Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Amefungua Mkutano 31 wa Shirika la Viwango Afrika (ARSO) : Viwango ni Mihimu kwa Kukuza Biashara na Masoko ya Kimataifa


 


Na Fauzia Mussa

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema usimamizi madhubuti wa viwango vya bidhaa ni kichocheo kikuu cha kukuza biashara na kufikia masoko ya kimataifa. 

Akiizungumza wakati akimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kufungua mkutano wa 31 wa Shirika la Viwango Afrika (ARSO), uliofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Golden Tulip, Hemed alisisitiza kuwa viwango ni msingi wa ubora, usalama na ushindani wa bidhaa.

Aidha Hemed alibainisha dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Katika kuimarisha taasisi za viwango ili kusaidia ustawi wa biashara ndani na nje ya nchi.

“Upatikanaji wa viwango bora si tu unalinda afya na usalama wa watumiaji, bali pia unasaidia bidhaa zetu kufikia masoko ya nje. Hii ni fursa kwa wajasiriamali wetu wadogo na wa kati, ambao ndio uti wa mgongo wa uchumi wetu,” alisema Hemed.

Alisisitiza kuwa viwango vina mchango mkubwa katika kukuza usalama wa watumiaji, kulinda mazingira, na kuimarisha ushindani wa bidhaa za Afrika sokoni. 

Sambamba na hayo alihimiza kuwepo kwa mifumo ya pamoja ya viwango barani Afrika kupitia taasisi kama Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS), na Umoja wa Viwango Afrika (ARSO).

 Hemed aliipongeza ARSO kwa juhudi zake za kuimarisha miundombinu ya viwango Afrika na kuwataka washiriki wa mkutano huo kuweka mkazo katika kubuni mifumo itakayosaidia kukuza ushindani wa viwanda vidogo na vya kati, hasa katika soko la pamoja la Afrika (AFCFTA).

Kwa upande wake, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omar Said Shaaban, alisema kuwa Zanzibar ina mpango wa kuanzisha maabara ya kisasa ya viwango itakayosaidia kuhakiki ubora wa bidhaa na huduma, pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa viwango na wadau wa sekta ya biashara.

“Leo hii, viwango vya ubora si hiari tena. Ni lazima kwa bidhaa zote zitakazoshindana katika soko la kimataifa. Tunajipanga kuhakikisha bidhaa kutoka Zanzibar zinakidhi mahitaji ya kimataifa,” alisema Shaaban.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dk. Ashura Kantunzi, alisisitiza umuhimu wa mkutano huo kwa bara la Afrika, akisema unatoa nafasi ya kutafakari namna bora ya kuboresha mazingira ya biashara kwa kuwasaidia wazalishaji, hasa wale wa biashara ndogo na za kati, kwa kuwapunguzia vikwazo vya viwango na kuwajengea uwezo.

“Tunatambua kuwa biashara ndogo na za kati ndizo injini ya uchumi. TBS na ZBS tunao mpango maalum wa kuwasaidia kwa mafunzo, miongozo rahisi ya viwango, na kuwahakikishia kuwa faida za soko huru zitawanufaisha moja kwa moja,” alisema Dk. Ashura.

Mkutano huo wa siku kadhaa unakusanya wadau kutoka nchi mbalimbali za Afrika kujadili mustakabali wa viwango barani Afrika, huku Zanzibar ikitazamiwa kufungua ukurasa mpya wa ubora, usalama na ushindani wa bidhaa katika soko la dunia.

 






No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.