Habari za Punde

Waziri Mhe.Tabia Azungumza na Kamati Maalumu ya Kuandia Kitabu cha Miaka 60 ya Mwenge wa Uhuru


Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid akizungumza na Kamati Maalumu ya kuandika Kitabu cha miaka 60 ya Mwenge wa uhuru wakati ilipofika Ofisini kwake Migombani kujitambulisha

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita ameitaka Kamati Maalumu ya kuandika Kitabu cha miaka 60 ya Mwenge wa uhuru, kuwajibika ipasavyo ili kitabu hicho kiweze kukamilika kwa muda uliopangwa.

Amesema hayo, wakati kamati hiyo, ilipofika kujitambulisha huko Ofisini kwake Migombani Wilaya ya Mjini.

Aidha ameitaka Kamati hiyo, kuhakikisha wanakutana na viongozi mbali mbali mashuhurI ili kupata taarifa za usahihi, zinazohusiana na Mwenge wa Uhuru.

Aidha amesema ni vyema kukutana na Viongozi Wastaafu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) ambao walishiriki katika kukimbiza mbio za Mwenge wa Uhuru ili kupata historia ya miaka ya nyuma.

Hata hivyo Waziri Tabia, ameitaka Kamati hiyo isimuache mtu yeyote ambae kwa njia moja au nyengine ameguswa na historia ya Mwenge wa Uhuru kwa kipindi cha miaka 60.

Nae Mwenyekiti wa Kamati ya utayarishaji wa Kitabu cha Miaka 60 ya Mwenge wa Uhuru, Waziri mstaafu wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amemshukuru Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulidi Mwita kwa kuwapa miongozo na ushauri jambo ambao litawawezesha kupata maoni kwa urahisi.

Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati hiyo, ambae pia ni Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Vijana, Shaib Ibrahim Mohamed amesema Kitabu hicho, kitasaidia kuhifadhi kumbukumbu na kujenga uelewa juu ya chimbuko na picha halisi ya mchango wa harakati za Mwenge wa Uhuru Tanzania.

“Kuwaelewesha vizazi vya sasa na vijavyo juu ya Mwenge wa uhuru, historia yake, Muasisi wake, chanzo, sababu na mabadiliko katika harakati za Maendeleo’’ alisema Mjumbe huyo.

Amesema wakati wa Serikali ya Mfumo wa Chama kimoja, Mwenge wa Uhuru ulikuwa ukiratibiwa na Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi ambapo tokea kuanza kwa mfumo wa vyama Vingi umekabidhiwa Serikali kuendesha harakati hizo.

Sambamaba na hayo Mjumbe Shaib, amewataka Wadau mbali mbali ikiwemo Waasisi wa Chama cha Mapinduzi na Viongozi Wastaafu kutoa mashirikiano ya kutosha ili kufanikisha zoezi hilo.

Kitabu cha Miaka 60 ya Mwenge wa Uhuru, kinatayarishwa na Kamati Maalumu, inayojumuisha Wizara mbili ambapo ni Wizara ya Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu na Wizara ya Habari, Vijana Utamaduni na Michezo na kinatarajiwa kuzinduliwa rasmi Oktoba mwaka huu.

 

Imetolewa na Kitengo cha Habari,

WHVUM.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.