Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Mgeni Rasmin Maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar

Makamu wa Pili wa Rais  wa Zanzibar akizungumza viongozi mbali mbali, mabaharia na wadau wa Sekta ya Bahari katika hafla ya ufungaji wa maadhimisho ya siku ya mabaharia duniani yaliyofanyika Kitaifa Zanzibar katika Ukumbi wa Sheikh Idris Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar.

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema serikali zinatambua na kuthamini mchango unaotolewa na mabaharia katika sekta ya bahari na maendeleo ya nchi.

Ameyasema hayo katika hafla ya maadhimisho ya siku ya mabaharia duniani yaliyofanyika kitaifa visiwani Zanzibar iliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idris Abdulwakil uliopo Kikwajuni mjini Zanzibar.

Amesema kwa kuzingatia umuhimu na mchango unaotolewa na mabaharia, serikali zinaendelea kuchukua juhudi mbali mbali za kutawisha kada ya mabaharia ikiwemo kuwa na sera na mipango ambayo itaiwezesha sekta hiyo kuwa na mchango wa maendeleo nchini.

Mhe. Hemed amefahamisha kuwa serikali imejipanga katika kuhakikisha maslahi ya mabaharia yanalindwa kwa kuridhia mkataba wa kimataifa ya kazi za baharini wa mwaka 2006 ambao utakuwa tiba kubwa ya changamoto nyingi zinazowakabili mabaharia hapa Tanzania.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, amesema serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia shirika la Uwakala wa Meli la Tanzania (TASAC), imekamilisha mfumo wa utoaji wa vyeti kwa njia ya kielektroniki kwa mabaharia.

Amesema mfumo huo utasaidia kutoa vyeti vinavyoendana na matakwa ya sasa ya shirika la bahari duniani na shirika la kazi duniani ambavyo vitaondoa uwezekano wa kughushi vyeti jambo litakalosaidia kuwafanya mabaharia kutambulika.

Aidha,  Mhe. Hemed amefahamisha kuwa serikali imenunua boti maalumu ya kisasa ya matibabu (Modern Ambulance Boat), yenye vifaa vya uokozi, huduma za dharura za afya na matibabu katika Ziwa Victoria.

Sambamba na hayo, Makamu wa Pili wa Rais amempongeza Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kuridhia kuanzishwa chuo cha mabaharia hapa Zanzibar, ambacho kitakuwa na chachu kubwa ya maendeleo ya fani ya ubaharia itakayoongeza idadi ya vijana kupata nafasi ya kujifunza masomo hayo.

Kadhalika amesema serikali imeweka sera nzuri za uwekezaji ambazo zimepelekea kuwepo kwa Chuo cha Mafunzo ya Ubaharia Zanzibar kinachomilikiwa na kampuni ya Danaos ambacho kinaratibu na kuendesha mafunzo mbali mbali ya ubaharia ili kukuza ufanisi wakazi zao melini na kutoa ajira kwa mabaharia wa Kitanzania katika meli za nje.

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Mhe.Dkt Khalid Salum Muhammed  amesema wanatambua kuwa kazi ya Ubaharia ni kazi ngumu yenye changamoto mbali mbali ikiwemo kuhatarisha maisha yao, kukaa muda mrefu katika meli hasa meli zi azofanyq safari zake nje ya nchi sambamba kukosa muda wa kutosha kwa ajili ya familia zao.

Dkt. Khalid amesema Serikali inaendela na jitihada za kuweka miundombinu imara ya usafiri na usafirishaji, kuzifanyia marekebisho sera na miongozo ya usafiri wa Baharini pamoja na  matumizi ya Teknoloji  itakayowezesha  utambuzi wa haraka wa  changamoto zinazojitokeza baharini.

Nae Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar ndugu Mtumwa Said Sandal amesema Serikali imeridhia mikataba mbali mbali ya Kimataifa inayowahakikishia mabaharia kufanya kazi zao wakiwa salama kwa kuzingatia itunzaji wa mazingira ya bahari pamoja na kuzingatiwa maslahi yao ipasavyo.

Sandal amesema kufuatia siku ya mabaharia duniani, Shirika la Bahari duniani(IMO) limesisitiza umuhimu wa usalama kwa mabaharia katika utendaji wa kazi zao na kuwataka wasimamizi wa mabaharia kuhakikisha wanapatiwa maslahi yao pamoja na mafunzo ya mara kwa mara kutokana na mabadiliko ya Teknolojia duniani ili nao waweze kuendana na mabadiliko hayo.

Amesema IMO imezinduq kampeni ya kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia katika kazi za ubaharia kwa mabaharia wanawake pamoja na kuwajengea uwelewa mabaharia wanawake juu ya kutoa taarifa kwa vitendo vya udhalilishaji wanavyokumbana navyo.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
Tarehe 25.06.2025

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.