Habari za Punde

Hotuba ya Waziri wa Afya katika maadhimisho ya siku ya Malaria duniani


Hutuba ya Mhe Waziri wa Afya Nd. Mahmoud Thabit Kombo kwa Waandishi wa Habari Katika Maadhimisho ya Siku ya Malaria Dunia
Zanzibar, 22/04/2016

Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya
Katibu Mkuu Wizara ya Afya
Naibu Katibu Mkuu Wizara
Wakurugenzi wa Idara mbali mbali za Wizara ya Afya
Nd. Waandishi wa habari pamoja na wadau wengine wa Afya; Assalam Alaikum

Kabla ya yote napenda kwa kuanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia afya njema na ni Imani yangu kuwa sote ni wazima. Aidha nachukua fursa hii kuwashukuru waandishi wote mliofika hapa kuungana nasi katika harakati za kumaliza ugonjwa wa malaria Zanzibar. Karibuni sana.

Ndugu Waandishi,
Tukiwa tunaelekea kwenye maadhimisho ya siku ya malaria duniani ambapo kilele cha maadhimisho haya hufanyika kila ifikapo terehe 25 Aprili, Zanzibar tunaadhimisha siku hii kwa kujivunia mafanikio makubwa tuliyoyapata katika kupambana na ugonjwa wa malaria. Takwimu za Wizara ya Afya zinaonesha kuwa tokea mwaka 2007, tatizo la malaria limepungua  kwa kiwango cha chini ya asilimia moja. Aidha, vifo vinavyotokana na malaria pia vimepungua. Mwaka jana (2015) watu ….walifariki kwa malaria. Mwaka huu hadi mwezi huu wanne hakuna mtu aliefariki kwa ugonjwa huu. Haya ni mafanikio makubwa ambayo si rahisi kuyapata nchi nyengine ya Afrika.

Lengo kuu la maadhimisho haya ni kuwakumbusha wananchi katika ngazi zote kuendelea kupambana na malaria kwa kufuata maagizo ya wataalam kwani ugonjwa wa malaria bado upo Zanzibar. Napenda kuwakumbusha wananchi kwamba ugonjwa huu unashamiri zaidi mara tu baada ya mvua za masika kumalizika kutokana na kutengenezwa mazalio ya mbu katika maeneo yote yanayotuwama maji ya mvua. Mtakumbuka kua mwaka huu tumepata mvua kubwa na sehemu nyingi maji yametuwama. Kutokana na hali hii uwezekano wa kuongezeka mazalio ni mkubwa na hatimae ugonjwa kuenea sehemu zote.


Nd. Waandishi,

Katika maadhimisho ya mwaka huu wa 2016, Wizara ya Afya imepanga kuendelea kutoa taaluma kwa jamii juu ya njia mbali mbali za kijikinga na malaria pamoja na maradhi mengine ya kuambukiza. Aidha ifikapo tarehe 24/04/2016 Wizara Afya imepanga kufanya matembezi ya hiari yatakayowajumuisha viongozi wa Wizara ya Afya,Viongozi wa Mikoa na Wilaya, Vikundi mbali mbali vya mazoezi pamoja na viongozi wa Taasisi za Chama na Serikali. Matembezi haya yanakwenda sambamba na kauli mbiu ya maadhimisho hayo ya malaria duniani isemayo ‘Maliza Malaria Kabisa’.

Ndugu Waandishi kazi ya kumaliza malaria si wajibu wa Wizara ya Afya peke yake, ila ni wajibu wetu sote kwa kila mtu na nafasi yake. Kwa mantiki hiyo nachukua nafasi hii kukualikeni nyote mlokuepo na waliokua hawapo nasi kwa muda huu kujumuika nasi katika maadhimisho hayo muhimu siku ya Jumapili.

Matembezi haya ya hiari yanategemewa kuanzia……………. Mnamo saa 12 asubuhi na kuishia katika kiwanja cha mpira cha Kikosi cha Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM) Maisara ambapo mgeni rasmi atakua kiongozi wetu Makamo wa Raisi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi. Mhe, Balozi atawahutubia washirika wa matembezi hayo kwa kuwapa nasaha washiriki na wananchi kwa jumla juu ya ugonjwa huu na hatua zilizofikiwa za kumaliza ugonjwa Unguja na Pemba.


Ndugu Waandishi
Kwa kuwa leo nimepata fursa ya kukutana nanyi, sina budi kuwajuilisha kwa mukhtasari kuhusu ugonjwa huu ikiwa tumo kwenye maadhimisho haya ili muwajuilisha wananchi. Wizara ya Afya inasisitiza kua malaria bado ipo Zanzibar na katika mikoa yote na zaidi ni Wilaya ya Magharibi A na B, Wilaya ya Kati na Micheweni Pemba.. Kwa maelezo hayo Wizara inawaka wananchi kwa ujumla kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga  ikiwemo kutumia vyandarua vilivyotiwa dawa, kusafisha mazingira tunayoishi ili kuondosha mazalio, kufunika maji ndani ya mahodhi, mapipa na sehemu nyengine ili kumnyima nafasi ya kuzaliana adui mbu waenezao malaria. Aidha, tunatoa wito kwamba mtu yeyote ndani ya familia anapojihisi homa aende kituo cha afya cha karibu ili kuchunguzwa kama ana homa ya malaria. Usitumie dawa ya malaria kutokana na ishara na dalili za malaria – chunguza damu.

Ndugu Waandishi
Ni vizuri kuwajuilisha kuwa katika mkakati huu wa kumaliza malaria Zanzibar, tunakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo maambukizi ya malaria kutoka kwa wasafiri wanaotoka nchi za jirani pamoja na Watanzania kutoka mikoa mbali mbali wanaokuja kuishi au kutembelea Zanzibar. Takwimu za Wizara ya Afya za mwaka 2015 zinaonyesha kua asilima 60 ya wagonjwa walioripotiwa kuwa na malaria walikua na historia ya kusafiri nje ya Zanzibar. 

Ndugu waandishi – kali mbiu niliyoitaja awali inaisisitiza jamii umuhimu wa kufuata maelekezo ya wataalamu pamoja na kutumia  kinga kama vile  chandarua kilichotiwa dawa kila siku wakati wa usiku na zaidi mtu anapotembelea Nchi, Mkoa, Wilaya au kijiji ambapo ugonjwa wa malaria ni tatizo kubwa. Wizara ya Afya bado itaendelea kutoa elimu ya Afya juu ya kinga ya malaria kupitia redio, television pamoja na matangazo katika viwanja vya ndege na bandarini ili kuwapata tahadhari wasafiri.

Ndugu waandishi ni Imani yangu kuwa taarifa hii mtaifikisha kwa jamii ili kutimiza wajibu wenu ulivyo wa kuwahabarisha wananchi taarifa sahihi kuhusu ugonjwa huu. Aidha, napenda kuwakumbusha tena kuuungana nasi siku ya Jumapili na kuweza kupata maoni kutoka kwa washiriki wa matembezi hayo juu ya juhudi za Serikali katika kuondosha ugonjwa huu.

Nawatakia kazi njema na ahsanteni kwa kunisikiliza.         


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.