6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAISHUKURU UNEP KWA MRADI WA KUHIMILI MABADILIKO YA TABIANCHI

Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bi Mwanasha Tumbo, akizungumza jambo wakati wa kikao cha kufunga shuguli za utekelezaji wa Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) kilichofanyika Desemba 15,2025

Serikali imelishukuru Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) kwa kuendelea kuiwezesha Tanzania kutekeleza miradi ya uhifadhi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

Shukrani hizo zimetolewa Desemba 15, 2025 na Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Bi. Mwanasha Tumbo wakati wa kikao cha kufunga shughuli za utekelezaji wa Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia MIfumo Ikolojia Vijijini (EBARR).

Bi. Mwanasha amesema UNEP imekuwa mshirika wa karibu na Tanzania katika kuwezesha utekelezaji wa miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi hatua iliyoiwezesha Serikali kutekeleza miradi mbalimbali katika halmashauri nchini.

“Tunaishukuru UNEP kwa kufanikisha hatua na mafanikio ya utekelezaji wa Mradi wa EBBAR, jambo zuri tunalojivunia na Serikali itahakikisha miradi iliyoanzishwa kupitia EBBAR inafikia malengo yake” amesema Bi. Mwanasha.

Ameongeza kuwa Serikali itahakikisha miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi iliyoanzishwa katika Halmashauri zote nchini kupitia EBBAR inakuwa endelevu na kuleta matokeo chanya katika jamii inayozunguka.

Bi. Mwanasha amesema, Serikali itahakikisha inafanya ufuatiaji wa karibu katika miradi hiyo iliyoanzishwa ili kuhakikisha wananchi wananufaika ipasavyo na kuimarisha mfumo wa usimamizi katika ngazi za halmashauri na vijiji.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) nchini, Bi. Clara Makenya amesema Shirika hilo linajivunia ushrikiano wake na Tanzania na kuwa ipo tayari kuendelea na ufadhili wa miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

“Mradi wa EBBAR ni miongoni mwa miradi ya mfano iliyogusa na kubeba maslahi mapana maisha ya jamii. UNEP ipo tayari kuhakikisha changamoto zote zinazogusa mazingira na mabadiliko ya tabianchi zinafanyiwa kazi na kupata majibu stahiki” amesema Makenya.

Amesema mazingira ni sekta mtambuka inayogusa makundi mbalimbali ya kljamii ikiwemo wanawake na hivyo ni wajibu wa wadau wote kuhakikisha walengwa wa miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi wanafikiwa kwa wakati.

Naye Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa EBBAR, Dkt. Makuru Nyarobi amesema hadi kufikia sasa Mradi umewezesha jumla wananchi 26,610, upandaji miti 350,000 pamoja na kurejesha uoto wa asili wa hekta 38,000 za ardhi iliyoharibika katika Halmashauri zinazotekeleza mradi huo.

“Tunashukuru kwa mafanikio yaliyofikiwa hadi sasa ambayo yamewezesha wananchi kupata shughuli wezeshi za kujiongezea kipato.Tumepanga kuongeza wigo wa utekelezaji wa mradi katika maeneo mengine nchini” amesema Dkt. Nyarobi.

Kikao hicho cha kufunga Mradi wa EBBAR kimehudhuriwa na wizara mbalimbali za kisekta ikiwemo Ofisi ya Makamu wa Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar, Wizara ya Maji, Wizara ya kilimo, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na wadau wa maendeleo ikiwepo UNEP. 

Mradi wa EBARR unasimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais ulianza kutekelezwa mwaka 2019 katika Wilaya ya Simanjiro (Manyara), Mpwapwa (Dodoma), Kishapu (Shinyanga), Mvomero (Morogoro) na Kaskazini ‘A’ Unguja (Zanzibar) chini ya ufadhili wa Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) chini ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP).

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Mazingira Umoja wa Mataifa nchini (UNEP), Bi. Clara Makenya (Upande wa kulia) akizungumza jambo wakati wa kikao cha kufunga shughuli za utekelezaji wa Mradi wa kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBBAR), kilichofanyika Disemba 15,2025 Jijini Dodoma.

Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) Dkt. Makuru Nyarobi akizungumza wakati wa kikao cha kufunga shuguli za utekelezaji wa mradi huo, kilichofanyika Disemba 15,2025 Jijini Dodoma.

Washiriki wakiwa katika picha ya pamoja baada ya ufunguzi wa kikao cha kufunga shughuli za utekelezaji wa Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) kilichofanyika Desemba 15,2025

Post a Comment

0 Comments