Na.Masoud Juma Wizara ya Afya Zanzibar.
Wizara ya Afya Zanzibar imepokea msaada wa vifaa tiba kutoka shirika la Amref Health Afirca wenye lengo la kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma bora za Afya ya Mama na Mtoto Zanzibar.
Akizungumza baada ya makabidhiano ya vifaa hivyo yaliyofanyika Wizara ya Afya Zanzibar Mnazimmoja Mchango huu mkubwa ni muendelezo wa sehemu ya programu yake “Uzazi ni Maisha” inayolenga kuimarisha huduma za uzazi salama na kuboresha afya ya mama na mtoto Zanzibar.
Katibu Mkuu Dkt Mgereza Mzee Miraji amesema shirika la Amref ni miongoni mwa mashirika ambayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa yakiisaidia Wizara ya Afya katika kuimarisha utoaji wa huduma bora za Afya katika Hospitali pamoja na Vituo vya Afya na kupunguza baadhi ya matatizo yanayozorotesha utoaji wa huduma hizo.
Amesema miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana kutokana na misaada inyotolewa na shirika hilo ni kuongezeka kwa huduma za uchunguzi wa maradhi mbalimbali katika jamii jambo linalosaidia Serikali kupitia Wizara ya Afya kutambua maradhi ambayo yanahitajika kupewa kipaumbele ili kuzuia madhara yake kwa jamii.
Aidha amesema mbali na kupokea msaada huo Wizara ya Afya ya pamoja na Amref zimetiliana saini mkataba wa ujenzi wa Taasisi ya saratani jambo litakaloisaidia serikali kufikia hatua ya utoaji wa matibabu ya kudumu kwa wagonjwa wa saratani ndani ya nchi.
Aidha ameipongeza idara ya tiba ya Wizara ya Afya kuendelea kushirikiana na Amref kwa lengo la kuisaidia Wizara kuendelea kupata misaada ya vifaa mbalimbali vyenye lengo la kuongeza nguvu katika utoaji wa huduma za matibabu stahiki kwa jamii.
Mkurugenzi mkaazi wa Shirika la Amref Tanzania Dkt Florence Temu amesema ili kufikia malengo ya utoaji wa vifaa tiba hivyo ni vyema kwa watumiaji wakawa na uelewa wa kutosha pamoja na kuendelea kuihamasisha jamii kutumia vituo vya AFya na Hospitali zilizopo nchini ili kunufaika na misaada hiyo.
Amefahamisha kuwa Serikali imeonesha dhamira ya dhati katika kuimairsha huduma kwa Afya ya Mama na mtoto jambo linalotoa nafasi kwa shirikia hilo kuendelea kuimarisha mashirikiano katia sekta hiyo ili kuendelea kuisaidia Serikali kufikia malengo yake.
Nae Meneja miradi ya Afya ya Uzazi, Mama na mtoto pamoja na Vijana kutoka Amref Dkt Sarafina Mkuwa amesema vifaa hivyo vilivyokabidhiwa ni matokeo ya programu ya uzazi ni maisha ambayo ilichukua nafasi kubwa katika kuhamasisha jamii kutoa michango ya kusaidia huduma za mama na mtoto hasa wakati anapojifungua.
Amesema Programu hiyo Imefanikiwa kusaidia Hospitali 28 pamoja na Vituo Vya Afya mbalimbali vya Zanzibar vyenye idadi kubwa ya wazazi ambao huvitumia kwa kujifungulia ili kutoa wepesi wa utoaji wa huduma hizo na kusaidia kupunguza madhara ikiwemo vifo vya mama na mtoto.
Jumla ya shilingi Milioni Mia Mbili Arubaini na Tano zimetumika kununulia vifaa hivyo ikiwemo vitanda vya kujingulia, mashine za kusaidia kupumua kwa watu wazima na watoto na vifaa vyengine mbalimbali vinavyowasaidia mama kabla na baada ya kujifungua ikiwa ni sehemu ya juhudi za wadau mbalimbali katika kuhakikisha sekta ya Afya inaendelea kuimarika.
Kampeni ya Uzazi ni Maisha Initiative inaendelea kuwa chachu ya kuimarisha uwezo wa vituo vya kutolea huduma za afya Zanzibar kupitia upatikanaji wa vifaa tiba na mahitaji muhimu ya uzazi salama, hivyo kuboresha afya ya mama na mtoto visiwani.
MWISHO.
0 Comments