MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amesema azma ya serikali ya awamu ya nane ni kuendelea kuzitatua changamoto mbali mbali zinazoikabili sekta ya elimu hapa nchini.
Ameyasema hayo alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa dakhalia ya wanawake inayojengwa katika skuli ya sekondari ya Fidel Castro, iliyopo Chake Chake kisiwani Pemba.
Amesema sekta ya elimu ndio kipaumbele cha serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, hasa ikizingatiwa kwamba uzalishaji wa wataalamu wazalendo waliobobea kwenye fani mbalimbali ndio watakaotatua changamoto za maendeleo ya Zanzibar.
Mhe. Hemed ameeleza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa dakhalia hiyo kutatoa nafasi kwa wanafunzi kusoma katika mazingira mazuri na yenye utulivu yatakayochangia kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu kwenye mitihani ya taifa.
Makamu wa Pili wa Rais amebainisha kuwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuweka mazingira bora na wezeshi kwenye elimu yatakayosaidia walimu na wanafunzi wanasoma na kufundisha kulingana na kiwango na hadhi ya elimu ulimwenguni.
Amewataka wanafunzi kuzidisha juhudi katika masomo yao ili kuendelea kufanya vizuri katika mitihani yao ya taifa, hatua ambayo itatengenezea mazingira mazuri ya maisha yao.
Akikagua ujenzi wa madarasa 16 yanayojengwa katika skuli ya msingi Mbuzini, Mhe. Hemed amesema ujenzi wa madarasa hayo utapunguza changamoto ya uhaba wa madarasa katika skuli hiyo sambamba na kupunguza msongamano wa wananfunzi madarasani ambapo kila darasa litakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 45.
Amefahamisha kuwa serikali itaendelea kuwawekea mazingira bora waalimu ikiwa ni pamoja na kuwaboresha maslahi na stahiki zao kwa kadiri bajeti itakavyoruhu ili kuwapa ari na hamasa ya kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa zaidi.
Ametoa agizo kwa mkandarasi anaejenga madarasa hayo kampuni ya Scenic Consultancy Ltd. kuhakikisha anamaliza ujenzi huo kwenye muda wa makubaliano, vyenginevyo utaratibu wa kisheria utachukua nafasi yake.
Kwa upande wake Ofisa Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mohammed Nassor Salim, amesema ujenzi wa dakhalia hiyo uatapunguza changamoto ya uhaba wa dakhalia hasa wanafunzi wasichana wanaosoma skulini hapo.
Amesema thamani zote kwa ajili ya dakhali hiyo tayari zimeshanunuliwa na zinatarajiwa kufungwa mara baada ya kukamilika kwa ujenzi.
Salim amewasilisha salamu za wanafunzi wa skuli ya sekondari ya Fidel Castro, ambao wameonesha kuridhishwa na miundombinu ya elimu iliyoimarishwa kwa ngazi zote na kumuahidi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi kuwa watasoma kwa juhudi.
Mshauri elekezi anaesimamia ujenzi wa mradi wa dakhalia wa Fidel Castro na madarasa ya skuli ya Mbuzini, Mhandisi Asya Massoud kutoka wakala wa Majengo Zanzibar (ZBA), alisema miradi hiyo kwa kila mmoja umegarimu shilingi bilioni 1.5, ambayo inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka huu.
Katika ziara hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitembeela na kukagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba za madaktari zinazojengwa katika hospitali ya Vitongoji, ambapo alionesha kuridhishwa na hatua iliyofikia ujenzi huo.
Amewataka wakandarasi kukamilisha mradi huo ndani ya muda uliopangwa ili kutoa fursa kwa madaktari kuhamia katika nyumba hizo jambo litarahisisha upatikanaji wa hudua muda wote hospitalini hapo.
Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
Tarehe 02.07.2025
No comments:
Post a Comment