Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita amewataka Wakandarasi wa Kampuni Skyway Construction kuongeza bidii katika ujenzi wa Ofisi ya Shirika la Magazeti ya Serikali Zanzibar ili iweze kukamilika kwa muda uliopangwa.
Ameyasema hayo wakati alipofanya ziara ya kukaguwa maendeleo ya Ujenzi wa Mradi wa Ofisi ya Shirika la Magazeti ya Serikali huko Tunguu Wilaya ya Kati.
Aidha amewataka wakandarasi hao, kufuata makubaliano yaliomo katika Mkataba, ikiwemo kujenga kwa ufanisi na kuzingatia viwango vinavyokubalika.
Amesema, Ujenzi wa Jengo hilo, umezingatia Watu wenye mahitaji Maalumu ili waweze kufika na kupata huduma kwa urahisi.
Hata hivyo Waziri Tabia amemuagiza Muhariri Mtendaji wa Shirika la Magazeti ya Serikali Zanzibar Ali Haji Mwadini, kuangalia maslahi ya Wafanya kazi ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi jambo ambalo litaimarisha utendaji wa Shirika hilo.
Sambamba na hayo ametoa wito kwa Wananchi kutoa mashirikiano kwa Wakandarasi ili kuondosha vikwazo vinavyoweza kujitokeza.
Kwa Upande wake, Muhariri Mtendaji wa Shirika hilo, Ali Haji Mwadini amesema kukamilika kwa ujenzi huo kutatoa fursa mbalimbali ikiwemo kuongeza mapato na kujiendesha wenyewe .
Nae Muhandisi kutoka Kampuni ya Skyway Construction Abubakar Khamis Shaaban amesema ujenzi huo, unaendelea vizuri licha ya kukabiliwa na changamoto ndogo ndogo ikiwemo kuwepo kwa Mwamba sehemu ya Uchimbaji.
Ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Shirika la Magazeti ya Serikali Zanzibar, unaojengwa na Kampuni ya Skyway Construction, umefikia asilimia 51 na unatarajiwa kukamilika ifikapo September mwaka huu.
No comments:
Post a Comment