Na Miza Kona/Rahma Khamis Maelezo-Zanzibar
Jumla ya wanafunzi 16,744 wamechaguliwa kuendelea masomo ya kidatu cha tatu kati ya wanafunzi 24,051 walioandikishwa kufanya mtihani wa kidato cha pili katika skuli za Unguja na Pemba mwaka jana.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa Habari Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Ali Juma Shamhuna amesema kiwango hicho cha ufaulu ni sawa na asilimia 69.6 ikiwa ni ongezeko la asilimia 4.0 ukilinganisha na matokeo ya mwaka jana.
Waziri Shamhuna amesema idadi ya wanafunzi wa kike waliofaulu ni kubwa zaidi ukilinganisha na wanaume ambapo wanawake ni 9,794 na wanaume 6,950.
Kwa upande wa matokeo ya Darasa la saba Waziri Shamhuna amesema jumla ya wanafunzi 24,235 kati ya wanafunzi 30,179 walioandikishwa wamechaguliwa kuingia kidato cha kwanza sawa na asilimia 84.5, wanafunzi 51 wamechaguliwa kujiunga na madarasa ya vipawa na wanafunzi 621 wamechaguliwa kujiunga na madarasa ya michepuo
Akitoa tathmini kwa wanafunzi wa Darasa la sita Waziri wa Elimu amesema kuwa jumla ya wanafunzi 25,773 wamechaguliwa kuiungia kidato cha kwanza sawa na asilimia 99.6 ambapo wanafunzi 44 wamechaguliwa kujiunga na madarasa ya vipawa.
Akitaja Skuli zilizofanya vizuri zaidi kidato cha pili Waziri Shamhuna amesema ni pamoja na Madungu ‘A’, Mauwani na Mahonda . Darasa la saba ni Skuli ya Alikhamis Camp, Mjimbini na Kangani na darasa la sita ni Kibweni, Mkunazini na Konde.
Amezitaja Skuli zilizofanya vibaya kitaifa kwa kidato cha pili ni Mfurumatonga, Uzi, na Mchangani, skuli ya Chambani, Kandwi , Mwambe shamiani, Mfurumatonga, Chambani na Mahonda wamefanya vibaya darasa la sita na saba .
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali amesema katika mitihani hiyo kesi nne za udanganyifu zilijitokeza zote kwa wanafunzi wa darasa la sita.
Aliwataja wanafunzi waliofanya vizuri zaidi kidato cha pili ni Philip William Panduka kutoka Skuli ya Mikunguni, darasa la saba ni Farid Ali Hamad kutoka Ziwani na darasa la sita ni Seif Khamis Nassor kutoka Skuli ya Madungu ‘A’.
Waziri Shamhuna amewataka wazazi na walezi wa wanafunzi ambao hawakufaulu mitihani hiyo kutovunjika moyo na badala yake amewashauri kuwapeleka vituo vya kujiendeleza.
Waziri huyo wa Elimu ameahidi kufanya utafiti na kuzifuatilia skuli zilivyofanya vibaya ili kuweza kufahamu tatizo na kulitafutia ufumbuzi unaofaa.
matokeo ya wanafunzi wengine yanapatikana wapi?
ReplyDeleteRukiaali950@gmail.com
Delete