, kuimarisha miundombinu ya elimu sambamba na kuwaangalia kwa karibu walimu na watendaji wa wizara ya Elimu.
Waziri Lela amesema kutokana na kipaombele walichopewa walimu na serikali ya awamu ya nane, walimu wameahidi kuwapigia kura wagombea wote watakao simamishwa na Chama cha Mapinduzi katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Akisoma risala ya Shirikosho la Walimu Zanzibar, Khamis Othman alisema lengo la kongamano hilo ni kurejesha shukurani kwa Dk. Samia Suluhu Hassan na Dk. Hussein Mwinyi kwa hadhi waliyoipandisha kwa sekta ya elimu na walimu.
Mwalimu Khamis amesema serikali ya awamu ya nane imelipa kipaombele suala la upandishwaji wa mishahara kwa walimu, kuimarishwa kwa mazingira ya kusomea na kufundishia, kuondolewa ada kwa wanafunzi ambapo wanasoma bila ya malipo.
Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
Tarehe 01.07.2025
No comments:
Post a Comment