Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango
amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu wa Vietnam Mhe. Ho Duc
Phoc, mazungumzo yaliyofanyika kando ya Mkutano wa Nne wa Kimataifa kuhusu
Ufadhili wa Maendeleo (FfD4) unaofanyika Jijini Sevilla nchini Hispania.
Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais amesema Serikali ya Tanzania inathamini ushirikiano ulipo baina yake na Vietnam ambao umedumu kwa miaka 60 hivi sasa. Amesema Vietnam ni kati ya nchi za kwanza zilizofungua ubalozi mapema zaidi mara baada ya uhuru na kushirikiana na Tanzania kupitia Serikali, Chama Cha Mapinduzi na Wananchi.
Amesema Serikali ya Tanzania itaendeleza ushirikiano mzuri uliopo na Vietnam ikiwemo kuunga mkono kwenye masuala yenye maslahi ya pamoja katika majukwaa ya kimataifa.
Makamu wa Rais amesema ushirikiano uliopo baina ya Tanznia na Vietnam unapswa kuongezwa zaidi katika uwekezaji, kilimo, biashara masuala ya ulinzi na kushirikiana pia katika masuala ya Kikanda na Kimataifa.
Ameishukuru Serikali ya Vietnam kwa kuridhia soko la bidhaa mbalimbali za Tanzania kama vile Korosho na bidhaa za misitu.
Makamu wa Rais ameipongeza Vietnam kwa kuandaa Tume ya Kwanza ya Ushirikiano ya Pamoja (JPC) mwaka 2014 na kuihakikishia kwamba Tanzania itaandaa Tume ya Pili ya Pamoja ya Ushirikiano mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Ameikaribisha Vietnam kuchangamkia fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania kama vile kilimo, viwanda vya nguo pamoja na viwanda vingine vya uzalishaji.
Makamu wa Rais amesema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na inatatua changamoto zote zinazojitokeza katika uwekezaji kupitia majukwaa mbalimbali ya utoaji maoni yaliyoandaliwa. Amesema Serikali ipo tayari kushirikiana Kampuni ya Vietnam ya Viettel inayomiliki Mtandao wa Simu wa Halotel kuendelea kufikisha huduma bora ya mtandao ikiwemo 5G.
Kwa upande wake Naibu Waziri Mkuu wa Vietnam Mhe. Ho Duc Phoc amesema Tanzania na Vietnam ameishukuru Tanzania kwa kuendelea kuiunga mkono Vietnam katika majukwaa ya Kimataifa na hivyo kudumisha ushirikiano mzuri uliopo.
Amesema ushirikiano wa kiuchumi unaendelea kuimarika ambapo Tanzania inatumia soko la Vietnam kuuza Korosho na bidhaa za misitu na kila mwaka mauzo ya biashara hizo hufikia dola milioni 150.
Amesema uchumi wa Mataifa hayo mawili unaendelea kutegemeana kwa kuwa Vietnam inazalisha bidhaa ambazo zinauzwa nchini Tanzania ikiwemo mavazi na chakula.
Ameongeza
kwamba ni vema kuendelea kuimarisha ushirikiano zaidi kwa kuwa bado yapo maeneo
ambayo yanaweza kuwekezwa zaidi kupitia mashirika mbalimbali ya kibiashara na
uwekezaji ya Vietnam.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Nchi anayeshughulikia Maendeleo wa Denmark Mhe. Elsebeth Søndergaard Krone, mazungumzo yaliyolenga kuimarisha zaidi ushirikiano wa kimaendeleo baina ya Tanzania na Denmark.
Makamu wa Rais ameishukuru Denmark kwa mchango iliyotoa katika maendeleo ya Tanzania katika sekta mbalimbali za uchumi ambazo zimebadili maisha ya watanzania ikiwemo miundombinu, sekta ya fedha, afya, maji na mengineyo.
Mazungumzo hayo yamesisitiza ushirikiano wa kimkakati zaidi katika biashara na uwekezaji na sekta zingine zenye manufaa kwa pande zote mbili ikiwemo nishati, mazingira, kilimo janja, miundombinu na kuiwezesha sekta binafsi.
Halikadhalika, Makamu wa Rais ameshiriki Mkutano wa pembezoni wa Nchi Zinazoendelea (LDCs) ulioongozwa na Waziri Mkuu wa Nepal Mhe. Kadga Sharma Oil na kuhudhuriwa na mataifa rafiki yaliyoendelea. Mkutano huo umejadili tathimini ya utekelezaji wa azimio la Mkutano wa Tano wa Umoja wa Mataifa wa Nchi Zinazoendelea uliofanyika Doha nchini Qatar mwaka 2023.
Aidha Mkutano huo umelenga kupanga mikakati katika kukabiliana na changamoto zilizojitokeza tangu azimio la Doha hususani masuala ya ufadhili pamoja na kuweka msisitizo katika kuongeza jitihada za kukusanya mapato ya ndani ili kufikia lengo la asilimia 13 ya pato la Taifa.
Imetolewa na Ofisi ya
Makamu wa Rais 01 Julai 2025 Sevilla –
Uhispania.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Waziri Mkuu wa Vietnam Mhe. Ho Duc Phoc pamoja na ujumbe waliofuatana nao mara baada ya mazungumzo yaliyofanyika kando ya Mkutano wa Nne wa Kimataifa kuhusu Ufadhili wa Maendeleo (FfD4) unaofanyika Jijini Sevilla nchini Hispania.
No comments:
Post a Comment